Madiwani wadai kondomu zimeadimika Mbeya

Muktasari:
- Baraza la madiwani halmashauri ya Jiji la Mbeya limehoji kukosekana kwa kondomu kwa takribani miezi minne katika kumbi za starehe, baa na kwenye vilabu vya pombe jambo lililoelezwa kuwa linaleta hofu ya kuongezeka kwa maambukizi ya Ukimwi.
Mbeya. Baraza la madiwani halmashauri ya Jiji la Mbeya limehoji kukosekana kwa kondomu kwa takribani miezi minne katika kumbi za starehe, baa na kwenye vilabu vya pombe jambo lililoelezwa kuwa linaleta hofu ya kuongezeka kwa maambukizi ya Ukimwi.
Aliyeibua hoja hiyo leo Ijumaa Mei 7, 2021 ni diwani wa Mbalizi Road, Adam Hussein kwenye kikao cha baraza hilo kilichoketi kujadili taarifa ya robo mwaka na kupitia fedha zilizopokelewa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Hoja hiyo iliungwa mkono na baraza la madiwani kwamba katika maeneo hayo sehemu ambazo zilikuwa zikitumika kuweka Condom zipo tupu.
"Kwa sasa tupo katika kukabiliana na maambukizi ya Ukimwi lakini kwenye vituo hakuna Condom, sasa tunazuia nini? Tunaomba kamati ya kuthibiti Ukimwi Jiji ipite kujiridhisha ili kunusuru wapiga kura wetu hali sio nzuri kwenye kata zetu,” amesema Hussein.
Mganga wa Jiji la Mbeya, Dk Jonas Lulandala amesema ni kweli Februari na Machi, 2021 kulikuwa na changamoto hiyo na tayari wamewasiliana na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) akibainisha kuwa kwa mwezi Aprili zimesambazwa katika maeneo mbalimbali mjini humo.