Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Milioni 100 zalipwa kwa waliopisha mradi wa gesi nadra ya helium

Mitambo ya utafiti uliopo katika kisima cha gesi ya hellium cha Itumbula wilayani Momba mkoani Songwe.

Muktasari:

  • Wakazi wa Wilaya ya Momba mkoani Songwe, waliopisha mradi wa gesi ya helium walipwa fidia Sh100 milioni huku mradi ukiwa katika hatua za mwisho za kuanza uzalishaji wa gesi hiyo nadra duniani.

Songwe. Fidia ya zaidi ya Sh100 milioni imelipwa kwa wakazi wa vijiji vitano vya Wilaya ya Momba Mkoani Songwe ambao wamepisha Kampuni ya Helium One, inayojihusisha na utafiti na uchimbaji wa gesi ya helium nchini Tanzania.

Vijiji vya Itumbula, Lwatwe, Masanyinta, Mkonko na Muungano ndio eneo unapotekelezwa mradi huo ambao ulianza mwaka 2015 kwa kufanya utafiti wa gesi hiyo katika Bonde la Rukwa Kusini.

Mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20 katika maeneo hayo na kuongeza mapato yanayotokana na madini nchini.

Akizungumza leo Aprili 24, 2025 wakati wa ziara ya wataalam kutoka Wizara ya Madini pamoja na waandishi wa habari, msimamizi katika maeneo ya utafiti na uendelezaji wa mradi huo, Emmanuel Ghachocha, amesema kuwa fidia hiyo imelipwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Amesema mradi umefanikiwa kufanya shughuli zake za kitafiti ikiwamo utafiti kwa njia ya mitetemo na uchimbaji wa visima vya utafiti.

Amesema kuanzia mwaka 2021 mpaka 2025 Kampuni ya Helium One  imekwisha chimba visima vinne, ambapo mafanikio makubwa yalionekana kwenye visima vya Itumbula West 1 na Tai 3 vilivyogundulika kuwa na mkusanyiko mkubwa wa gesi ya helium.

Amesema baada ya kufanyika majaribio (Extended Well Testing) Kisima cha Itambula 1 ilionesha kuwa na uwezo wa kuzalisha Gesi hiyo kwa kiwango cha asilimia 7.9 na kuwa utafiti wa kina uliofuata pia ulionesha uwezo wa kuzalisha gesi ya Helium kwa  kiwango cha asilimia 5.5 juu ya ardhi.

“Mradi huu unatarajiwa kudumu kwa takribani kipindi cha zaidi ya miaka 20 ya uendelezaji na uzalishaji wa gesi hiyo,” amesema Ghachocha.

Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Songwe, Mjiolojia Chone Malembo, amesema Songwe ina nafasi kubwa ya kuwa kinara wa uzalishaji wa gesi ya helium nchini, jambo ambalo litaongeza mchango wa mkoa huo katika Pato la Taifa kupitia sekta ya madini.

Malembo amebainisha kuwa, katika mwaka 2023/2024, mkoa ulikusanya zaidi ya Sh37 bilioni kutokana na shughuli za madini na kwa robo ya tatu ya mwaka 2024/2025 ukikusanya zaidi ya Sh36 bilioni na matarajio ni kufikia Sh40 bilioni ifikapo mwisho wa mwaka huu wa fedha.

Mjiolojia kutoka Wizara ya Madini, Venosa Ngowi, ameeleza kuwa, Tanzania imebarikiwa kuwa gesi ya helium katika maeneo mbali mbali ikiwemo katika Bonde la Ziwa Rukwa na Bonde la Eyasi Wembere.

Ngowi amefafanua kuwa, gesi hiyo ina matumizi muhimu katika sekta mbalimbali ikiwemo afya (hasa kwenye MRI Scanner), teknolojia ya anga, utafiti wa sayansi ya angahewa, pamoja na usafiri wa anga kama vile roketi na vifaa vya ndege.

Mkazi wa Kijiji cha Itumbula, Mary Vicent  ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita na Kampuni ya Helium one kwa kukamilisha kulipa fidia kwa wananchi waliopisha mradi.

“Huu ni mradi wa kihistoria kwa eneo letu. Mbali na fidia, tunatarajia vijana wetu kupata ajira, na huduma za kijamii kama barabara na maji kuimarika kutokana na uwepo wa mradi,” amesema Mary.

Kwa sasa, nchi zinazoongoza kwa uzalishaji wa gesi ya helium duniani ni Marekani, Urusi, Qatar, Saudi Arabia na Algeria.