Mabaki ya mwili wa dereva wa lori la mafuta lililowaka moto Msamvu, yatambulika

Mabaki ya malori mawili yaliyogongana uso kwa uso na kuwaka moto eneo la Nane nane barabara ya Morogoro - Dar es Salaam na kusababisha Vifo vya watu watatu. Picha Hamida Shariff
Muktasari:
- Baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara mabaki ya miili ya waliofariki kwenye ajali ya malori yaliyowaka moto, mabaki ya mwili wa dereva wa lori la mafuta yametambulika, huku mabaki ya miili miwili yakiendelea kuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro.
Morogoro. Mganga Mkuu mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro, Dk Daniel Nkungu amesema mabaki ya mwili mmoja kati ya mitatu ya waliofariki kwenye ajali ya malori yaliyowaka moto Msamvu Morogoro, umetambuliwa.
Amesema kinachofanyika sasa ni ndugu kukamilisha taratibu za kipolisi ili waweze kukabidhiwa mwili wa mpendwa wao.
Akizungumza na Mwananchi Dk Nkungu amesema kuwa mabaki ya mwili uliotambuliwa na ndugu ni ya aliyekuwa dereva wa lori la mafuta Majaliwa Chunga (54) mkazi wa Ruaha mkoani Iringa, ambapo miili mingine iliyobaki imeendelea kuhifadhia katika hospitali hiyo.
"Miili iliyopatikana kwenye ajali ile ilikuwa kwenye hali mbaya kiasi cha kushindwa kutambulika kwa kuangalia kwa macho, kimsingi ni mabaki ya miili hivyo hospitali kwa kushirikiana na wenzetu wa Jeshi la Polisi ilibidi tuchukue sampuli na kuzipeleka kwa mkemia," amesema Dk Nkungu.
Amesema baada ya sampuli hizo kuchukuliwa watu watakaokwenda kutafuta miili ya ndugu zao waliokufa kwenye ajali hiyo, watalazimika kufuata utaratibu kwa kwenda kwanza Polisi ili kupata mwongozo wa namna ya kuitambua miili ya wapendwa wao.
"Sisi kama hospitali tutaendelea kuitunza miili hii kwa heshima na staha zote kama miili mingine mpaka hapo itakapotambuliwa na ndugu," amesema Dk Nkungu.
Amewashauri wananchi ambao wana wasiwasi na ndugu zao kuwepo kwenye ajali hiyo kufika katika kituo cha Polisi kikubwa cha mkoa wa Morogoro, ili wapewe utaratibu wa kutambua mabaki ya miili hiyo na kukabidhiwa.
Ajali hiyo iliyohusisha malori mawili moja likiwa la mafuta na lingine la mizigo ilitoa usiku wa kuamkia Machi 4,2025 eneo la Nanenane barabara ya Morogoro - Dar es Salaam baada ya malori hayo kugongana uso kwa uso kisha kuwaka moto.
Kwa mujibu wa kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Linus Mnyambwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori la mizigo lililokuwa likitokea Msamvu, ambaye hakuzingatia sheria za usalama barabarani kwa kutaka kulipita gari la mbele yake bila kuchukua tahadhari, hivyo kugongana uso Kwa uso na lori la mafuta.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye eneo la ajali Kamishna Mnyambwa aliwataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuzuia ajali zinazotokana na uzembe.