Magari yagongana Moro, wawili wafariki

Lori la mizigo na lori lililobeba Petrol na disel yakiteketea kwa moto baada ya kugongana uso kwa uso usiku wa kuamkia leo Machi 4, 2025 eneo la Nane Nane barabara ya Morogoro -Dar es Salaam. Picha Jackson John
Muktasari:
- Ajali hiyo imetokea usiku leo Machi 4, 2025 ambapo lori wa mafuta liligongana uso kwa uso na lori la mizigo kisha kuwaka moto na kusababisha vifo vya watu wawili.
Morogoro. Watu wawili wamefariki dunia papohapo katika ajali iliyohusisha malori mawili kugongana uso kwa uso na kuwaka moto eneo la Nanenane Barabara ya Morogoro-Dar es Salaam.
Ajali hiyo imetokea usiku wa saa 7 leo Jumanne, Machi 4, 2025 ambapo malori hayo mawili moja ni lori lenye tenki mbili zenye mafuta likiwa linatoka Dar es Salaam na lingine ni lori la mizigo likiwa linatoka Morogoro kwenda Dar es Salaam.

Mkaguzi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Faraja Pazzy amesema baada ya kufanikiwa kuzima moto huo kwenye lori la mizigo kulikuwa na watu wawili ambao walikuwa wameshafariki.
Amesema idadi kamili ya watu waliokuwemo kwenye lori la mafuta bado halijafahamika hadi kazi ya kuzima moto itakapomalizika.
"Kwa sasa vifo tulivyoviona ni vya watu wawili lakini idadi hii inaweza kuongezeka kwa kuwa lile lori la mafuta moto bado ni mkubwa na mfahamu lilikuwa na petroli na dizeli, hivyo tunaendelea na jitihada za kuudhibiti moto huu ili kujua kama kuna wengine waliokufa ama ni hawahawa wawili tu," amesema Pazzy.

Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Juma Ramadhan amesema lori mbili aina ya fuso zilikuwa zimeongozana zikitokea Msamvu kuelekea Nanenane zilipofika kwenye tuta yule wa mbele alifunga breki ghafla kwa ajili ya tuta, yule wa nyuma baada ya kuona mwenzake kafunga breki alijaribu kumkwepa ndiyo akagongana uso kwa uso na hilo lori la mafuta lililokuwa likitokea Dar es Salaam,” amesema Ramadhan.

Lori la mizigo na lori lililobeba Petrol na disel yakiteketea kwa moto baada ya kugongana uso kwa uso usiku wa kuamkia leo Machi 4, 2025 eneo la Nane Nane barabara ya Morogoro -Dar es Salaam. Picha Jackson John
Shuhuda huyo amesema baada ya malori hayo kugongana kilitokea kishindo kilichoambatana na mlipuko na hapo malori yote mawili yakaanza kuwaka moto.
Mwananchi inaendelea na jitihada za kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro kupata maelezo zaidi kuhusiana na ajali hiyo.
Endelea kufuatilia Mwananchi