Lori lenye shehena latumbukia Ziwa Victoria

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Nyakaliro wakiwa ndani ya boti wakienda eneo ambako lori lenye shehena ya mizigo lilipotumbukia. Picha na Daniel Makaka
Muktasari:
Lori lilibeba shehena ya mifuko ya saruji na bidhaa mbalimbali za dukani limetumbukia ndani ya Ziwa Victoria baada ya kuserereka kutoka ndani ya kivuko cha Mv Kome II kinachofanya safari zake kati ya Nyakaliro na Kisiwa cha Kome.
Buchosa. Lori lenye shehena ya mifuko ya saruji na bidhaa mbalimbali za dukani limetumbukia ndani ya Ziwa Victoria baada ya kuserereka kutoka ndani ya kivuko cha Mv Kome II kinachofanya safari zake kati ya Nyakaliro na Kisiwa cha Kome.
Tukio hilo limetokea leo Mei 2, 2023 muda mfupi baada ya lori hilo lililokuwa likitokea mjini Sengerema kwenda Kisiwa cha Kome kuingia ndani ya kivukoambapo kabla ya kutumbukia, liliserereka na kugonga kingo za mbele za kivuko hicho.
Meneja wa Vivuko Kanda ya Ziwa, Vitalis Bakuri amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba namba za usajili wala mmiliki gari bado hazijafahamika.
“Tunamshukuru Mungu hakuna maisha ya binadamu iliyopotea katika ajali hiyo,” amesema Bakuri
Amesema gari hilo liliingizwa salama ndani ya kivuko, kisha dereva ambaye pia hakumtaja jina alishuku kwa nia ya kuweka kigingi ndipo gari lilipoanza seleleka, kugonga kingo za mbele za Kivuko cha Mv Kome II na kutumbukia ziwani.
"Ajali hiyo haikuathiri na haitaathiri safari za kivuko kusafirisha abiria na mizigo,” amesema Bakuri
Diwani wa Kata ya Nyakaliro, Paul Kabugwe amesema hilo ni tukio la kwanza katika eneo hilo la gari kutumbukia ziwani huku akiwaomba madereva kuongeza umakini kulinda usalama wa abiria, mizigo na magari wakati wa kuingia na kutoka ndani ya kivuko.
Watumiaji wa vyombo vya usafirishaji kuongeza umakini kwa usalama wao, abiria na vyombo vyao pia imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga huku akimshukuru Mungu kwa kunusuru maisha ya watu katika ajali hiyo.