Mfalme Zumaridi akamatwa Mwanza

Muktasari:
- Hii ni mara ya tatu Zumaridi kuingia mgogoro na vyombo vya dola, ambapo kwa mara ya kwanza kanisa lake lilifungiwa mwaka 2019.
Mwanza. Diana Bundala, maarufu Mfalme Zumaridi anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kwa tuhuma za kugeuza makazi yake kuwa kanisa, kuendesha shughuli za kidini bila usajili na kuhubiri kwa sauti ya juu.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa jioni ya leo Alhamisi Mei 15, 2025 imesema Zumaridi ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Buguku, kata ya Buhongwa jijini Mwanza pia anahojiwa kuhusiana na taarifa inayoendelea kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, akiwaeleza watoto kuwa yeye ndiye Mungu wao.
"Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linapenda kutoa taarifa kuwa leo Mei 15, 2025 saa 4 asubuhi limemkamata na linaendelea kumuhoji Diana Edward Bundala ambaye pia hujitambulisha kwa jina la Mfalme Zumaridi ambaye ameyageuza makazi yake kuwa kanisa.
"Anatuhumiwa kuendesha shughuli za kidini bila usajili pamoja na kufanya mahubiri kwa waumini wake kwa sauti ya juu katika eneo hilo ambalo ni makazi ya watu na kusababisha usumbufu,"imeeleza taarifa hiyo.
Mutafungwa ameongeza kuwa, Zumaridi anahojiwa pia kuhusiana na taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii akionekana kwenye picha mjongeo akiwa na kundi la watoto wenye umri mdogo akiwaeleza kuwa yeye ndiye Mungu wao, ambaye ana uwezo wa kuwatenganisha na kifo.
"Uchunguzi kuhusiana na tukio hili unaendelea, Jeshi la Polisi katika uchunguzi huo litashirikiana na taasisi nyingine za Serikali, hivyo linawaomba wananchi wenye taarifa mbalimbali zinazoweza kusaidia uchunguzi wa tuhuma hizi wafikishe kwa Jeshi la Polisi,"amesema Mutafungwa.
Ameongeza kuwa uchunguzi utakapokamilika hatua za kisheria zinazostahili zitachukuliwa dhidi ya Zumaridi.
Hii ni mara ya tatu, Zumaridi kuingia mgogoro na Serikali pamoja na jeshi hilo ambapo Novemba 18, 2019 kanisa lake lilifungwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dk Philis Nyimbi kwa madai ya kuendesha ibada zinakinzana na sheria ya nchi, ikiwemo kutumia katiba ya kanisa lingine.
Pia Februari, 2022 Zumaridi alikamatwa na jeshi hilo kwa kosa la usafirishaji haramu wa binadamu 149 pamoja na tuhuma za kuwatumikisha watu hao ambao kati yao watoto walikuwa 24 wenye umri kati ya miaka minne hadi 17 kisha Machi, 2022 alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza yeye na wafuasi wake.
Ambapo alisomewa mashitaka matatu ya kuzuia maofisa wa Serikali kutekeleza majukumu yao, kufanya mkusanyiko usio na kibali na usafirishaji haramu wa binadamu lililokuwa likimkabili Mfalme Zumaridi peke yake. Hata hivyo, Desemba, 2022 Mahakama hiyo iliwaachia huru.