Mfalme Zumaridi afunguka magumu aliyopitia gerezani

Mhubiri, Diana Bundala maarufu Mfalme Zumaridi akizungumza na mwandishi wa Mwananchi muda mfupi baada ya kuwasili nyumbani kwake akitokea katika Gereza la Butimba alikokuwa anatumikia kifungo cha mwaka mmoja. Picha na Mgongo Kaitira
Mwanza. Mhubiri Diana Bundala amerejea uraiani baada ya kusota katika Gereza la Butimba jijini Mwanza alipokuwa akitumikia kifungo chake cha mwaka mmoja huku akifunguka magumu aliyopitia.
Diana maarufu kwa jina la Mfalme Zumaridi na waumini wake 83 walikamatwa Februari 26, 2022 nyumbani kwake Mtaa wa Buguku, Kata ya Buhongwa kisha kufunguliwa kesi tatu Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza.
Mhubiri huyo na wenzake walifunguliwa kesi zenye mashtaka tofauti ikiwamo ya kuzuia maofisa wa Serikali kutekeleza majukumu yao, usafirishaji haramu wa binadamu na kufanya kusanyiko lisilo na kibali.
Awali katika hukumu, Hakimu Mkazi Mfawidhi Monica Ndyekobora alisema kati ya washtakiwa tisa katika kesi ya kuzuia maofisa wa umma kutekeleza majukumu yao, wanane hawana hatia.
Hata hivyo, Zumaridi alikutwa na hatia kisha akahukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela alichotumikia kwa siku 30 kutokana na kukaa miezi 11 mahabusu.
Kuhusu kesi ya usafirishaji haramu wa binadamu, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) alimfutia mashtaka mhubiri huyo baada ya kudai hana nia ya kuendelea nayo, huku kesi nyingine wakionekana hawana hatia.
Jana akiwa na furaha, Zumaridi alipokewa na mamia ya waumini nyumbani kwake Mtaa wa Buguku akitokea gerezani baada ya kutumikia kifungo chake.
Akizungumza na waumini wake, Zumaridi aliishukuru Serikali kwa kuimarisha ulinzi dhidi yake wakati wote katika kesi zilizokuwa zinamkabili huku akiwapongeza waumini wake kwa kuwa wavumilivu.
“Nawapongeza waumini wangu kwa kukaa na mimi wakati wote, kuniletea mahitaji mbalimbali gerezani, wamepigwa na mvua na jua, lakini walikuwa wanakuja asubuhi hadi mwisho wa kesi hizi,” alisema Zumaridi.
“Nawapongeza kwa sababu hawajaniacha kwa kipindi chote, mwingine amevunjwa na kupata kilema cha kudumu yupo na bado anakiri kwamba mimi ni mtumishi wa Mungu.”
Maisha ya gerezani
“Sikuamini ningefunguliwa kesi za aina hii; maisha ya gerezani, kwangu ni mateso makubwa, tulikuwa tunanyanyaswa, wakati mwingine tunatumikishwa ilhali tuna majeraha yaliyotokana na kipigo wakati wa ukamataji,” alidai Zumaridi.
Huku akionyesha kusikitishwa na mapito yake, Zumaridi alimuomba Rais Samia Suluhu Hassan kufanya ufuatiliaji wa karibu kubaini vitendo vya kikatili vinavyoendelea magereza.
“Kule ndani kuna wanawake ambao wamefungwa wakiwa na watoto ambao sasahivi wamekuwa na umri wa kwenda shule lakini hawajaenda. Naomba wawasaidie watoto wale wapate haki ya elimu,” alidai Zumaridi.
Pia, alisema miongoni mwa mambo yaliyomshtua ni kuwa na tuhuma za usafirishaji wa binadamu anazodai hakuwa anatambua maana ya tuhuma hizo hadi alipokamatwa na kuishi mahabusu zaidi ya miezi 11.
“Sijawahi kusafirisha binadamu wala nilikuwa sijui maana yake hadi pale nilipofungwa gerezani, askari wa magereza nilipowauliza ndiyo wakaniambia maana yake ambayo kiuhalisia watu niliyotuhumiwa kuwasafirisha nilikuwa nawasaidia kuwasomesha,” alisema Zumaridi.
“Sitaki kusema ibada zangu zitakuwaje, lakini niseme tu kuwa Watanzania wamtegemee Zumaridi wa tofauti na mpya. Hakuna tukio litakalomkuta mtumishi wa Mungu kila jambo lina kusudi lake, mpaka sasa nina alama sikuwa nayo nilikuwa napigiwa waya na vyuma hadi leo nina alama,” alisema.
Hata hivyo, aliishauri Serikali kwa kuzingatia muda wa uendeshaji wa mashauri ikiwamo kukamilisha upelelezi wa kesi kwa wakati ili kutoa fursa kwa washtakiwa kurejea uraiani na kuendeleza shughuli zao za uzalishaji.
“Kwa kipindi chote nilichokaa gerezani sikuwa nafanya uzalishaji wowote, hata watoto niliyokuwa nawasomesha walikwama kiasi kwamba kama upelelezi wa kesi zangu ungekamilika ndani ya miezi mitatu ningerejea uraiani mapema na mambo yangu yasingekwama,” alisema Zumaridi.
Alisema hana ushindani na Serikali bali ushindani wa kiimani huku akiahidi kuendeleza shughuli za ibada kistaarabu bila kumkwaza mtu yeyote.
Zumaridi alisema jopo la mawakili wake, Erick Mutta, Steven Kitale, Amri Linus na Merckzedeck Gunda wanaendelea kufuatilia mali zilizochukuliwa nyumbani kwake ikiwamo kadi za benki, hati za nyumba na simu zake.