Lilian Lema ataja mambo matatu yanayokwamisha uzazi wa mpango

Mtengenezaji wa maudhui mtandaoni, Lilian Lema.
Muktasari:
- Mtengenezaji maudhui mtandaoni, Lilian Lema amechangia mjadala wa Mwananchi Space ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja Shirika la Marie Stopes Tanzania (MST), amebainisha mambo matatu yanayorudisha nyuma utekelezaji wa uzazi wa mpango.
Dar es Salaam. Mtengenezaji wa maudhui mtandaoni, Lilian Lema ametaja sababu tatu za kwanini jamii hazipendi kutumia uzazi wa mpango ikiwemo ukosefu wa taarifa sahihi.
Pili, vijana wengi wamejawa na uoga kwenda kwenye vituo vya afya na gharama za kuweka uzazi wa mpango wengi wakifikiria uamuzi wa kuangalia njia nyingine kama kumeza P2 ambazo zinapatikana kirahisi.
Njia hizo amebainisha leo Jumatatu Septemba 25, 2023 katika mjadala wa Mwananchi Space ulioandaliwa na Mwananchi Communications Ltd (MCL) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja Shirika la Marie Stopes Tanzania (MST) wenye mada ya ‘uzazi wa mpango ni hatua katika kufikia lengo kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi?
“Taarifa pitofu zinasambaa na zina nguvu kuliko taarifa sahihi na kuna wanaoamini ukitumia uzazi wa mpango kama kitanzi au kijiti kinaweza kupotelea mwilini au wakitumia kinga au vizuizi vinawasha,” amesema
Lilian amepandekeza ili kuhamasisha jamii kwa kutoa taarifa sahihi kupitia mitandao ya kijamii kwani vijana wengi wanaanza michezo hiyo bado wangali wadogo.
“Wanafanya katika njia ambayo si salama, tukijitahidi kusambaza taarifa sahihi na kutumia watu maarufu itasaidia kuelimisha kizazi hiki,” amesema
Awali, akichangia katika mjadala huo, William Huruma ameshauri Watanzania kupewa elimu ya afya ya uzazi huku akibainisha baadhi yao hawana na wakishaipata basi waanze kutumia uzazi wa mpango.
Hoja iliyoungwa na Mwananchi mwingine Fredy Kavishe aluyeomba kujua kuhusu unyanyapa unaofanywa na baadhi ya watoa huduma wa afya kwa mama ambaye mimba yake imeharibika, kwa kutaka kujua mikakati ya kuboresha suala hilo.
“Katika vituo vya mikoani au nje ya miji mwanamke akiharibikiwa ananyanyapaliwa na baadhi ya wakunga, tunataka kujua Serikali inamkakati gani katika kuzuia unyanyasaji huu,” alihoji Kavishe