Kutoka China: China na utamaduni wa kuthamini chai
Muktasari:
- Katika nchi nyingi za Afrika chai hunywewa wakati wa asubuhi ila ni tofauti na nchini China, ambako hunywewa wakati wowote kwa maana ya asubuhi, mchana, jioni. Kwa kifupi muda wowote ni wakati wa chai.
Mwishoni mwa Novemba mwaka huu, Shirika la Elimu na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco), lilihuisha orodha yake ya urithi wa utamaduni usioshikika, mbinu za jadi za Kichina za kutengeneza chai zilikuwa miongoni mwa vitu vilivyoorodheshwa.
Orodha hiyo ilipitishwa na mkutano wa 17 wa kamati ya kiserikali ya Unesco ya kulinda urithi wa utamaduni usioshikika uliofanyika mjini Rabat, Morocco.
Orodha hiyo mpya inaifanya China kuwa na jumla ya vitu 43 vilivyoorodheshwa, ikishika nafasi ya kwanza duniani.
Mkurugenzi wa idara ya urithi wa utamaduni usioshikika wa Wizara ya Utamaduni na Utalii ya China, Wang Chenyang aliitaja hatua hiyo kama ushindi kwa nchi yake, akisema kwa mara nyingine inaonyesha mchango muhimu wa ustaarabu wa China kwa utamaduni wa binadamu.
Kwa haraka unaweza usielewe kwa nini chai, ukizingatia chai ni kuchemsha tu maji na kutia majani. Lakini sivyo, nchini China utegenezaji wa chai si lelemama wala si kitu kinachofanyika kwa wepesi.
Kuandaa chai nchini China kunahitaji weledi. Kuanzia kulima chai, kuvuna majani ya chai, kuyaandaa kwa ajili ya kufungasha, kuandaa kinywaji chake na unywaji wa chai yenyewe ni somo ambalo hata baada ya kuhudhuria darasa lake unahitaji muda wa ziada kulielewa vilivyo.
Nikiwa hapa China nilipata fursa la kuhudhuria darasa la chai, nakumbuka wakati wa somo la unywaji wa chai mwalimu alieleza kitu ambacho sikuwahi kukifahamu, alisema: “Ukiwa ugenini ukipewa chai nusu kikombe maana yake mwenyeji anataka ukae, ila ukijaziwa kikombe maana yake kunywa umalize uondoke”.
Kwa mujibu wa utamaduni wa chai nchini China, tulio wengi tulishawahi kufukuzwa majumbani kwa watu au kulazimishwa kufukuzwa, pale unapomiminiwa kidogo, unajikuta unamwambia mwenyeji jaza tu hamna shida.
Nchini China kuna utajiri wa chai, pia zipo aina mbalimbali za kinywaji hicho na kila aina ina uandaaji wake na kiwango cha joto kinachotakiwa.
Chai ina maana gani China
Katika kupekuwa mtandao kupata maarifa juu ya kinywaji cha chai, taarifa nyingi za kihistoria zilizopo zinaeleza kuwa kinywaji cha chai asili yake ni nchini China na Myanmar na jambo la kushangaza zaidi mataifa mengine yamekijua kinywaji hicho karne ya 16.
Kwa sasa chai sio ya China pekee, bali ni kinywaji maarufu duniani, inakadiriwa kuwa watu zaidi ya bilioni mbili hunywa chai kila siku, zaidi ya nchi 60 huzalisha zao hilo maarufu la biashara duniani kwa miongo mingi, inaelezwa kuwa karne ya 17 kinywaji hicho kilipata umaarufu mkubwa barani.
Mataifa mengi duniani watu wake hutumia chai kama kifungua kinywa au kinywaji cha wakati wa baridi.
Ukifika nchini China utapata hisia halisi kuwa kweli huenda chai ilianzia hapo, unywaji wa chai katika Taifa hili linaloongoza kwa watu wengi duniani ni utamaduni.
Karibu kila mahali utakapokwenda utakaribishwa kwa kinywaji hicho, katika mikutano mikubwa, midogo na ya kati lazima utakuta chai, hivyo siyo tu kiburudisho, bali ni ukarimu kwa mgeni tofauti na namna ilivyozoeleka sehemu nyingine, huku chai hainywewi ikiwa imetiwa sukari na si ya moto sana.
China kuna aina nyingi za chai na wengine hawawezi kutofautisha ladha isipokuwa wazoefu na wabobevu katika eneo hilo.
Kuna nchi nyingi zinazalisha chai kwa wingi Afrika ikiwemo Kenya, Uganda, Malawi, Tanzania, Rwanda na Msumbiji, lakini ukitaka kupata ladha tofauti za chai, utazipata China.
Katika kuenzi utamaduni wa chai katika Taifa hilo kwenye jimbo la Fujian, ambalo ni maarufu kwa kilimo cha chai, kuna bustani mahususi kwa ajili ya kinywaji hicho iitwayo Yanzike Ecological Tea Garden.
Bustani hii ilianzishwa rasmi mwaka 2018 ikiwa na ukubwa wa ekari 66.7.
Butsani hiyo unaweza kuiita kama shamba darasa tu, maana kilimo cha chai katika jimbo hilo kimeenea maeneo mengi, lakini katika eneo hilo wanalima chai ya aina yake, hakuna matumizi ya kemikali kama mbolea na mbinu za kupambana na wadudu na magonjwa ya mimea zinatumika zile za asili.
Mbinu za kisasa zinatumika kutoa taarifa za hali ilivyo katika bustani hiyo sanjari na kupima udongo, ili kupata taarifa za kuongeza ufanisi katika uzalishaji na ubora wa bidhaa yenyewe.
Hata nishati inayotumika hapo ni ya nguvu ya jua.
Machi mwaka jana wakati wa ziara ya Rais Xi Jinping, katika jimbo la Fujian alitembelea bustani hiyo, alielekeza kuendelea kupigia chapuo utamaduni wa chai na kukuza sekta ya kilimo cha zao hilo.
Vyombo vya habari vya ndani ya China viliielezea ziara hiyo kama ya kumkumbusha mbali Xi, aliyefanya kazi huko kwa muda mrefu na wakati huo alilisistiza kilimo cha zao hilo kama mkombozi wa uchumi.
Katika mji wa Wuyishan ambapo inapatikana bustani hiyo zao la chai kumepatikana ajira kwa watu wengi kuanzia uzalishaji wa chai yenyewe, uongezaji wa thamani na bidhaa za chai, kwa ufupi mnyororo wa thamani ya zao hilo unaonekana waziwazi.
Ili kuwa na uendelevu Serikali ya Wuyishan pamoja na ya jimbo la Fujian wameanzisha taasisi ya utafiti wa zao la chai katika eneo hilo.
Kwenye migahawa mbalimbali ndani ya jimbo hilo ambalo ni kitovu cha chai na mnyororo wa thamani mzima, kuna bidhaa nyingi zinazotengenezwa kwa chai, zikiwamo ice cream ya chai na baadhi ya vyakula vinapikwa kwa ladha ya kinywaji hicho.