Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zingatia haya fursa za Watanzania China

Muktasari:

  • Miongoni mwa mambo yanayowakwamisha baadhi ya Watanzania kushindwa kunufaika na fursa zilizopo China ni pamoja na kutojua au kutozingatia sheria na taratibu za usafirishaji bidhaa, uzalishaji hafifu wa bidhaa kwa ajili ya kusafirisha kwenda China, pamoja na kutozingatia kuongeza thamani ya bidhaa zao.



Dar es Salaam. Wakati uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na China ukitajwa kuzalisha fursa lukuki, kiini cha baadhi ya Watanzania kushindwa kunufaika na fursa hizo chawekwa bayana.

Miongoni mwa mambo yanayowakwamisha ni pamoja na kutojua au kutozingatia sheria na taratibu za usafirishaji bidhaa, uzalishaji hafifu wa bidhaa kwa ajili ya kusafirisha kwenda China, pamoja na kutozingatia kuongeza thamani ya bidhaa zao.

Pia vifungashio duni vya baadhi ya bidhaa zinazosafirishwa pamoja na baadhi yao kufanya mambo ambayo ni kinyume na sheria ya nchi hiyo.

Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Juni 25, 2026 na Balozi wa Tanzania nchini China, Dk Suleiman Haji Suleiman wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema Tanzania kwa sasa inauza bidhaa zenye thamani ya takribani dola bilioni 1.8 (Sh4.7 trilioni) pekee katika soko la China, sawa na chini ya asilimia 10 ya biashara yote kati ya nchi hizo mbili, huku bidhaa zinazoagizwa kutoka China zikifikia zaidi ya dola bilioni 21.3 (sawa na Sh55.91 trilioni).

"Tunaona kuna pengo kubwa katika mizania ya biashara. Wenzetu wanauza bidhaa nyingi kwetu kuliko tunavyouza kwao, jambo linaloonyesha bado hatujatumia kikamilifu fursa zilizopo katika soko la China," amesema.

Amefafanua kuwa moja ya vikwazo vinavyowarudisha nyuma baadhi ya Watanzania kunufaika na fursa hizo ni pamoja na  kutokuwa na uzalishaji wa kutosha wa bidhaa zinazohitajika katika soko la China pamoja na ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu namna ya kufikia wanunuzi wa nchi hiyo.

Pia amesema baadhi ya Watanzania hawaelewi sheria za kusafirisha bidhaa na namna ya kuomba vibali vya lazima nchini China, jambo linalofanya biashara zao kukwama bandarini.

"Suala la vifungashio kwa baadhi ya bidhaa zinazosafirishwa pia ni changamoto, baadhi ya watu wanasafirisha bidhaa kama korosho kwa kufungasha katika magunia hali inayopunguza thamani ya bidhaa hizo," amesema.

Pamoja na changamoto hizo, Dk Suleiman ametaja baadhi ya bidhaa ambazo zinaendelea kupata mahitaji makubwa nchini China kuwa ni pamoja na parachichi, korosho, ufuta, katani, tumbaku, karafuu na mazao mengine ya kilimo, akisisitiza kuwa Tanzania ina nafasi kubwa ya kuongeza mapato ya fedha za kigeni endapo wazalishaji na wafanyabiashara wataongeza uzalishaji wenye ubora unaokidhi viwango vya kimataifa.

Aidha, amebainisha fursa katika sekta ya utalii, ambapo baada ya filamu ya ‘Amazing Tanzania’, idadi ya watalii wa wa China imeongezeka kutoka 14,000 mwaka 2022 hadi kufikia 82,000 mwaka huu.

Katika elimu, alieleza kuwepo kwa ufadhili wa masomo na hata mafunzo ya muda mfupi ya Akili Bandia (AI) kwa vijana.

Amesema ubalozi wa Tanzania nchini China umejipanga kuhakikisha unatoa huduma kwa Watanzania wote wanaohitaji msaada wa kuingia katika soko la nchi hiyo bila ubaguzi.

"Siyo vyema kufika ubalozini pindi tu wanapopata majanga, wanaweza kufika kwa ajili ya kupata ushauri wa fursa mbalimbali zinazopatikana.”

“Ubalozi uko tayari kuwahudumia Watanzania wote bila kujali uwezo wao au ukubwa wa biashara zao. Kazi yetu ni kuhakikisha wanapata taarifa, mwongozo na usaidizi unaohitajika ili waweze kutumia fursa zilizopo China," amesema.

Ameongeza kuwa wananchi watakaotembelea maonyesho ya Sabasaba watapata nafasi ya kupata maelezo mbalimbali kuhusu fursa za biashara, uwekezaji na namna ya kupeleka bidhaa zao katika soko la China.

Aidha, amewataka wafanyabiashara na wazalishaji wa ndani kutumia vizuri uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya Tanzania na China kwa kuongeza thamani ya bidhaa zao na kuzingatia viwango vinavyotakiwa katika masoko ya kimataifa.

Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza pengo la biashara kati ya nchi hizo mbili na kuongeza mchango wa sekta ya biashara katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Ikumbukwe kuanzia Mei mosi, 2026, China imeanza kutekeleza rasmi utaratibu wa kuondoa ushuru wa forodha (zero tariff) kwa bidhaa kutoka Tanzania na nchi nyingine 52 za Afrika zenye uhusiano wa kidiplomasia na taifa hilo.

Hatua hiyo inatajwa kuwa ya kihistoria huku ikifungua soko la watu zaidi ya bilioni 1.4 kwa bidhaa za Afrika bila kikwazo cha ushuru.