Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kulala mahabusu adhabu wanaopita barabara za mwendokasi

Muktasari:

  • Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema awali madereva walipokamatwa wakipita barabara ya mwendokasi hawakuadhibiwa.

Dar es Salaam. Kwa wenye haraka wanaolazimisha kutumia barabara za Mabasi yaendayo Haraka (BRT) za mradi wa awamu ya kwanza wakikamatwa na polisi watarajie kutozwa faini, kulala mahabusu, kisha kufikishwa mahakamani.

Baadhi ya madereva wa magari ya Serikali na binafsi tayari wameshaadhibiwa kwa nyakati tofauti walipopita katika barabara za BRT Morogoro, Kawawa hadi Morocco.

Adhabu hiyo haiwahusu wanaotumia barabara za mwendokasi Kilwa, maeneo Karume hadi Jitegemee  ambako wameruhusiwa na Serikali kutokana na mradi  wa mabasi hayo kutoanza kazi.

Awali, madereva waliotumia barabara hizo walipokamatwa walirudishwa walikotoka ili kutafuta njia zingine na kuendelea na safari.

Hivi sasa dereva wa gari, bajaji au pikipiki anapokamatwa katika barabara za BRT ni lazima kulala mahabusu, kufikishwa mahakamani na kisha kulipishwa faini kulingana na kosa alilotenda.

Hatua hiyo inatokana na Jeshi la Polisi kushirikiana na walinzi wa barabara hizo, kuwakamata wanaokiuka sheria na utaratibu kwa kupita njia za BRT.

Hata hivyo, utaratibu unaruhusu magari ya polisi, zimamoto, ambulensi na magari ya viongozi wanaotakiwa kuwahi sehemu kupita kwa dharura.

Septemba 16, 2022 Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillius Wambura alikazia utaratibu wa magari yanayoruhusiwa kupita kwenye barabara za mwendokasi, akisema yanatakiwa kupita wakati wa dharura na si vinginevyo.

Hata hivyo, alieleza si wakati wote magari hayo yatatakiwa kupita kwenye barabara hizo.

“Siyo sahihi magari hayo kupita wakati wote isipokuwa wakati wa dharura. Sitegemei gari la polisi anayekwenda ofisini asubuhi akapita kwenye barabara ya mwendokasi,” alisema.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), William Gatambi ameliambia Mwananchi kwa sasa anayekamatwa zinatumika sheria za kawaida za usalama barabarani.

“Endapo sheria ya Dart ikipitishwa ya viwango vya adhabu vitakuwa tofauti. Kwa sasa ukikamatwa unapelekwa Central Police (Kituo Kikuu cha Polisi), unalipishwa adhabu na kulala,” amesema.

Amesema kwa mujibu wa sheria ya Dart itakayotoka, adhabu itakuwa viwango vya juu ili watu wasijaribu kupita katika barabara hizo, akisisitiza hairuhusiwi kupita katika njia hizo.


Ushuhuda waliokamatwa

Baadhi ya madereva waliokamatwa kwa kosa la kupita barabaza za BRT wameieleza Mwananchi leo Jumatano Machi 5, 2025 namna walivyokamatwa na polisi katika maeneo tofauti ya Kimara, wilayani Ubungo.

Dereva wa Serikali (jina tumelifadhi) amesema alikamatwa Ubungo saa moja usiku, licha ya kujieleza kwa askari na walinzi wa barabara hizo, hakueleweka.

“Sitaisahau siku ile nilipiga simu hadi… lakini askari hawakuelewa, wakaniambia haiwezekani lazima niende nikalale Central Police kisha nilipe faini ndipo niachiwe huru,” amesema.

Amesema baada ya majadiliano yaliyodumu kwa saa mbili aliamriwa kuwasha gari kuelekea kituo cha polisi kwa hatua zaidi.

“Nilipofika Central niliingizwa moja kwa moja mahabusu, niliwakuta madereva wengine wa Serikali na binafsi wakiwa ndani kwa kosa la kupita mwendokasi. Kesho yake asubuhi nilitoka kwa kulipa faini zaidi ya Sh60,000 kupitia namba ya malipo ya Serikali,” amesema.

Dereva Abdul Juma, amesema alikamatwa saa mbili usiku Kimara, baada ya kukuta askari zaidi ya wanne na walinzi wa miundombinu ya BRT walioweka vizuri katika njia hiyo.

“Waliniambia lete leseni yako, geuza gari uelekeo wa kwenda Central hakuna mjadala. Si kuzuri kupita mwendokasi, ukidakwa faini, kulala mahabusu lazima, haikwepeki,” amesema.

Amesema ukikamatwa unapita mwendokasi unapaswa kujiandaa kulala mahabusu, kisha kulipa faini ambayo inawezekana ikalipiwa mahakamani.

Dereva wa bajaji, Anord Komba, amesema alikamatwa Januari, mwaka huu, Ubungo Maji baada ya kupita katika barabara hizo.

“Ilikuwa asubuhi nilikuwa nakwepa foleni kwenye barabara ya kawaida nikajikuta napita mwendokasi, nilikamatwa na kupelekwa Central pale stesheni,” amesema.


Kauli ya Muliro  

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema awali madereva walipokamatwa walirudishwa ili kujirekebisha.

“Tuligundua hawajali chochote, miongoni mwao wanakuwa walewale, wanajirudia. Kulingana na uzito wa suala hili (kupita mwendokasi), sasa hivi tukikukamata tunakuweka mahabusu.

“Kwanza tunakuhoji kwa saa nne ile ya kwetu ya kisheria, kisha tunapumzika, tunakuhoji tena saa nne nyingine. Tunataka kujua una akili timamu? Je unajua maana ya barabara za mwendokasi? Athari zake kwa magari ya kawaida? Je unazitambua barabara za mwendokasi?” amesema.

Kamanda Muliro amesema kutokana na mahojiano wamebaini asilimia kubwa ya madereva wanaokamatwa wana ufahamu mkubwa ndiyo maana kesho yake wanapelekwa mahakamani ambako wanalipa faini au kwenda jela.

“Lengo la polisi siyo faini bali kuzuia makosa ya watu kupita mwendokasi kinyume cha utaratibu,” amesema.

Ingawa hakuwa tayari kutaja idadi ya madereva waliokamatwa, amesema wanaoongoza kuvunja utaratibu ni wenye magari binafsi.

“Madereva wa Serikali ni waoga, tofauti na binafsi ambao wakikamatwa wapo tayari kulipa faini, lakini lengo letu siyo faini bali waache kupita katika barabara hizo,” amesema.