Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mtazamo wa wadau magari binafsi kulipia barabara ya BRT

Muktasari:

  • Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dart, Dk Athuman Kihamia amesema pendekezo likifika kwao watalifanyia kazi.

Dar es Salaam. Wakati Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akiwataka wataalamu wa sekta ya ujenzi kubuni mbinu za kupunguza foleni mijini, akipendekeza kutumiwa njia za Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) na magari binafsi kwa kulipia, baadhi ya wadau wameibua mtazamo tofauti.

Ulega alitoa pendekezo hilo Februari 13, 2025 kwenye mkutano wa baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo uliofanyika mkoani Singida,

"Kwa nini barabara moja ibaki tupu kwa muda mrefu wakati magari mengine yamekwama kwenye foleni? Nchi nyingine zinatumia mfumo wa kulipia ili kuepuka foleni, tunaweza kufanya hivyo hapa pia," alisema Ulega.

Baadhi ya wadau wa usafirishaji waliozungumza na Mwananchi leo Februari 15, akiwamo Mwenyekiti Chama cha Wamiliki wa Malori Wadogo na Wakati Tanzania (Tamstoa), Chuki Shabani amesema uamuzi huo hautaleta tija kama hakutakuwa na barabara za kutokea nje ya mji.

Amesema unaweza kusaidia katikati ya jiji lakini inapofika maeneo ya Kibaha kuelekea Chalinze hali inaweza kuwa mbaya zaidi kutokana na barabara kuwa nyembamba.

“Ndiyo maana katika mapendekezo yetu tulisema ili kupunguza foleni, kuna haja ya kutengeneza barabara mbadala hata za changarawe ambazo malori yatapita na barabara za kawaida tukaachia magari madogo na ya usafiri wa umma.

“Kusema kuruhusiwa watu kupita mwendokasi ndiko kutaleta ahueni, siyo kweli zaidi kunaweza kuongeza foleni katika barabara hiyo kwa kuwa kila mtu atataka kuwahi na ipo siku jiji likafunga kabisa,” amesema.

Katibu wa Umoja wa Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Shifwaya Lema amesema ni wazo zuri lakini inapaswa kutolewa elimu kwanza ili kuepusha ajali.

Amesema yatahitajika maelekezo ya nani anayestahili kupita katika barabara hizo, vinginevyo itakuwa vurugu.

“Nadhani ni jambo jema kufanya hivyo ukizingatia Serikali imewekeza fedha nyingi katika mradi huo, kikubwa elimu itolewa mapema ili uamuzi huo uwe na inaweza kusaidia maamuzi hayo kuwa na tija,” amesema.

Hata hivyo, amesema foleni katikati ya jiji inasababishwa na uwepo wa bajaji, hali iliyothihirika wakati wa mkutano wa nishati Afrika uliofanyika hivi karibuni walipozuiwa kuingia katikati ya jiji.

Mwekezaji katika sekta ya usafiri wa daladala, Break Salim Break, amesema uamuzi huo ukifikiwa utasaidia kupunguza foleni na wako tayari kulipia.

“Hata wakisema wanaturuhusu tulipie labda Sh2,000 kila safari tutakuwa tayari kwa kuwa tunajua tutawahi kwenda na kurudi, lakini pia tutapunguza matumizi ya mafuta,” amesema.

Mchambuzi wa masuala ya uchumi na kijamii, Oscar Mkude amesema Serikali iseme iwapo imeshindwa kuendesha mradi huo kwa kuwa haikuwa lengo kutumiwa na magari mengine.

Amesema zimekuwapo kauli mbalimbali za viongozi kuhusu ujio wa mabasi mengine, akieleza yakifika barabara hazitatosha iwapo magari binafsi yataruhusiwa kupita.

Kwa mujibu wa Serikali hadi sasa Barabara ya Morogoro inahitaji mabasi 170, huku ya Mbagala ikihitaji mabasi 500.

Hivi karibuni Kampuni ya Uendeshaji wa Mabasi ya Mwendo wa Haraka (Udart), inatarajia kuleta mabasi 100.

“Labda watuambie ni suala la kuyaruhusu kwa muda huu ambao mabasi hayo yapo machachae na barabara zingine bado hazijaanza kutumika, lakini kama itakuwa ndiyo moja kwa moja, tutapoteza maana nzima ya mradi huo,” amesema.

Mkude amesema: “Kwa kuwa watu wengi wapo tayari kusimama kwenye hayo mabasi kwa kukujua wanatoka kituo A na kufika B kwa haraka, lakini leo ukisema magari mengine yapite humo ina maana hawataona sababu ya kuyapanda hasa kutakapokuwa na basi la mwendokasi mbele linaloshusha abiria inabidi wa nyuma msimame.

“Malengo ya kuwa ni mradi huu ni ifike mahali mtu aone fahari kuacha gari nyumbani na kupanda mabasi hayo japo ni wazo zuri la kuongeza mapato lakini pia tufikirie ndiyo malengo hasa ya uanzishwaji wa mradi huu?” amesema.


Walichosema DART

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dart, Dk Athuman Kihamia amesema kilichosemwa na waziri ni pendekezo na kuwapa kazi hiyo wataalamu kulifanyia kazi.

Dk Kihamia amesema endapo litakuja kupelekwa kwao rasmi basi na wao wataangalia namna ya kulitekeleza.

“Kwa sasa siwezi kusema lolote kama hili linawezekana au la kwa kuwa kilichosemwa na waziri ni pendekezo la kuwapa watu kulifanyia kazi, ila litakapokuja kwetu rasmi tutaona vile tunaweza kufanya kwa upande wetu,” amesme.

Msimamo ACT-Wazalendo

Waziri Kivuli wa Miundombinu ACT-Wazalendo, Mohammed Mtambo katika taarifa yake leo Februari 15 amesema wanapinga kauli ya waziri Ulega.

Amesema mradi huo ulijengwa kwa fedha za walipakodi wa Tanzania, hivyo ni haki ya kila mwananchi kuutumia bila vikwazo vya gharama.

“Kuweka ada kwa huduma ambayo ilikusudiwa kupunguza msongamano wa magari na kurahisisha usafiri wa umma ni kinyume cha malengo. Huu ni ubaguzi wa wazi ambapo sasa wananchi masikini watalazimika kubaki kwenye foleni kwa sababu hawawezi kumudu gharama mpya,” amesema.

Amesema ACT-Wazalendo inasisitiza kuwa barabara ya mwendokasi ni mali ya umma na haitakiwi kuwa biashara ya kuwanufaisha wachache.

“Waziri Ulega angejikita kuchukua hatua madhubuti za kutatua changamoto za uendeshaji wa mabasi ya mwendokasi ili kuleta ufanisi na kumaliza tatizo la msongamano, uhaba wa magari na uchakavu,” amesema.

ACT-Wazalendo imesema Serikali ina wajibu wa kuhakikisha huduma za usafiri wa umma zinabaki kuwa nafuu na kupatikana kwa wananchi wote bila ubaguzi wa kiuchumi.

“Kama Serikali inaona kuna haja ya kuwa na barabara ya haraka ya kulipia (Express toll road) ijenge au iruhusu sekta binafsi ijenge kwa ajili hiyo badala ya kutumia miradi iliyojengwa kwa fedha za umma au mikopo itakayolipwa na fedha za umma ili kuwanufaisha watu wachache tu,” amesema.

Amesema chama hicho kinaitaka Serikali kuacha mara moja mawazo hayo, badala yake kuelekeza juhudi katika kuboresha miundombinu kwa ajili ya wote.

“Tunatoa wito kwa Serikali kutafakari ujenzi wa barabara za mzunguko (ring roads) kuzunguka mji wa Dar es Salaam ili kuyaondoa malori kutumia barabara za katikati ya mji yanapobeba mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam,” amesema.