Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kivumbi kipya mjadala wa bandari

Dar es Salaam. Muswada mpya wa Sheria ya Uwekezaji uliowasilishwa bungeni kwa mara ya kwanza hivi karibuni umeibua mjadala mpya, ukihusishwa na sakata la makubaliano ya uendeshaji na uboreshaji wa bandari nchini.

Muswada huo, pamoja na mambo mengine, unapendekeza kutotumika kwa sheria mbili zilizopitishwa na Bunge mwaka 2017 kwa madhumuni ya kulinda rasilimali za nchi katika miradi ya uendelezaji na uboreshaji wa bandari.

Sheria hizo ni ile ya Mamlaka ya Nchi kuhusu Umiliki wa Rasilimali na Maliasili na Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu masharti hasi katika mikataba inayohusu Rasilimali na Maliasili za nchi Sura ya 450, zote za mwaka 2017.

Hatua hiyo imetajwa kuwa inalenga kuondoa vifungu hivyo ili kutengeneza mazingira ya Kampuni ya DP World kufanya uwekezaji nchini.

Tayari muswada huo umesomwa kwa mara ya kwanza Juni 28, 2023 bungeni na Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria itauchambua kwenye vikao vya Kamati Agosti mwaka huu, huku wadai mbalimbali wakiwa tayari wamealikwa kwa ajili hiyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria, Dk Joseph Mhagama hakupatikana kuzungumzia muswada huo, lakini mjumbe wa kamati hiyo ambaye ni Mbunge wa Ziwani (CCM), Ahmed Juma Ngwali alisema muswada wao na wajibu wao kama kamati ni kutafuta maoni na kuyachakata.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Selemani Kakoso (Mpanda Vijijini, CCM) alisema muswada huo umelenga kuboresha uwekezaji katika bandari.

“Mabadiliko haya yanalenga kufanya maboresho, lakini tulichoishauri Serikali, tuangalie mazingira hata kama tunaingia kwenye uwekezaji tuingie mikataba ambayo ina manufaa kwa nchi. Hicho ni kitu cha msingi hata kwenye kamati yetu tuliishauri Serikali na wameyachukua na kuyafanyia kazi.

“Maoni yetu sisi kama kamati kama kwanza tuliyatoa, tuliishauri Serikali kwenye maeneo ambayo watu walikuwa na wasiwasi.

“Suala la uwekezaji kwa bandari ya Dar es Salaam ni muhimu kwa sababu ukiangalia kwenye ukanda wa Afrika Mashariki pwani yote hiyo, yaani uanzie kule Afrika Kusini hadi Somalia, sisi bandari tunayoizidi ni ya Somalia ambako hakuna hata Serikali,” alisema.

Alipotafutwa Mwanasheria wa Wizara ya Ujenzi, Mohamed Salum, alimtaka mwandishi kuuliza swali hilo kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Eliezer Feleshi alipopigiwa simu jana, alimtaka mwandishi kumtafuta baadaye, lakini alipopigiwa tena simu yake haikupatikana.

Hata hivyo, katika maelezo yake yaliyoambatanishwa na muswada huo, Feleshi anasema:

“Sehemu ya nne na tano ya muswada zinapendekeza marekebisho ya Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa mali na rasilimali asilia, Sura ya 449 na Sheria ya Mapitio na majadiliano kuhusu masharti hasi katika mikataba ya mali na rasilimali Asilia, Sura ya 450 ili kuhakikisha kuwa utekelezaji wa sheria hizo hauathiri utendaji wa maeneo ya bandari, bandari za nchi kavu na bandari za maeneo ya maziwa nchini.

“Madhumuni ya marekebisho haya ni kewezesha bandari katika Jamhuri ya Muungano kufikia viwango vya kimataifa vya kiutendaji na kuvutia nchi nyingi zaidi na shehena kubwa za mizigo kutumia bandari za hapa nchini,” inasema sehemu ya muswada huo iliyosainiwa na Feleshi.


Wadai waukosoa

Akizungumza na Mwananchi jana kuhusu muswada huo, Wakili Boniface Mwabukusi alisema sheria zinazofanyiwa mabadiliko kupitia muswada huo zitawaondolea nguvu wananchi juu ya umiliki wa rasilimali za nchi.

Alisema matokeo yake Serikali itafanya jambo lolote bila wananchi kuulizwa, kushirikishwa wala kuwepo uwazi wa majadiliano ya mikataba iliyokuwepo katika hatua zote.

“Mabadiliko haya yanayofanyika si kwa masilahi ya umma, sheria hizi zinalenga kuondoa uamuzi kwenye mikono ya watu na kupeleka kwenye mikono ya wageni na viongozi wachache,” alidai.

Mwabukusi alisema, Serikali inataka kuondoa kifungu cha pili cha Sheria ya Mamlaka ya nchi kuhusu umiliki wa mali na rasilimali Sura ya 449 na kupendekeza masharti ya sheria hiyo yasitumike.

“Kifungu cha pili cha sheria kinataka kuondoa takwa lililoingiza bandari, maziwa na uwekezaji wowote unaohusu bahari isiwe sehemu ya maliasili, kwa hiyo wanaepuka kifungu kulazimisha wananchi kushirikishwa na hivyo wawe wanafanya maamuzi wenyewe,” alisema.

Mwabukusi aliungwa mkono na Wakili mwenzake, Jebra Kambole aliyesema marekebisho hayo yanaboresha mazingira ya uwekezaji utakaofanywa na Kampuni ya DP Wolrd ya Dubai katika bandari za Tanzania.

“Hayati Rais John Magufuli alitunga sheria ambazo zinalinda rasilimali za nchi na hizo sheria za kulinda rasilimali za nchi zilikuwa hasa kwenye mikataba kama hii ya DP World.

Alisema muswada ukipita sheria ya ulinzi wa maliasili na makubaliano ya mikataba hazitatumika katika mambo yanayohusiana na usafiri wa majini, bandari kavu na maziwa.

Akijadili hilo, mwanaharakati Bob Wangwe alisema muswada huo wa sheria una maana Bunge na Serikali wameamua kwa namna yoyote lazima mkataba wa DP World ufanyiwe kazi.

“Sheria yetu iliyofanyiwa mabadiliko mwaka 2017 ilikuwa inalinda rasilimali zetu, hivyo inabana utekelezaji wa mkataba wa DP World, sasa hawa wameamua kufanyia mabadiliko ili waweze kuingia mkataba huo,” alisema.

Ili kupata ufumbuzi, Wangwe alisema atatafuta busara za mahakama kupewa tafsiri.

Moja ya taasisi zilizopewa muswada huo kutoa maoni ni Twaweza, ambayo ilikiri kupokea wito huo.

Hata hivyo, Meneja utetezi wa taasisi hiyo, Annastazia Rugaba alisema bado wanatafuta wataalamu wa kuuchambua muswada huo ili kupata maoni ya kupeleka bungeni.

Mbali na sheria hizo, muswada huu unapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Nguvu ya Atomu, Sura ya 188, Sheria ya Chuo cha Bahari Dar es Salaam na Sheria ya Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda, Sura ya 159.