Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mawakili waiomba mahakama uwekezaji bandari usubiri, Serikali yaomba muda

Muktasari:

Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya imeombwa kuharakisha kupitia maombi ya kupinga mkataba wa uwekezaji wa bandari kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai kupitia Kampuni DP World.

Mbeya. Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya imeombwa kuharakisha kupitia maombi ya kupinga mkataba wa uwekezaji wa bandari kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai kupitia Kampuni DP World.

Wakili wa waleta maombi, Boniface Mwabukusi amesema hayo leo Jumatatu Julai 3, 2023 mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Dastan Ngunguru huku akisisitiza shughuli za uwekezaji wa kampuni hiyo zisubiri shauri hilo.

Mwabukusi amesema kuwa wakati Mahakama ikiendelea kupitia ombi hilo ndani ya siku 17 shughuli zozote mwekezaji kwenye bandari zisiendelee.

“Utekelezaji wa kitu kinacholalamikiwa pande zote mbili zikutane na kujadili na kwamba ugomvi uliopo baina ya wananchi na Serikali ni kupoteza rasilimali za nchi,” amesema.

Ameiomba Mahakama tukufu kujibu maombi kwa muda uliopangwa kulingana na aina ya shauri kwa maslai mapana ya taifa na Watanzania kwa ujumla.

Mwanasheria wa Serikali, Hangi Chang'a ameiomba kesi hiyo ipangwe Julai 14 mwaka huu ili waweze kupitia hoja na kutenda haki kulingana na mwenendo wa kesi.

“Tulipewa siku 21 tangu tulipopokea maombi na leo zimebaki siku 17 tunaomba tupewe muda kupitia kulingana na hali ya kesi yenyewe,” amesema.

Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Dustan Ndunguru amesema kesi hiyo ni ya kikatiba na inasikilizwa na majaji watatu inapaswa kupitia maombi kwa umakini pasipo kuleta athari.

Amesema kesi hiyo ni kesi ya msingi inahitaji mwenendo wake kwenda vizuri kwa upande zote mbili na kesi hiyo itasikilizwa mfululizo kuanzia Julai 20 mwaka huu.

Awali kesi hiyo ilifunguliwa na wanasheria Juni 26 mwaka huu kupinga mkataba wa  bandari na kuanza kusikilizwa leo Julai 3, 2023.

Kesi hiyo namba 05/2023 imewahusisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Katibu wa Bunge.

Kwa upande wa waleta maombi wanaongozwa na Mwanasheria wa kujitegemea, Boniface Mwabukusi, Philipo Mwakilima na Livino Ngalimitumba.

Upande wa majaji wengine watakaosikiliza kesi hiyo ni Abdi Kagomba na Mustaphar Ismail, huku mawakili wa Serikali ni Hangi Chang'a na Ayoub Sanga.