Kitonga, maeneo yenye ajali nyingi kufungwa kamera

Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoani Iringa, Salim Abri Asas akizungumza baada ya kumaliza ukaguzi wa maeneo yenye ajali za mara kwa mara
Muktasari:
- Kutokana na ajali za mara kwa mara katika eneo la Mlima Kitonga na mengine yenye changamoto hiyo, Kamati ya Usalama Barabarani mkoani Iringa imedhamilia kufunga kamera ili kuongeza usalama.
Iringa. Wakati ikiwa imepita siku mbili tangu basi la Premier Express kupata ajali katika Mlima wa Ipogoro, Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa imeanza mchakato wa kufunga kamera katika maeneo hatarishi ambayo yamekuwa na ajali nyingi ikiwamo Mlima Kitonga ili kuongeza usalama.
Maeneo mengine hatarishi yatakayoguswa na kamera hizo ni pamoja na Changalawe – Mafinga, Wilayani Mufindi maarufu kwa jina la Majinja na Mlima Nyang’oro, Barabara ya Dodoma-Iringa.
Akizungumza baada ya kukamilisha ziara ya kukagua maeneo hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani, Salim Abri Asas amesema kamera hizo ni miongoni mwa mikakati maalumu waliyojiwekea katika kuhakikisha wanapunguza ajali za barabarani.
Amesema tayari wameshaanza mchakato wa kutafuta wataalamu kwa ajili ya kazi hiyo.
“Teknolojia ukiangalia siyo gharama sana wakati mwingine tuna ‘complicate’ tu, tunaweza kuanza hapa ‘Changarawe’, tukaenda Kitonga kamera ikawa inamonitor saa 24. Askari hawezi kuwa analinda magari saa 24. Madereva nao wajue itakuwa inakamata mpaka namba za magari,” amesema Salim Abri na kuongeza;
“Niwaambie kabisa madereva kamera itakuwa inakamata mpaka namba zao za gari tuwaambie kabisa madereva watakaokuwa wanapita barabara ya Mkoa wa Iringa, muda wao wa kufanya vurugu umeisha,” amesema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amesema katika mifumo ya udhibiti wa ajali lazima kuhakikisha maeneo mengi yanakuwa salama zaidi.
“Mfano eneo hili la Changarawe, upande mmoja kuna mlima, mteremko mkali halafu mlima tena kwa hiyo hapa madereva wanajiachia lazima tufanye jambo katika mifumo ya udhibiti wa ajali kuhakikisha tunaongeza usalama,” amesema.
Kwa upande wao baadhi ya madereva wamesema uwepo wa kamera utasaidia kupata taarifa za madereva ambao kwa makusudi wanavunja sheria bila kujali usalama wa abiria walio wapakia.
“Ni kweli wakati mwingine ajali tunasababishiwa, uwepo wa kamera utasaidia kudhibiti ajali za barabarani. Hofu yangu ni kamera zenyewe kuharibiwa au kuibiwa,” amesema Yasin Kikoti, dereva na mkazi wa Mafinga.