Prime
Kilio mgawanyo fedha za mfuko wa jimbo

Muktasari:
- Bunge limeidhinisha Sh81.864 bilioni kwa ajili ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira)
Dodoma. Mbunge wa Jang’ombe, Ali Hassan Omar maarufu King ameibua malalamiko kuhusu mgawo wa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo, akieleza hauna usawa.
Ameibua malalamiko hayo jana, Ijumaa Aprili 25, 2025, alipochangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Waziri wa wizara hiyo, Hamad Masauni aliliomba Bunge liidhinishe maombi ya makadirio ya mapato na matumizi ya Sh81.864 bilioni, Bunge liliyapitisha.
Mbunge huyo amesema wabunge kutoka Zanzibar hawatendewi haki, kwani mara nyingi wamekuwa wakilalamika juu ya jambo hilo, lakini wanaona utekelezaji haupo na kinachofanyika ni sawa na ‘turuhani’.
Turuhani ni nyongeza ambayo hupewa mtu aliyenunua nazi nyingi ambazo hupewa kwa kubeba bila kuangalia hata kama ni mbovu.
King amesema wabunge wa Zanzibar walipopiga kelele kuwa majimbo ya Bara wanapewa mamilioni ya fedha, waliongezewa kidogo.
Mbunge huyo amesema majimbo ya Tanzania Bara yanapewa fedha nyingi kwenye mfuko huo, lakini upande wa Zanzibar hazifiki kiwango hicho, lakini cha ajabu wote wanapimwa katika kapu moja la CCM.
“Kuna wakati nilisimama kutaka kugoma nisichukue hiyo fedha, hivi mwaka mzima unapewa Sh12 milioni huku mwingine akipewa Sh500 milioni, je, mnaweza kuwa sawa?” amehoji.
Ameomba Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia upya utaratibu huo, akisema wote ni wabunge na wanawakilisha watu kwenye malengo ya pamoja ambayo ni kuwatumikia wananchi.
Pia ameiomba Serikali kuimarisha masuala ya uvuvi kwa kuwa ndiyo fursa pekee iliyobaki visiwani humo, kwani ardhi imekwisha.
Amesema wakati wa Mapinduzi Zanzibar ilikuwa na watu wasiozidi 350,000 lakini katika Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 wanakadiriwa kuwa 1.8 milioni huku ardhi ya kisiwa hicho ikiendelea kumezwa na bahari.
Mbunge wa Sumve, Kasalali Mageni amelalamikia wakuu wa mikoa na wilaya kwa kuingilia kesi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa sababu chombo hicho kinafanya kazi yake vizuri, lakini wateule hao hutumia nafasi zao kudidimiza.
Kasalali amesema mara nyingi kumekuwa na matatizo makubwa mijini yanayosababishwa na kelele kutoka kwenye kumbi za starehe na vilabu vya pombe, lakini wakiwakamata viongozi wa juu huwatoa.
“Napendekeza NEMC iwe mamlaka kamili, chombo hiki kinafanya kazi nzuri lakini hakina meno, fikiria kelele za mijini lakini wakifungia baa ama ukumbi kwa sababu ya kelele wanakwenda wakuu wa mikoa au wilaya wanatoa amri ya kufungua, hii siyo sawasawa,” amesema.
Akiwasilisha hotuba yake, Waziri Masauni amesema vipaumbele ni kushughulikia masuala ya Muungano na kuanzisha Kituo cha Kumbukumbu za Nyaraka za Muungano.
Amesema Serikali itaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 na mradi wa kujenga uwezo wa kitaifa wa kuandaa taarifa za utekelezaji wa mabadiliko ya tabianchi.
“Serikali itaendelea kuratibu maandalizi ya Mpango wa Matumizi ya Maeneo ya Maji, kuhamasisha uwekezaji wa kimkakati na jumuishi na kufanya kaguzi za fedha zilizopokelewa na matumizi yake,” amesema.
Akisoma taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Dk Oscar Kikoyo ameitaka Serikali kuhakikisha fedha zinazoombwa zinatumika vizuri.
Kamati imependekeza kuwa Serikali ijenge utaratibu wa kuwasilisha mbele ya kamati taarifa mbalimbali za utekelezaji wa bajeti kwa mujibu wa sheria.