Kilio cha Watanzania waliokwama Ukraine

Muktasari:
- Wakati majeshi ya Russia yakiendelea kushambulia miji nchini Ukraine, baadhi ya Watanzania wanaoishi nchini humo wameeleza machungu ya vita hivyo wasijue hatima yao.
Dar es Salaam. Wakati majeshi ya Russia yakiendelea kushambulia miji nchini Ukraine, baadhi ya Watanzania wanaoishi nchini humo wameeleza machungu ya vita hivyo wasijue hatima yao.
Tayari Serikali ya Tanzania imeshatoa maelekezo kwa Watanzania wanaoishi nchini Ukraine ikiwataka kukimbilia kwenye nchi za Poland, Romania, Slovakia na Hungary.
Hata hivyo, akizungumza jana kwa mtandao wa WhatsApp, kiongozi wa wanafunzi katika Chuo Kikuu Sumy State, Dk Lahsen Mohammed Kheir, alisema kuondoka nchini humo kwa sasa ni kuhatarisha zaidi maisha.
“Huku kinachoendelea kila siku ni mabomu tu. Kuamua kuondoka kwenda sehemu nyingine ni kujihatarishia maisha kwa sababu miji yote imezungukwa na majeshi,” alisema.
Alisema kila mabomu yanaporushwa, huwa wanakimbilia kwenye mahandaki yaliyo karibu na vyuo ili kujificha.
Hata hivyo, alisema baadhi ya wanafunzi wa Tanzania waliowahi kuondoka kabla ya uvamizi walifika mpaka wa Poland na kufanikiwa kuvuka.
“Wapo waliofika mpakani na kuingia Poland, lakini nako kuna changamoto ya foleni kubwa na inachukua muda mrefu mpaka mtu ahudumiwe. Mtu anakaa hadi saa nane ndio anahudumiwa na kuna baridi kali.
“Wapo waliopokelewa na wameingia Poland. Huko wanapokelewa na Watanzania wengine,” alieleza.
Kwa upande mwingine, Kheir alisema jana walifanya kikao na mabalozi wa Tanzania walioko katika nchi za Ujerumani na Russia kuhusu hali hiyo kupitia mtandao wa Zoom.
“Tumeshauriana tuendelee kukaa hapa kwa sababu hali siyo nzuri,” alisema.
Maelezo hayo yameungwa mkono na mwanafunzi mwingine anayeishi mji wa Kharkiv ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, akisema hakuna usalama zaidi ya kujifungia ndani.
“Ukisafiri kwenda sehemu nyingine ni hatari kwa sababu wanajeshi wa Russia wametanda mitaani na wengine wanavaa sare za jeshi la Ukraine. Njia ya treni iliyobaki ni moja tu na hiyo ikipigwa bomu ndiyo basi tena,” alisema.
Hata hivyo, alisema walifanikiwa kujikusanyia vyakula vya kutosha tangu hatari ya vita ilipoanza.
“Tunachoomba kwa sasa wasije kuzima umeme, gesi na maji, hapo ndipo hakutakuwa na mawasiliano na hali itakuwa mbaya zaidi,” alisema.
Wadai kubaguliwa
Wakati hali ya usalama ikiwa tete, taarifa katika mashirika ya habari ya kimataifa zimeeleza kuwepo kwa ubaguzi wa rangi, hasa kwa Waafrika, waliokuwa wanakikimbia vita wanapofika mipakani, ambapo baadhi yao wamezuiwa kupanda treni ili kuondoka.
Kufuatia hali hiyo, Serikali ya Marekani imetangaza kuandaa utaratibu wa kuhakikisha kila mtu, ikiwemo wanafunzi wa Kiafrika, wanaoondoka Ukraine kutafuta hifadhi wanapata haki sawa.
Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken imesema nchi hiyo itaendelea kutoa misaada ya kibinadamu kwa Ukraine na kuzitaka nchi na wadau wengine kuwawezesha watu wanaokimbia vita kupata hifadhi bila kujali tabaka, dini au utaifa.
“Marekani ni moja ya wafadhili wakubwa wa Ukraine katika misaada ya kibinadamu, ikitoa zaidi ya Dola 405 milioni kwa familia zilizo hatarini tangu Russia ilipoanza mzozo na Ukraine miaka minane iliyopita.
“Msaada wa sasa utakuja kupitia mashirika huru ya misaada ya kibinadamu na itatolewa kwa usawa, ubinadamu na uhuru,” imesema taarifa ya Marekani.
Nchi hiyo imeziomba nchi jirani na Ukraine kuwakarimu wakimbizi wa vita, wakati juhudi za kidiplomasia zikiendelea.
Russia yazidisha mashambulizi
Wakati mazungumzo kati ya Russia na Ukraine yakiendelea katika mpaka wa Belarus, Ikulu ya Kremlin nchini Russia jana ilisema ni mapema mno kufikia hitimisho kutoka kwa duru ya kwanza ya mazungumzo.
Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov alisema Rais Vladimir Putin amefahamishwa kuhusu mazungumzo hayo, lakini ni mapema mno kutathmini matokeo yake.
Tayari ya majeshi ya Russia yameshafanya mashambulizi katika miji ya Kharkiv, Kherson wakisonga mbele kutoka Crimea wanayoidhibiti.
Ukraine inasema zaidi ya raia 350 wameuawa tangu Moscow ilipoanzisha mashambulizi yake Alhamisi iliyopita.
Russia imekubali kuwa imepata hasara lakini haijasema ni wanajeshi wangapi wameuawa kufikia sasa.
“Tusubiri hadi mwisho wa operesheni hii,” alisema Peskov.
Waziri wa ulinzi wa Moscow, Sergei Shoigu alisema mapema jana kwamba Russia itaendelea na mashambulizi yake nchini Ukraine hadi “malengo yake yatimizwe.”
Alisema Moscow inalenga kuwaondoa Wanazi nchini Ukraine, na pia kuilinda Russia dhidi ya tishio la kijeshi linaloandaliwa na nchi za Magharibi.
Wakati huo huo, Serikali ya Uingereza iko tayari kuiondoa Russia kama mmoja wa wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufuatia uvamizi wa Ukraine, msemaji wa Waziri Mkuu Boris Johnson alisema jana Jumanne.
“Nadhani ni jambo ambalo tunataka kulijadili na Umoja wa Mataifa kwa uwazi,” msemaji huyo ambaye amezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, aliwaambia waandishi wa habari.