Prime
Kilio cha wafanyabiashara bandarini

Malalamiko
Akizungumza na gazeti hili juzi, Erick Jackson, ambaye ni msafirishaji wa mazao ya chakula kwenda nje ya nchi alisema changamoto si tu kwa wanaopakia mizigo, bali hata wanaosafirisha mizigo, kwani inachukua muda mrefu kupakiwa.
“Siku hizi mpaka umalize taratibu zote za kupakia kontena inachukua muda mrefu, kuna kontena nimelituma Misri imepita siku karibia 50 bado halijafika, kwanza lilichelewa kutoka hapa lakini hata kufika limechelewa,” alisema.
“Meli nyingi zimekwama hapa zikisubiri mzigo wa kurudi nao, mzigo upo lakini kontena hamna ni za kusubiri, nyingi zimeenda China na mataifa mengine kurudi zinachelewa, hususan za Ulaya, Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini kutokana na hali ndogo ya usalama katika Bahari ya Shamu,” alisema.
Kwa upande wake, Ramadhan Said ambaye ni dereva wa kampuni ya Makombe Logistics alisema ana takribani wiki nzima tangu alipowasili na mzigo wa shaba kutoka nchini Zambia, lakini hajui ataruhusiwa lini kushusha mzigo huo bandarini hapo.
“Kwa kawaida huwa nachukua saa kadhaa kama tano, lakini imekuwa ni tofauti kidogo. Wenyewe wanavyodai kuwa kuna meli haijaja kutokana na sikukuu za mwisho wa mwaka, ndiyo maana tunakutana na adha hizi,” alisema.
Said alisema, “Wanachokifanya wanaandika namba ya kontena na namba ya simu, zamu ikifika wanakupigia simu,” alisema.
Kwa upande wake, Eliachim Kivae wa kampuni ya kupokea mizigo ya Vamwe International Logistics, alisema ucheleweshaji huo unasababishwa na ufanisi mdogo wa ushushaji wa mzigo katika bandari hiyo.
“Unakuta meli kubwa zinachukua hata mwezi kwenye foleni, ndiyo maana wanaondoka na kwenda bandari nyingine,” alisema.
Alitaja pia ongezeko la bei ya kukodi makontena kutoka Dola za Marekani 3,500 (Sh8.76 milioni) hadi 6,000 (Sh15 milioni), akisema lilisababishwa na maambukizi ya Uviko-19 na kusababisha ucheleweshaji wa meli.
Taffa walia na vifaa
Licha ya maboresho yaliyofanyika bandarini hapo, Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (Taffa), Edward Urio ameliambia gazeti hili hivi karibuni kuwa, bado kuna upungufu wa vifaa katika bandari nchini.
“Uwekezaji umefanyika lakini bado vifaa havipo vya kutosha, hili ni jambo tunalopaswa kuliangalia ili kuongeza ufanisi na kuvutia wateja wengi,” alisema.
Hata hivyo, alieleza uwepo wa changamoto katika kuzitangaza baadhi ya bandari, mathalani ya Tanga, hali inayosababisha zisitumiwe na wasafirishaji ilhali zipo katika jiografia shindani.
“Wengi hawaelewi kama kijiografia Bandari ya Tanga ndiyo bandari shindani kwa Bandari ya Mombasa, kwa maana ya ujirani na eneo ulilopo,” alisema.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wakala wa Meli (Tasaa), Daniel Mallongo, alisema msongamano unaolalamikiwa upo pia katika bandari nyingine za Afrika, akitaja sababu mojawapo kuwa ni sikukuu ya Krismasi.
Alisema nchi zote huwa zinaingiza mizigo mingi, kabla ya bandari kufungwa.
“Kama China, wiki ijayo wanafunga angalau kwa wiki tatu hawafanyi kazi, kwa hiyo watu wengi huwa wanaagiza vitu kwa wingi,” alisema.
Wiki iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa alitaja changamoto ya miundombinu ya reli kwa ajili ya kutoa mizigo bandarini, akisema ina uwezo wa kutoa mizigo kutoka katika bandari hiyo kwa asilimia tatu pekee, huku mingine ikihudumiwa na malori.
Alitaja pia kuharibika mara kwa mara kwa skana inayotumika kuskani mizigo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo magari kugonga.
Mvua za El-Nino ni changamoto nyingine iliyotajwa na Mbossa, akisema inaponyesha inasababisha shughuli ya upakuaji wa baadhi ya mizigo kama vile ngano kusimama.
Ujio wa DP World
Miongoni mwa mikakati iliyowekwa na Serikali kutatua changamoto zinazojitokeza katika bandari nchini ni kusaka wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Oktoba 22, 2023 Serikali ya Tanzania ilitia saini mikataba mitatu ya uwekezaji na uendelezaji wa Bandari ya Dar es Salaam kati ya Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Serikali ya Dubai kupitia Kampuni ya DP World.
Kabla ya utiaji saini huo, Serikali iliingia makubaliano na Serikali ya Dubai kuhusu uwekezaji huo (IGA) ambayo yalikosolewa vikali na wadau mbalimbali, wakisema hautakuwa na manufaa kama inavyoelezwa.
Mikataba iliyosainiwa ni pamoja na Mkataba wa nchi mwenyeji (HGA), Mkataba wa ukodishaji na uendeshaji wa gati 4-7 na uendeshaji wa pamoja wa gati 0-3 kati ya TPA na DP World kwa shughuli za kibiashara na kiserikali.
Hata hivyo, hadi sasa DP World haijaanza kazi rasmi katika bandari hiyo.