Bandari ya Mbamba Bay kukuza biashara Tanzania, Zambia na Malawi

Muktasari:
- Bandari ya Mbamba Bay Bandari hiyo iliyopo mwambao mwa Ziwa Nyasa mkoani Ruvuma, inatarajiwa kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo tatu
Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay ukikamilika unatarajiwa kukuza biashara kati ya nchi za Tanzania, Zambia na Malawi.
Bandari hiyo iliyopo mwambao mwa Ziwa Nyasa mkoani Ruvuma, inatarajiwa kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo tatu.
Akizungumza jana Januari 3, 2024 wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa usanifu na ujenzi wa uendelezaji wa bandari hiyo, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema kuwapo kwa bandari hiyo ni fursa ya kijiografia.
Amesema uwepo wa jiografia hiyo unaunganisha nchi zote tatu kama njia fupi na yenye gharama nafuu za usafiri na usafirishaji.
“Bandari ya Mbamba Bay ni kiungo muhimu cha biashara na uchumi kwa mikoa ya mwambao mwa Ziwa Nyasa na ushoroba wa Mtwara ambao ni ukanda muhimu wa kiuchumi,” amesema Waziri Mbarawa.
Pia, amesema uwekezaji katika bandari hiyo utaongeza fursa za kibiashara kwa wananchi wa mwambao wa Ziwa Nyasa ambao sasa watanufaika zaidi na soko kubwa la mazao ya chakula na biashara lililopo Malawi na Zambia.
Pia, amesema Mbamba Bay itafungua fursa za kibiashara za bidhaa za nyumbani na viwandani kutoka katika masoko ya kimataifa ya nje ya nchi ambayo ni kiungo muhimu katika usafirishaji kati ya Bahari ya Hindi na Bandari za Ziwa Nyasa kupitia ushoroba wa Mtwara.
Waziri Mbarawa amesema uwepo wa bandari hiyo ni pamoja na kukuza viwanda vidogo na vya kati.
“Bandari hii ikikamilika itakuwa na uwezo wa kupokea meli zenye uwezo wa kubeba mizigo mikubwa na kuboresha usalama wa watu na vyombo pamoja na kuibua fursa za ajira na biashara wakati wa awamu za ujenzi na uendeshaji,” amesema Mbarawa.
Mamlaka ya Bandari (TPA) imesaini mkataba wa usanifu na ujenzi wa uendelezaji wa Bandari ya Mbamba Bay na Mkandarasi Kampuni ya Xiamen Ongoing Construction Group Co. Ltd ya China kwa utekelezaji wa mradi huo kwa muda wa miezi 24 kwa gharama ya mradi ya Sh75.8 bilioni.
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa amesema katika mwambao wa Ziwa Nyasa kuna bandari nane ambazo ni Mbamba Bay, Liuli, Manda, Kiwira, Lupingu, Itungi, Ndumbi na Matema.
Amesema bandari hizo ni muhimu kwa wananchi na uchumi wa nyanda za juu kusini na ushoroba wa Mtwara katika kuhudumia Tanzania na nchi jirani za Malawi na Zambia kwa kuwa hupitisha mazao ya samaki, vimiminika, makaa ya mawe na abiria.
“Mwaka 2022/23 Bandari za Ziwa Nyasa zilihudumia shehena ya kiasi cha tani 11,635 hii ni ongezeko la kiwango cha shehena kutoka tani 5,410 za mwaka 2021/22.
“Vilevile kiwango cha abiria kiliongezeka kutoka abiria 2,437 mwaka 2021/22 hadi abiria 72,081 mwaka 2022/23,” amesema Mbossa.
Amesema utekelezwaji wa ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay ni wenye tija na manufaa makubwa kwa TPA na Taifa kwa jumla.
Hata hivyo, mwaka jana Serikali ilitenga Sh60 bilioni kuboresha miundombinu ya bandari 15 zilizopo mikoa mitano ya Kanda ya ziwa, zinazosafirisha mizigo kwenda nchi za Afrika Mashariki.