Kilimo cha bangi, mirungi chawaponza

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Aretas Lyimo akizungumza na waandishi wa habari Mjini Babati Mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo.
Muktasari:
- Watu hao 69 wamekamatwa katika mikoa saba nchini ikiwemo Dar es Salaam, Arusha, Morogoro, Iringa, Pwani, Mara na Kilimanjaro.
Babati. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini imesema imeishawatia mbaroni watuhumiwa 69 wanaojishughulisha na kilimo cha bangi na mirungi kwa kipindi cha Juni hadi Oktoba mwaka huu katika mikoa mbalimbali kinyume na sheria za nchi.
Taarifa za kunaswa wananchi wanaolima bangi na mirungi zilitolewa na Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo, Aretas Lyimo wakati akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 31 mjini Babati mkoani Manyara.
Lyimo amesema wamejipanga kufanya operesheni mikoa yote na kuendelea kutoa elimu kwa kuwa mikoa yote nchini inalima bangi na mirungi.
Hata hivyo, amesema kwa operesheni ambazo wameishafanya Arusha walikamata watu 19, Kilimanjaro 11, Morogoro 19, Iringa tisa, Mara 11 na mikoa ya Dar es Salaam na Pwani hakutaja idadi licha ya operesheni kufika.
"Operesheni zinaendelea Nchi nzima tutashirikiana na viongozi kuanzia ngazi ya vitongoji hadi Taifa ili kuhakikisha dawa za kulevya hazilimwi hapa nchini," amesema Lyimo.
Kamishna jenerali huyo amesema watazishirikisha mamlaka za maji na mabonde ya maji kwa kuwa wananchi ndiyo wanalima dawa za kulevya kwenye vyanzo vya maji.
Amesema awali walipoanza operesheni walianza na dawa za kulevya za viwandani zikiwemo Heroine na Cocaine ila walifanikiwa kuzidhibiti kwa kiasi kikubwa.
"Bangi na mirungi bado ni tatizo kubwa Tanzania na inalimwa mikoa yote hapa nchini jamii na serikali tuipige vita dawa za kulevya kwa nguvu zote," amesema Lyimo.
Amesema baada ya mamlaka hiyo kufanikiwa kudhibiti matumizi ya dawa za viwandani sasa watu wengi walipokosa dawa za viwandani sasa wamegeukia bangi na mirungi.
"Tutashirikiana na wazazi na walezi kupambana na dawa za kulevya maana watoto wakitumia wanakosa maadili na kuanza kuwatukana wazazi," amesema Lyimo.
Amesema madhara ya kutumia bangi na mirungi hayaishii kwa watumiaji tu bali yanawafikia watu wengine ndiyo maana wanataka watokomeze uuzaji wa dawa kwa asilimia 80.
Amesema sheria inakataza kilimo cha bangi na mirungi mtu anayebainika kuilima adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 au kifungo cha maisha jela.
Amefafanua kuwa wapo watu wanasema kwanini kilimo cha bangi na mirungi kisiruhusiwe kama nchi nyingine lakini anadai bangi inayolimwa nchi zingine ni tofauti na ya Tanzania kwa kuwa yao siyo kali ila ni kwa ajili ya dawa ila ya Tanzania inaharibu ubongo.
Mkazi wa Kata ya Bonga mjini Babati, Mariam Mkomba ameipongeza mamlaka hiyo kwa namna wanavyoendesha operesheni mbalimbali za kupambana na dawa za kulevya mikoa tofauti hapa nchini.