Adaiwa kukutwa na mirungi ndani ya treni

Muktasari:
- Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inatarajia kusikiliza mashahidi sita na vielelezo vitatu katika kesi ya dawa za kulevya aina ya mirungi zenye uzito wa kilo tano inayomkabili Mariam Makisa (54).
Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili Mariam Makisa (54) ya dawa za kulevya, umedai kuwa mshtakiwa huyo alikutwa ndani ya treni ya abiria akiwa akiwa na dawa za kulevya aina ya mirungi zenye uzito wa kilogramu tano.
Katika kesi ya msingi inadaiwa Mei19, 2023 ndani ya treni ya abiria mshtakiwa huyo alikutwa na dawa za kulevya zenye uzito wa kilo tano aina ya mirungi.
Akimsomea hoja za awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Oktoba 2, Wakili wa Serikali Erick Kamala amedai kuwa, Mei 19, 2023 mshtakiwa huyo alikutwa ndani ya treni ya abiria iliyokuwa ikisafiri kutoka Tanga kuelekea Moshi akiwa na dawa za kulevya aina ya mirungi zenye uzito wa kilo tano.
Inadaiwa kuwa mshitakiwa huyo alikutwa na dawa hizo mara baada ya jeshi la polisi kufanya ukaguzi ndani ya treni hilo na alipohojiwa alikiri kukutwa na dawa hizo ambapo askari polisi hao walimkamata.
"Septemba 4, 2023 mshitakiwa huyo alifikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka yanayomkabili," amedai Kamala.
Wakili Kamala alidai wanatarajia kuwa na mashahidi sita na vielelezo vitatu vitakavyorumika katika ushahidi huo.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo baada ya kusomewa hoja za awali alikiri kuwa jina lake, umri wake na eneo analoishi lakini shtaka linalomkabili la kusadirisha dawa za kulevya hizo alikana.
Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 16, 2023 kwa ajili ya usikilizwaji.