Kihongosi: Sitaruhusu kikwazo cha kuzuia maendeleo Arusha

Muktasari:
- Jukumu lake kubwa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kupitia usimamizi makini wa fedha na miradi inayotekelezwa na Serikali.
Arusha. Mkuu mpya wa Mkoa wa Arusha, Kenan Kihongosi amesema hatakubali kikwazo chochote kitakachozuia maendeleo ya wananchi wa mkoa huo, huku akisisitiza kwamba ajenda yake kuu ni kujenga imani ya wananchi kwa Serikali na kuharakisha maendeleo.
Akizungumza leo Jumatatu Juni 30, 2025, wakati wa makabidhiano ya ofisi kati yake na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda, Kihongosi amesema kuteuliwa kwake na Rais Samia Suluhu Hassan ni dhamana ya kuwatumikia wananchi, hivyo amewaomba watumishi na wananchi wa Arusha ushirikiano ili kusukuma mbele ajenda ya maendeleo.
“Rais aliponiteua aliniagiza kazi maalumu na alizungumza hadharani. Sina sababu ya kurudia maneno yake, ila ninamaanisha sitaruhusu kikwazo chochote kitakachozuia maendeleo ya wananchi,” amesema Kihongosi.
Ameongeza kuwa jukumu lake kubwa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kupitia usimamizi makini wa fedha na miradi inayotekelezwa na Serikali.
“Ajenda yetu ni wananchi kuwa na imani na Serikali. Fedha zinaletwa, miradi inajengwa na wajibu wetu ni kusimamia kikamilifu hadi kukamilika,” amesema Kihongosi.
Amewaomba watumishi kufanya kazi kwa umoja na uaminifu, akiwakumbusha kuwa nafasi walizonazo ni dhamana waliyopewa kwa niaba ya wananchi.
Aidha, ametumia fursa hiyo kumpongeza Makonda kwa kazi kubwa aliyoifanya Arusha.
Amesisitiza umuhimu wa kuishi kwa upendo, akihimiza watu kuepuka kugombana, kuumiza wengine, kuwasema vibaya au kupanga mabaya dhidi ya wenzao.
“Mungu kila mmoja amemuandikia nafasi yake. Huna sababu ya kugombana au kuumiza watu. Tumuachie Mungu atimize alichopanga,” amesema.
Akizungumza na baadhi ya wananchi waliojitokeza kushuhudia makabidhiano hayo, Kihongosi amewakumbusha namna alivyoshirikiana nao ikiwemo katika ujenzi wa shule alipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha na kuwaomba waendeleze ushirikiano huo.
“Asitokee mtu akawaambia msishirikiane na Serikali yenu. Serikali ndiyo jicho na msaada wa mwisho kwa wananchi,” amesema.
Makonda amewashukuru wananchi kwa ushirikiano waliompa wakati wa uongozi wake. Pia amewashukuru viongozi wa dini kwa kumuombea, hasa wakati alipokuwa anaumwa.
Amekiri kupitia kipindi kigumu cha kuumwa na akasema ipo siku ataeleza kwa undani kilichotokea. “Wengine walitangaza mpaka msiba, lakini Mungu anajua kwa nini niko hai leo,” amesema.
Makonda ambaye kwa sasa ameomba ridhaa ya kuwania ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini kwa tiketi ya CCM, amewaomba wananchi kumuunga mkono Kihongosi kwa ushirikiano mkubwa.
Pia amemshauri Kihongosi kumtanguliza Mungu katika majukumu yake ili aweze kutoa haki na kuleta ustawi.
“Shirikiana na kila mtu. Wananchi wa Arusha wana mawazo mazuri. Yapokee na uyapange kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu. Sina shaka nawe,” amesema Makonda.