Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Samia ataja sababu kumteua Sirro, atoa maagizo kwa viongozi wapya

Muktasari:

  • Balozi Simon Sirro alikuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) tangu Mei 28, 2017 na alistaafu Julai 20, 2023 baada ya kukaa katika wadhifa huo kwa kipindi cha miaka mitano, baada ya kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametaja sababu ya kumteua Balozi Simon Sirro kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma akisema ni sababu za kiusalama katika eneo hilo, huku akiitaja Ngorongoro kuwa ni pasua kichwa.

Sambamba na hilo, Rais ametoa maagizo kwa viongozi mbalimbali aliowateua akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Mhandisi Machibya Masanja.

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Jumamosi, Juni 28, 2025 wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali walioteuliwa Juni 24, katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino, jijini Dodoma.

Amesema katika uteuzi wake ameteua wakuu wa mikoa watano pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Simon Sirro.

“Wanne kati yao ni vijana mliopikwa ndani ya Umoja wa VIjana wa Chama cha Mapinduzi, kwa hiyo sina wasiwasi nanyi tumeangalia utendaji wenu tumewafuatilia kwa karibu, tumeona kipindi hiki hatuna haja ya kutoa watu nje kuleta huku tumeona tuwapandishe muendeleze mifumo kwa waliotoka.

“Mkoa wa Kigoma ni wa kimkakati, unaopakana na nchi jirani ni wenye mambo mengi. Kwa hiyo tumetoa pale Kamanda wa Polisi, tunakurudisha Kamanda wa Polisi lakini kamanda wewe umechanganya na ujuzi wa diplomasia, nimekuona utafaa kwenye mkoa ule, najua nimeshakutumia sana kama IGP, Balozi lakini bado nakuona nenda kafanye kazi,” amesema Rais Samia.

Katika hatua nyingine amemtaka mkuu mpya wa Mkoa wa Arusha, Kenan Kihongosi, kuhakikisha anawaunganisha wananchi wa mkoa huo na kuendeleza kasi ya utendaji aliyoionyesha akiwa Simiyu.

“Muda mfupi nilikuwa kwenye mkoa wako Simiyu, nimeona kazi nzuri uliyoifanya. Na kwa sababu Mkuu wa Mkoa wa Arusha (Paul Makonda) amejiuzulu ili kuingia kwenye kinyang’anyiro, nimekuhamisha kutoka Simiyu kwenda Arusha. Najua Arusha unapajua vizuri, nguvu uliyoitumia Simiyu nenda kaitumie Arusha. Najua unaweza kawaunganisha wana Arusha,” amesema.

Uteuzi wa Kihongosi umefanyika baada ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, kuchukua fomu ya kuwania ubunge, hatua iliyomlazimu kuachia wadhifa huo serikalini.


Atoa maagizo TRC

Pamoja na hayo Rais amempa maagizo Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Machibya akimtaka kwenda kukamilisha kazi iliyoachwa na Masanja Kadogosa.

Amesema TRC kuna kazi kuu mbili akiwataka kutoka kwenye fikra za miundombinu peke yake na kwenda kibiashara zaidi akisema SGR inajengwa kwa uwezo wetu na kwamba nchi itakwenda hivyo na misaada.

“Kazi yangu na wenzangu ni kutafuta fedha ili kazi hii iendelee tunataka kufikia 2030, kilomita zaidi ya 2000 ziwe zimekamilika. Tuwe tumeshajiunga na Burundi tuingie huko, nenda kasimamie operesheni zote kama tulivyokubaliana,” amesema.

Pia, amemtaka kuhakikisha TRC wanaingiza sekta binafsi kwani shirika hilo haliwezi kwenda bila sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu na usafirishaji mizigo, akiwataka wafikirie kwa upana zaidi.

Amesema maeneo kadhaa yanataka kufanyiwa marekebisho, akimtaka kwenda kusimamia pia kuondoa mlolongo mrefu wa tenda kwani masuala ya reli na bandari ndiyo kila kitu katika biashara.

Pia, Rais alifanya uapisho kwa viongozi aliowateua kipindi cha hivi karibuni, akitoa maagizo kwa viongozi wa Ngorongoro na kuwataka kwenda kumwakilisha ipasavyo.

“Ngorongoro ni pasua kichwa, mpaka mwenyekiti analalamika unanibadilishia watu kila siku, nawaambia sijampata ninayemtaka anisaidie kwa imani yangu utanisaidia,” amesema.

Rais Samia amesema anahitaji kuona uongozi mpya unabainisha maeneo yanayotakiwa kubaki kwa ajili ya uwekezaji na mengine kwa ikolojia na maeneo mengine wapewe watu wanaoweza kufanya uwekezaji.

“Katunze ikolojia, pia kuna mgogoro na wenyeji kwa sheria zetu wenyewe wanyeji sasa wamezidi, ng’ombe, mbuzi, kondoo na wanyama wafugwao ndiyo wamejaa kuliko wanyama wa mwituni wanaoleta utalii.

“Ngorongoro ni mrithi wa dunia, tukiharibu dunia haitatusamehe kama kuna miiba yoyote ndani toa, najua kuna watu wamelowea hapo na wasingependa kuona mgeni ameingia hapo,” amesema.

Pia, Rais Samia ametoa maagizo kwa viongozi wengine aliowateua akiwemo Annamringi Macha aliyempeleka Simiyu, akitaka aende akaendeleze mazuri aliyoyaanzisha Kihongosi.

Pia, alimtaka Mkuu mpya wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, Mboni Mhita Mkuu mpya wa Mkoa wa Shinyanga na Mkuu mpya wa Mkoa wa Songwe Jabiri Omary Makame na Katibu Tawala wa mkoa huo Dk Frank Hawasi.

“Songwe si parahisi sana, nendeni mkasaidiane kwa karibu, sitaki kusikia kuna migongano kwenu au kwa mnaowakuta kama kuna shida tumieni busara kutatua.”

Rais Samia aliwataka wakuu wote wa mikoa kusimamia amani na usalama kwenye maeneo yao, kwani wao ndiyo wenyeviti wa ulinzi na usalama kwenye maeneo yao, hasa kipindi hiki ambacho nchi inakwenda kwenye uchaguzi.

“Kuna chokochoko zinaweza kutokea, nataka mkasimame imara tunakwenda kwenye mchakato wa uchaguzi, nendeni kama makamishna mkahakikishe mikoa inakwenda salama,” amesema.

Ameagiza waende wakasimamie fedha za miradi ya serikali, na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa thamani ya fedha inayopelekwa na serikali kwa ajili ya kutatua shida za Watanzania na si vinginevyo, huku akiwataka kwenda kukuza mapato na kuwasikiliza wananchi.

Pia ametoa maagizo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena kwa kuanza kumpa hongera na pole, akisema amefanya kazi nzuri alipokuwa awali.