Kicheko ujenzi wa kilometa 12.8 za barabara Ilemela

Muonekano wa barabara ya Buswelu-Nyamadoke-Nyamhongolo Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza yenye urefu wa kilometa 9.5 inayotarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami. Picha na Mgongo Kaitira
Muktasari:
Barabara hizo zinazojengwa kwa kiwango cha lami ziko katika Kata za Buswelu, Nyamhongolo na Nyakato ambapo ujenzi wake unatarajiwa kuanza Novemba 20, 2023 na kukamilika Januari 22, 2025.
Mwanza. Zaidi ya Sh23.4 bilioni zinatarajiwa kutumika kutekeleza mradi wa ujenzi wa barabara tofauti zenye urefu wa jumla ya kilometa 12.8 katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza.
Barabara hizo zinazojengwa kwa kiwango cha lami ziko katika Kata za Buswelu, Nyamhongolo na Nyakato ambapo ujenzi wake unatarajiwa kuanza Novemba 20, 2023 na kukamilika Januari 22, 2025.
Mradi hiyo inayotekelezwa na Kampuni ya Nyanza Road Works Limited chini ya usimamizi wa Mkandarasi Mshauri wa Kampuni ya Nimeta Consults Limited unatekelezwa kwa fedha za mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia (WB) kupitia mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya miji Tanzania (TACTIC).
Akizungumza leo Jumatatu Oktoba 23, 2023 wakati wa hafla ya kukabidhi mradi kwa mkandarasi, Mratibu wa TACTIC Manispaa ya Ilemela, Juma King’ora ametaja barabara itakazojengwa kupitia mradi huo kuwa ya Buswelu-Nyamadoke-Nyamhongolo yenye urefu wa kilometa 9.5.
Mratibu huyo aliyezungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Manispaa ya Ilemela, Kiomoni Kibamba ametaja barabara nyingine kuwa ni ya Buswelu-Busenga-Kiwanda cha Coca Cola Nyakato yenye urefu wa kilometa 3.3.
‘’Kukamilika kwa barabara hizo kutaboresha na kurahisisha mawasiliano kwa wananchi kwa kumaliza changamoto ya kukosa usafiri wa umma, hasa nyakati za masika kwa mabasi madogo ya abiria maarufu kama daladala kukatisha safari kutokana na ubovu wa barabara,’’ amesema King’ora
Manispaa ya Ilemela ambayo ni miongoni mwa Halmashauri 11 nchini zinazoanza utekelezaji wa mradi wa TACTIC awamu ya kwanza (Tie 1) itatekeleza mradi wa ujenzi wa Soko la Kirumba na barabara zinazoizunguka zenye urefu wa kilometa 2.9. Utekelezwaji mradi huo unatarajiwa kuanza Januari, 2024.
Halmashauri nyingine iliyo katika mradi wa TACTIC ni Jiji la Arusha, Dodoma, Mbeya, Mwanza, Manispaa ya Kigoma, Songea, Sumbawanga, Tabora na Halmashauri ya Mji Geita.
Miongoni mwa sifa zilizozipa miji na majiji hayo fursa ya kuwemo kwenye mradi huo ni wingi wa idadi ya watu na kasi ya ukuaji.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala, Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Fatma Msengi amemtaka mkandarasi kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati huku akionya kuwa Serikali itafuatilia kwa karibu utekeleza na haitasita kuchukua hatua stahiki itakapobidi.
“Serikali imekamilisha mahitaji yote muhimu ikiwemo kulipa fidia kwa wananchi kupisha mradi; hatutavumilia ucheleweshwaji usio na sababu za msingi,’’ amesema na kuonya Msengi
Mhandisi Mkadiriaji Majenzi kutoka kampuni ya Nyanza Road Works Limited, Maro Juma ameahidi kutekeleza mradi huo kwa wakati kwa mujibu wa mkataba huo huku akiwaomba wananchi kwenye maeneo ya mradi kutoa ushirikiano uanohitajika.
Madiwani wachelekea
Diwani wa Kata ya Buswelu, Sara Ngw’ani amesema utekelezwaji wa mradi huo siyo tu utaboresha na kurahisisha mawasiliano, bali pia umejibu kilio cha muda mrefu cha wananchi kuhusu ubovu wa barabara za kata hiyo.
“Ubovu wa barabara hizi ni miongoni mwa kero tunazokutana nazo kila tukifanya mikutano, mradi huu utapunguza malalamiko ya wananchi,” amesema Ng’wani.
Kauli kama hiyo pia imetolewa na Diwani wa Kata ya Nyakato, Jonathan Mkumba akiishukuru Serikali kwa kutmiradi ya sekta ya afya na maji.
Wananchi watoa ya moyoni
Stella Alloyce, mkazi wa Busenga amesema utekelezaji wa mradi huo utawaondolea wananchi adha ya kukosa huduma muhimu ikiwemo ya magari ya wagonjwa ambayo kwa sasa hayawezi kufika eneo hilo kutokana na ubovu wa barabara.
‘’Kwa sasa tunalazimika kutumia usafiri wa pikipiki kuwasogeza wagonjwa hadi eneo linalopitika pindi tunapokuwa na wagonjwa wanaohitaji huduma ya gari la wagonjwa kukimbizwa hospitali. Wajawazito, wazee na watoto ni miongoni mwa makundi yanayoathirika zaidi wakati wa dharura ya kiafya,’’ amesema Stella
Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Daladala Mkoa wa Mwanza, Mjalifu Manyasi amepongeza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara hizo kwa kiwango cha lami akisema kutawaondolea adha ya uharibifu wa magari kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara.