KESI YA MAUAJI INAYOWAKABILI ASKARI POLISI MTWARA: Mahakama yazungumzia utata uchukuaji sampuli za mama wa marehemu

Muktasari:
- Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, licha ya kubainisha utata uliopo kuhusu mchukuaji wa sampuli za mate ya Hawa Ally ambaye ni mama mzazi wa mafanyabiashara wa madini marehemu Mussa Hamis, imekubali vielelezo vilivyoletwa mahakamani na shahidi namba 10 upande wa Jamhuri, viweze kupokelewa.
Mtwara. Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara imebainisha kuwepo kwa utata kuhusu nani aliyechukua sampuli za mate ya mama wa aliyekuwa mfanyabiashara na mchimba madini, Mussa Hamis kwa ajili ya vipimo vya vinasaba.
Hata hivyo Mahakama hiyo imesema kuwa utata huo hauwezi kuathiri upokeaji wa fomu ya haki na ridhaa ya mama huyo, Hawa Ally, kuwa kielelezo cha upande wa mashtaka katika ya mauaji mchimba madini huyo inayowakabili maofisa saba wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara.
Jaji Edwin Kakolaki anayesikiliza kesi hiyo, amebainisha hayo katika uamuzi wake wa pingamizi lililowekwa na mawakili wa utetezi katika kesi hiyo, ambao walipinga fomu hiyo inayoonyesha kuwa mama huyo alielezwa haki zake na kuhakikishiwa kulindwa na kuridhia kuchukuliwa sampuli hizo, isipokewe kuwa kielelezo cha upande wa mashtaka.
Jana mawakili hao wa utetezi katika kesi hiyo kupitia kwa kiongozi wa jopo lao, Majura Magafu waliipinga fomu hiyo ambayo shahidi wa 10 wa upande wa mashtaka aliomba kuitoa, wakidai kuwa hana mamlaka ya kuitoa kwani siye aliyechukua sampuli hizo kutoka kwa mama huyo kama alivyodai.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara (OC- CID), Mrakibu wa Polisi (SP), Gilbert Sostenes Kalanje; aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Maurice Onyango.
Wengine ni aliyekuwa Ofisa Intelijensia ya Jinai Wilaya (DCIO) Mtwara ASP Nicholaus Stanslaus Kisinza; Mkaguzi Msaidizi (A/Insp) Marco Mbuta Chigingozi; Mkaguzi (Insp) John Yesse Msuya, aliyekuwa Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara; A/Insp. Shirazi Ally Mkupa na Koplo Salim Juma Mbalu.
Wanadaiwa kumuua kwa makusudi Mussa Hamis Januari 5, 2022 katika Kituo cha Polisi Mitengo, Wilaya ya Mtwara, Mkoa wa Mtwara, na kwenda kuutupa mwili wake katika Kijiji cha Majengo, Kata ya Hiari karibu na kiwanda cha simenti cha Dangote.
Wanadaiwa kumuua kwa kumziba mdomo na pua kwa kutumia tambala, baada ya kumchoma sindano ya dawa ya usingizi, ili asiendelee kuwadai pesa na mali zake walizozichukua, walipokwenda kumpekua nyumbani kwake, Kijiji cha Ruponda, wilayani Nachingwea, Mkoa wa Lindi wakimtuhumu wizi wa pesa na pikipiki.
Shahidi huyo wa 10, Mkemia wa Serikali kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) Kanda ya Kusini Mtwara, Abdillahi Mustafa ameieleza Mahakama kuwa ndiye aliyechukua sampuli za mama huyo na kuzipeleka Dar es Salaam pamoja na mifupa hiyo kwa uchunguzi wa vinasaba.
Baada ya maelezo yake aliiomba Mahakama hiyo ipokea fomu aliyoijaza ikionyesha mama huyo kukiri kuwa alielezwa haki zake kabla ya kuchukuliwa sampuli hizo na kuridhia kuchukuliwa sampuli, iwe kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.
Lakini mawakili wa utetezi wakaibua pingamizi wakidai kuwa shahidi huyo hana mamlaka ya kuitoa (kuiwasilisha mahakamani) fomu hiyo ili ipokewe na kuwa kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka wakidai kuwa si yeye aliyemchukua sampuli hizo kutoka kwa mama huyo.
Badala yake walidai kuwa kwa ushahidi wa vielelezo vya upande wa mashtaka, sampuli hizo zilishachukuliwa na zilikuwa zimehifadhiwa katika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Mtwara na kwamba shahidi huyo yeye alipelekewa tu.
Mawakili wa Serikali walipinga hoja hiyo ya upande wa utetezi, pamoja na hoja nyingine wakidai kuwa msingi wa ustahili wa shahidi kuwasilisha kielelezo mahakamani hujengwa na ushahidi wake wa mdomo, na si maudhui ya nyaraka nyingine kama walizotumia mawakili wa utetezi.
Hata hivyo, katika uamuzi wake, Jaji Kakolaki amekubaliana na hoja ya utetezi kuwa kulingana barua ya RCO Mtwara pamoja na fomu yake ya makabidhiano ya vielelezo (PF180), hazitoi mwanga wala maelezo ya nani alichukua sampuli hizo kutoka kwa mama huyo.
Jaji huyo ameeleza kuwa baada ya kupitia hoja za pande zote inakubaliana na Wakili Magafu kuwa kabla ya kielelezo kupokewa, lazima kiangaliwe kama kimekidhi sifa zote za kustahili kupokewa.
Kwa Mujibu wa Jaji Kakolaki, vigezo hivyo ni kwanza, kama kina uhusiano na shauri, kama kinakusudia kujibu hoja bishaniwa na kama kinakidhi matakwa ya kisheria na kama mtoa kielelezo mwenyewe pia anakidhi matakwa ya kisheria, ikiwa ni pamoja na kuwa na ufahamu nacho.
Baada ya kutaja sifa hizo Jaji Kakolaki amesema kuwa ni wazi fomu hiyo inakidhi kigezo cha kwanza cha kuwa na uhusiano na shauri kwani inakusudia kujibu hoja kama sampuli za Hawa zilichukuliwa, pia inakusudia kuthibitisha kuwa sampuli ilichukuliwa kwa Hawa na kwa utashi wake.
Kuhusu ustahilifu wake, amesema kuwa baada ya kuangalia nyaraka zilizoongelewa yaani kielelezo cha 10 cha upande wa mashtaka (barua ya RCO na Fomu ya Polisi ya Makabidhiano ya vielelezo), kuna utata wa nani alichukua sampuli hizo.
"Mahakama hii imefikia uamuzi kwamba suala la nani alichukua sampuli hiyo, (nyaraka hizo, barua ya RCO na PF180) halitoi mwanga au maelezo yoyote kwamba ni nani alichukua na kwa ridhaa ya nani,” amesema Jaji Kakolaki.
Hata hivyo amesema kuwa Mahakama haioni ni kwa jinsi gani kielelezo hicho namba 10 (barua ya RCO na PF180), kinaweza kuathiri msingi wa upokeaji fomu hiyo ambao kimsingi ulitolewa kwa mdomo na shahidi.
Hivyo amesema kwamba hoja ya nani aliwasilisha sampuli ile au ni nani aliyemwakilisha mtoa sampuli (Hawa) mbele ya shahidi namba 10 Mahakama inaona kwa sasa haviwezi kutumika kuamua kama fomu hiyo ipokelewe au isipokewe maana nyaraka hizo zinakinzana.
"Kwa hiyo Mahakama inaona suala hilo haliwezi kuamuliwa kwa sasa (katika hatua ya upokewaji wa kielelezo hicho), mpaka itakapopata ushahidi mwingine," amesema Jaji Kakolaki na kuhitimisha hoja hiyo, huku akiongeza kusema.
"Kwa kuwa shahidi alielezea kwa mdomo msingi (wa upokeaji kielelezo hicho), hivyo Mahakama hii inaona kuwa kwa sasa kielelezo hicho kinastahili kupokelewa na shahidi ana ufahamu nacho maana alikifanyia kazi. Mahakama hii inaona hoja za pingamizi hazina mashiko na inaitupilia mbali."
Alichokieleza shahidi wa 10
Kwa mujibu wa ushahidi wake akiongozwa na Mwendesha Mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Pascal Marungu, Januari 24, 2022 akiwa zamu kwenye dawati la kupokea sampuli na vielelezo na kuchukua sampuli, alipokea vifurushi vinne vyenye vielelezo kutoka ofisi ya RCO Mtwara, vilivyowasilishwa na Inspekta Adelina.
Alibainisha kuwa Vielelezo hivyo, viliambatana na barua kutoka kwa RCO Mtwara, aliyoandikiwa meneja wa GCLA, Kanda ya Kusini Mtwara pamoja na PF180 (fomu ya Polisi ya kukabidhia vielelezo vya kesi).
Shahidi huyo alivitaja vielelezo hivyo vilivyokuwa vimefungwa ndani mifuko na ‘nylon’ na kuwekwa ndani ya bahasha za khaki na kufungwa kwa lakiri za Jeshi la Polisi zenye rangi nyekundu kuwa kifurushi A kilikuwa na mbavu nane zilizodhaniwa kuwa za binadamu.
Kifurushi B kilikuwa na mifupa miwili iliyodhaniwa kuwa ya mguu wa kulia wa binadamu, C walikuwa ni funza na D ilikuwa suruali na kwamba baada ya kuvikagua alivisajili kwenye kitabu cha kupokelea vielelezo na kuvipa namba ya usajili ya maabara.
"Pia aliletwa mama mmoja ambaye alijitambulisha kwa jina la Hawa Bakari Ally kwa ajili ya kuchukuliwa sampuli zitakazochunguzwa na kulinganisha na kielelezo A (mifupa ya mbavu), B (mifupa ya mguu) na D (suruali)," alidai shahidi huyo.
Aliongeza kuwa alimweleza huyo mama kuwa amepelekwa kwake kuchukuliwa sampuli ili kusaidia kwenye uchunguzi wa vielelezo vya mbavu nane, mifupa ya mguu na suruali zinazodhaniwa kuwa ni za binadamu aliyetajwa kwenye barua ya RCO kuwa ni Mussa Hamis Hamis.
"Pia nilimueleza kwamba lengo la kuchukuliwa sampuli ni ili kutambua ukweli kama vinasaba vya vielelezo hivyo vitahusiana na vinasaba kutoka kwenye sampuli zake, ili kubaini kuwa vielelezo hivyo ni vya mtoto wake Mussa", alidai na kuongeza:
"Huyo mama alisema yuko tayari kuchukuliwa sampuli kama atakavyoelekezwa. Nilimhakikishia kuwa sampuli hizo ni kwa ajili ya uchunguzi huo tu na si kwa ajili nyingine. Pia nilimweleza kwamba yeye ndiye mmiliki halali wa sampuli hizo na tutazichukua kwa ridhaa yake.
Alidai kuwa baada ya mama huyo, Hawa, kuridhia kuchukuliwa sampuli hizo na kama alichukua fomu ya haki na uthibitisho wa ridhaa kwa mujibu wa Sheria ya Vinasaba vya Binadamu namba 8 ya mwaka 2009 akampa akasaini.
Alichokisema Wakili Magafu
Pamoja na hoja nyingine za kupinga fomu hiyo, Wakili Magafu amedai kuwa wanapinga fomu hiyo isipokelewe kwa kuwa haijawekewa msingi sahihi na upande wa mashtaka ili iweze kupokelewa.
"Shahidi huyu kwa mujibu wa ushahidi wake hakuwahi kuchukua sampuli ya mpanguso wa kinywa kutoka kwa Hawa Bakari Ally," amedai Wakili Magafu.
Amefafanua kuwa wakati shahidi huyo anatoa ushahidi wake, alitaka uungwe mkono na kielelezo cha 10 (barua ya RCO kwenda ofisi y GCLA Mtwara, ya Januari 24, 2022.
Wakili Magafu amedai kuwa kwa mujibu wa barua hiyo tayari katika ukurasa wa tatu alipelekewa sampuli za mpanguso wa kinywa wa Hawa Bakari Ally.
Ameongeza kuwa barua hiyo pia ilikuwa imeambatanishwa fomu ya Polisi namba 180 (PF180), fomu ya makabidhiano ya vielelezo) ambayo kwenye koramu ya pili inaonyesha kuwa RCO, ameambatanisha sampuli iliyochukuliwa kwa Hawa Bakari Ally ambayo ni mpanguso wa kinywa (mate).
"Mheshimiwa kutokana na hali hiyo sampuli anazodai shahidi kuzichukua Januari 24, tayari zilishachukuliwa na zilikuwa ofisini kwa RCO na sasa anamtuma Inspekta Adelina azipeleke kwa shahidi na si kwamba zilichukuliwa na shahidi," amesisitiza Wakili Magafu.
Majibu ya Serikali
Akijibu hoja, Wakili wa Serikali, Marungu amedai kuwa shahidi ameweka msingi vizuri tangu mwanzo wakati anaanza ushahidi wake mpaka kufikia kutoa kielelezo hicho.
Amedai kuwa shahidi alielezea jinsi alivyompokea Hawa Bakari Ally na alivyomwelezea kusudio lake na lengo la kumchukua sampuli, haki zake na kwamba mmiliki wa hizo sampuli ni yeye tu na Hawa akampa jibu kuwa yuko tayari kuchukuliwa sampuli, akasaini fomu hiyo, pamoja na yeye shahidi.
Amedai kuwa kuhusianisha barua zinazoonyesha kuwa shahidi alipelekewa sampuli zile si hoja ya msingi kwa kuwa Wakili Magafu alitumia maudhui ya nyaraka nyingine (barua ya RCO) kupinga upokewaji wa nyaraka hiyo.
Hivyo Wakili Marungu amedai kuwa msingi wa kielelezo hujengwa kwa ushahidi wa mdomo wa shahidi.
Hata hivyo, Wakili Magafu amesisitiza hoja yake hiyo na kutoa ufafanuzi zaidi.
Kesi hiyo bado inaendelea, katika hatua ya maswali ya dodoso.