KESI YA MAUAJI INAYOWAKABILI ASKARI POLISI MTWARA: Mahakama yaamuru mifupa inayodaiwa ya marehemu iendelee kuhifadhiwa
Muktasari:
- Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara imehitimisha kikao cha kwanza cha usikilizwaji wa kesi ya mauaji ya aliyekuwa mfanyabiashara na mchimba madini, Mussa Hamis huku ikiamuru mifupa inayodaiwa kuwa ya marehemu huyo, iendelee kuhifadhiwa kwa matumizi ya mahakama licha ya mama wa marehemu Mussa Hamisi kuomba apewe mabaki hayo.
Mtwara. Licha ya mama wa aliyekuwa mfanyabiashara na mchimba madini, marehemu Mussa Hamis kuomba apewe mabaki ya mifupa inayodaiwa kuwa ya marehemu mwanaye, Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara imeelekeza mifupa hiyo iendelee kuhifadhiwa.
Mahakama hiyo imetoa maelekezo hayo leo Ijumaa Desemba Mosi, 2023, baada ya kuhitimisha kikao cha kwanza cha usikilizwaji wa kesi ya mauaji ya mchimba madini huyo inayowakabili maofisa saba wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mtwara.
Mama huyo aliomba akabidhiwe mabaki ya mifupa hiyo wakati alipotoa ushahidi wake, Novemba 14, 2023, akiwa shahidi wa kwanza katika kesi hiyo.
Katika maelekezo hayo Mahakama hiyo imeelezwa mifupa hiyo ihifadhiwe katika Ofisi za Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) Kanda ya Kusini Mtwara, ambalo ndiko imesema kuwa ni mahali sahihi na salama.
Kesi hiyo namba 15 ya mwaka 2023 inasikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki, kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara (OC- CID), Mrakibu wa Polisi (SP), Gilbert Sostenes Kalanje; aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara, (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Maurice Onyango.
Wengine ni aliyekuwa Ofisa Intelijensia ya Jinai Wilaya (DCIO) Mtwara ASP Nicholaus Stanslaus Kisinza; Mkaguzi Msaidizi (A/Insp) Marco Mbuta Chigingozi; Mkaguzi (Insp) John Yesse Msuya, aliyekuwa mganga mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara; A/Insp. Shirazi Ally Mkupa na Koplo Salim Juma Mbalu.
Wanadaiwa kumuua kwa maksudi Mussa Hamis Januari 5, 2022 katika kituo cha Polisi Mitengo Wilaya ya Mtwara, Mkoa wa Mtwara, na kwenda kuutupa mwili wake katika kijiji cha Majengo Kata ya Hiari karibu na kiwanda cha Sementi cha Dangote.
Wanadaiwa kumuua kwa kumziba mdomo na pua kwa kutumia tambala, baada ya kumchoma sindano ya dawa ya usingizi, ili asiendelee kuwadai pesa na mali zake walizozichukua walipokwenda kumpekua nyumbani kwao, kijiji cha Ruponda wilayani Nachingwea, Lindi; wakimtuhumu wizi wa pesa na pikipiki.
Mifupa hiyo ni mbavu nane pamoja na miwili ya mguu wa kulia, iliwasilishwa mahakamani hapo na shahidi wa tisa wa upande wa mashtaka, na kupokewa kuwa vielelezo vya upande wa mashtaka, Jumatano, Novemba 29, 2023.
Hoja ya utunzaji wa mifupa hiyo ilianza siku hiyo baada ya shahidi huyo wa tisa, Fidelis Charles Bugoye, Mkemia wa Serikali Mwandamizi, kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Makao Makuu Dar es Salaam.
Bugoye ndiye aliyefanya uchunguzi wa vinasaba vya mifupa hiyo iliyopatikana mahali.ambako.mwili wake ulitupwa baada ya kuuawa; na kulinganisha na vinasaba kwenye sampuli ya mate ya mama wa marehemu Mussa, Hawa Bakari Ally ambavyo vilioana.
Siku hiyo baada ya shahidi huyo kumaliza ushahodi wake kabla ya kesi kuahirishwa kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Maternus Marandu, baada ya shahidi wa tisa, aliwasilisha hoja ya utunzaji wa mifupa hiyo.
Wakili Marandu aliiomba Mahakama kuwa kwa vielelezo hivyo ni mabaki ya viungo vya binadamu vinapaswa kuhifadhiwa mahali maalumu wakati kesi hiyo itakapokuwa inaendelea mpaka hapo mahakama itakapotoa maelekezo mengine.
Wakili Marandu alipendekeza kuwa mahali sahihi ni ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali lakini akaomba kwa siku hiyo vipelekwe katika kituo cha Polisi kabla ya kesho askari Polisi kufanya utaratibu wa kuvihamisha kwenda kuvikabidhi ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Majura Magafu aliunga mkono kuwa ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ni mahali sahihi pa kuhifadhi vielelezo hivyo.
Hata hivyo Wakili Magafu alitahadharisha kuwa kulingana na unyeti wake vinatakiwa kukabidhiwa katika ofisi hiyo moja kwa moja badala ya kuvipeleka Polisi kwanza huku akitoa hoja kwamba shahidi aliyeviwasilishwa ndiye anapaswa kukabidhiwa avipeleke, tena kwa maandishi.
Wakati Wakili Magafu akitoa hoja hiyo Shahidi huyo, alikuwa ameshatoka nje ya ukumbi wa Mahakama baada ya kuhitimisha ushahidi wake.
Lakini hata askari Polisi pamoja na mmoja wa waendesha mashtaka walipokwenda kumuangalia nje hakupatikana, tayari alishaondoka eneo la Mahakama na hakupatikana kwenye simu.
Kutoka na hali hiyo ndipo Jaji Kakolaki akaelekeza vielelezo hivyo vibaki katika mikono ya Mahakama kwa leo hadi kesho utakapofanyika utaratibu mwingine.
"Kwa kuwa ni viungo vya binadamu vinahitaji kutunzwa kwa utu na mahali salama", amesema Jaji Kakolaki na kuongeza kuwa hivyo kwa siku hiyo vielelezo hivyo vibaki katika mikono ya Mahakama hadi hapo kesho itakapotoa maelekezo mengine kuhusu mahali pa kuvihifadhi.
Leo baada ya shahidi wa mwisho kumaliza ushahidi wake na kuhitimisha usikilizwaji wa kesi hiyo katika kikao hiki cha kwanza, Wakili Marandu akaikumbusha tena mahakama kuhusiana na utunzaji wa mifupa hiyo, baada ya kuwasilisha hoja ya kuiahirisha kesi hiyo hadi kikao kingine.
"Mheshimiwa Jaji huyu ndio shahidi wetu wa mwisho kwa session (kikao) hii na kwa vile leo ndio tarehe ya mwisho ya session tunaomba shauri hili lishirishwe mpaka hapo litakapangiwa tarehe nyingine na msajili kwa sababu bado tuna Mashahidi wengine."amesema Wakili Marandu na kuongeza:
"Hata hivyo pia tuna ombi lingine kuhusu exhibit PE6 (kielelezo cha sita cha upande wa mashtaka ambacho ni mbavu nane), PE7 (mifupa ya mguu) na PE8 (suruali ya marehemu)".
Ameongeza kusema; "Mara ya mwisho Mahakama ilisema vihifadhiwe na Mahakama lakini kwa kuwa sasa ni muda mrefu tunaomba mahamaka itoe order (amri) vihifadhiwe mahali salama kusuniri session ijayo."
Wakili Marandu amesema kuwa wanajua kuwa shahidi wa kwanza upande wa mashtaka, Hawa Bakari Ally ambaye ndiye mama wa marehemu aliomba akabidhiwe lakini akasema kwa ajili ya kutenda haki wanaomba masalia hayo yahifadhiwe ili kuweza kuendelea kutumika kwenye shauri hili.
Wakili Magafu alipopewa na na Mahakama kujibu hoja hizo mbili amesema kuwa hawana pingamizi kuhusu ahirisho la kesi hiyo mpaka kikao kingine lakini akaomba kikao kingine kitakapopangwe kipewe muda wa kutosha, yaani mrefu.
"Bado tuna mashahidi wengi na mpaka sasa tuko na shahidi wa 10 tu na ukiangalia idadi ya mashahidi wa upande wa mashtaka na wa utetezi bado ni wengi.", amesema Wakili Magafu.
Hata hivyo wakili Magafu alitahadharisha kuwa bado Mahakama haijfikia uamuzi wa mwisho kuwa mifupa ile ni ya Mussa Hamisi na hivyo inapaswa ikabidhiwe kwa mama yake na kwamba bado kuna ushahidi mwingine, hivyo isije kuleta mkanganyiko katika jamii.
Baada ya hoja hizo Jaji amewashukru mawakili wa.pande zote na wote waliowezeha kesi hiyo kufikia hapo pamoja na waandiaho wa habari kwa kuuhabarisha umma kujua kinachoendelea mahakamani katika kesi hiyo na wote waliokuwa wanafika kujisikiliza.
Na kuhusu vielelezo hivyo yaani mifupa hiyo amesema:
"Natoa maelekezo viwekwe sehemu salama ambako ni Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Kusini Mtwara. Basi naahirisha shauri hili mpaka kikao kingine kitakapopangwa ambapo mtajulishwa. Kwa muda wote huo washtakiwa mtaendelea kuwa mahabusu."
Katika kikao hiki cha kwanza cha usikilizwaji wa kesi hiyo kilichoanza Novemba 13, 2023 upande wa mashtaka umewaita mashahidi 10 waliotoa ushahidi wao kati ya mashahidi 72 wanaotarajiwa kuitwa na upande wa mashtaka (ingawa wanaweza kupunguza idadi hiyo kadri watakavyoona inafaa).
Pia upande wa mashtaka umewasilisha mahakamani jumla ya kielelezo 11 ikiwemo mifupa hiyo.