Prime
Kesi dhidi ya Lissu kunguruma tena leo?

Muktasari:
- Lissu anakabiliwa na kesi mbili za jinai ikiwemo ya uhaini, ambayo imekuwa ikiibua mvutano mkali baina ya mawakili wa pande zote kuhusiana na hatima ya upelelezi wake.
Dar es Salaam. Kesi mbili zinazomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, leo Jumanne Julai Mosi, 2025, zinaendelea kunguruma katika hatua tofauti.
Lissu anakabiliwa na kesi ya uhaini pamoja na ya kuchapisha taarifa za uwongo mitandaoni, katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu, zinazosikilizwa na mahakimu wawili tofauti.
Kesi hizo zote zimepangwa kuendelea leo mahakamani hapo katika hatua tofauti.
Wakati kesi ya uhaini imepangwa kutajwa kujua hatima ya upelelezi ulikofikia, kesi ya kuchapisha taarifa za uongo imepangwa kuendelea kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashitaka.
Kesi ya uhaini
Katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga, Lissu anakabiliwa na shitaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Anadaiwa Aprili 3, 2025 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Kesi hiyo imefunguliwa mahakamani hapo kwa ajili ya uchunguzi wa awali kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu ambayo ndio ina mamlaka ya kuisikiliza, baada ya upelelezi kukamilika.
Kila mara kesi hiyo inapotajwa imekuwa ikiibua mvutano mkali wa hoja baina ya mawakili wa pande zote kuhusiana na hatima ya upelelezi.
Kila mara upande wa mashitaka umekuwa ukiieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, maelezo ambayo upande wa utetezi haukubaliani nayo ukidai unachelewa na kuhoji sababu za kuchelewa kwa upelelezi wa shitaka ambalo liko wazi kulingana na maelezo yake.
Hata hivyo, mara ya mwisho kesi hiyo ilipotajwa mahakamani hapo Juni 16, 2025, Lissu aliieleza Mahakama kuwa japo ana jopo la mawakili takriban 30 anaowaamini uwezo wao lakini ameamua kujitetea mwenyewe katika kesi hiyo.
Aliieleza Mahakama kuwa amefikia uamuzi huo kutokana na kukosa ushirikiano na mawakili wake hasa katika kujadiliana kuhusiana na mwenendo wa kesi hiyo, akidai kuwa wananyimwa fursa hiyo na Jeshi la Magereza.
Pamoja na uamuzi huo wa kujitetea mwenyewe, pia Lissu aliwasilisha mahakamani hapo malalamiko mengi ya ukiukwaji wa haki aliodai kutendewa katika mahabusu ya Gereza la Ukonga anakohifadhiwa.
Hakimu Kiswaga alikubaliana na uamuzi wake wa kujitetea mwenyewe huku akielekeza kuwa malalamiko yake ya ukiukwaji haki zake Mahakama itayafanyia kazi kiutawala.
Kuhusu upelelezi wa kesi hiyo, upande wa mashitaka uliieleza Mahakama kuwa, jalada la upelelezi wa kesi hiyo ambalo awali liliwasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) lakini likarudishwa kwa ajili ya upelelezi zaidi, lilikuwa limesharejeshwa tena kwa DPP.
Kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga aliieleza Mahakama kuwa DPP alikuwa anaendelea kulipitia kabla ya kufikia uamuzi wa hatua inayofuata, na akaomba Mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo.
Baada ya mvutano baina ya Lissu na waendesha mashitaka, Hakimu Kiswaga aliahirisha kesi hiyo mpaka leo, huku akisisitiza upande wa mashitaka kutoa mrejesho wa hatima ya upelelezi huo.
Hivyo wakati kesi hiyo inatajwa leo, inatarajiwa upande wa mashitaka kuieleza Mahakama uamuzi alioufikia DPP baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa kwake, iwapo anaridhika nao kuwa unakidhi kujenga kesi na hivyo kuipeleka Mahakama Kuu kwa ajili ya kuanza usikilizwaji au laa.
Japo hoja hiyo ilipingwa vikali na jopo la mawakili wa Lissu; Mpale Mpoki (kiongozi wa jopo), Dk Rugemeleza Nshala, Peter Kibatala, Jeremiah Mtobesya, Jebra Kambole na Hekima Mwasipu, wakiiomba Mahakama iifute kesi hiyo, lakini Mahakama ilikubaliana na hoja na maombi ya upande wa mashitaka.
Kesi ya kuchapisha taarifa za uongo
Katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geoffrey Mhini, Lissu anakabiliwa na mashitaka matatu.
Katika mashitaka hayo yote anadaiwa kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa Youtube, kinyume na Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015, kifungu cha 16.
Katika mashitaka hayo, Lissu anadaiwa kumuhusisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutenguliwa kwa wagombea wa chama chake katika maeneo mbalimbali wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa, 2024.
Pia anadaiwa kuwatuhumu askari Polisi kuhusika katika wizi wa kura kupitia vibegi na majaji kutokutenda haki kwa madai ya kutaka wapate uteuzi wa Rais kuwa majaji wa Mahakama ya Rufani.
Anadaiwa kutenda makosa hayo Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaa, kwa nia ya kulaghai umma.
Kesi hiyo ilianza kusikilizwa katika hatua ya kutoa ushahidi Jumatatu Juni 16, 2025, ambapo shahidi wa kwanza wa upande wa mashitaka alianza kutoa ushahidi wake.
Shahidi wa kwanza katika kesi hiyo aliielekeza Mahakama namna alivyobaini matamshi ya Lissu kwenye picha mjongeo (video) kuwa na viashiria vya jinai.
Shahidi wa kwanza kufungua pazia ni Mkaguzi (Inspector) John (45). Inspekta John alieleza ni mwajiriwa wa Jeshi la Polisi alifanya kazi Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Dar es Salaam.
Alibainisha anafanya kazi kitengo cha upelelezi wa makosa ya mtandao, katika dawati la doria la mitandaoni, kama mpelelezi.
Katika ushahidi wake akiongozwa na mwendesha mashitaka, Wakili Katuga, Inspekta John alieleza Mahakama kuwa aliposikiliza maneno ya Lissu katika video hiyo ya ukubwa wa MB500 alibaini kuwa yalikuwa na viashiria vya jinai, kisha akaipakua.
Baada ya maelezo marefu, kabla ya kuhitimisha ushahidi wake upande wa mashitaka uliomba ushahidi wa shahidi huyo uharishwe ili kusubiri mtaalamu wa picha aje atoe ushahidi wake kwanza, ndipo shahidi huyo amalizie ushahidi wake.
Ingawa maombi hayo yalipingwa vikali na kiongozi wa jopo la mawakili wa Lissu, Mpale Mpoki pamoja na Wakili Peter Kibatala, hata hivyo Hakimu Mhini baada ya kusikiliza hoja za pande zote alikubaliana na maombi ya upande wa mashitaka.
Hivyo aliahirisha kesi hiyo mpaka leo itakapoendelea kwa ushahidi wa shahidi wa pili, kabla ya shahidi wa kwanza kumalizia ushahidi wake.