Kaya zaidi ya 28,000 zakabiliwa na upungufu wa chakula Monduli
Muktasari:
Kaya 553 za wilaya ya Monduli, Mkoa wa Arusha zimepewa msaada wa mahindi tani 12 ili kukabiliana na njaa kutokana na uhaba mkubwa wa chakula ulitokana na ukame.
Monduli. Kaya 553 za wilaya ya Monduli, Mkoa wa Arusha zimepewa msaada wa mahindi tani 12 ili kukabiliana na njaa kutokana na uhaba mkubwa wa chakula ulitokana na ukame.
Afisa Miradi wa Shirika la Utafiti, Maendeleo na Huduma kwa Jamii (CORDs), Martha Katua akizungumza wakati wa kugawa chakula hicho, jana Jumamosi, Desemba 3, 2022 alisema shirika hilo limetoa msaada huo baada ya kubaini kaya nyingi zinakabiliwa na uhaba wa chakula.
Katau alisema wamegawa tani 12 za mahindi kwa kaya 553 katika Kata ya Mfereji Wilaya ya Monduli ambayo ipo pembezoni mwa wilaya hiyo.
Alisema vijiji ambavyo vimenufaika na msaada huo ni Indonyonodo ambacho kimepatiwa tani 6.5 kwa kugawanywa kwa Kaya 301 na Kijiji cha Amalua Kaya 252 zimepata tani 5.5 za mahindi.
"Katika jamii hizi ambazo zinategemea ufugaji kuna uhaba mkubwa wa chakula kwani zinategemea kuuza mifugo ili kupata chakula lakini sasa mifugo mingi imekufa kwa ukame," alisema
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Kilimo, wilaya ya Monduli Theobald Ngobya alisema wilaya hiyo inahitahi tani 28,000 za chakula.
Ngobya alisema kumekuwepo na uzalishaji mdogo wa chakula kwa misimu zaidi ya kiwili mfululizo katika wilaya hiyo hatua ambayo imesababisha upungufu wa chakula.
Alisema wilaya hiyo inaupungufu wa mahindi tani 22,550 na maharagr Tani 7578 ili kupunguza tatizo la uhaba wa chakula katika maeneo mengi.
"Msimu uliopita tulizalisha tani 5,639 za mahindi na tani 1,337 tu kiasi ambacho ni kidogo," alisema
Baadhi ya wanufaika wa msaada huo, Samweli Lonina na Neema Peter walishukuru CORDs kwa msaada wa mahindi ambao unaokoa maisha yao.
Lonina alisema wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula hasa kutokana na ukame huku Neema akisema hivi sasa hata maziwa hawapati kwani mifugo mingi imekufa na mingine imedhoofika kwa kukosa malisho.
"Tunaomba Serikali na wadau wengine watusaidie chakula kwani licha ya kupata msaada huu bado tuna uhaba wa chakula," amesema.