Kauli ya mwisho ya Sia kabla kutokea ajali iliyoua wanafamilia wanne

Aminata Juma mfanyakazi wa Shirika la Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Agosti 4, 2023 akiwa nyumbani kwa Dk Norah Msuya Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Mmoja wa wafanyakazi wenzie na Sia Msuya amemuelezea marehemu huyo kama miongoni mwa watu wengu upendo na alipenda watu wawe na furaha.
Dar es Salaam. ‘‘Lile tabasamu ambalo tumekuwa tumezoea kumuona nalo dada Sia ndiyo hilo nililomuona nalo jana akiwa kwenye usingizi wa mauti’’.
Hiyo ni kauli ya Aminata Juma mfanyakazi wa Shirika la Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) aliyekuwa akifanya kazi na Sia Msuya aliyefariki na ndugu zake watatu katika ajali ya gari iliyotokea usiku wa Agosti 2.
Aminata anamuelezea Sia kama mtu mkarimu na mwenye upendo aliyetaka kuona siku zote watu wana furaha.
“Mimi nafanya kazi idara ya rasilimali watu yeye alikuwa kurugenzi ya utekelezaji oparesheni, Ijumaa alikuja ofisini kwetu na tukazungumza.
“Muda wote wa mazungumzo yetu alikuwa akinieleza mimi ni nani na anavyofurahia mafanikio yangu, akaniambia Aminata simama nikukumbatie basi tukakumbatiana,” amesema Aminata.
Bado Sia aliendelea kuzungumza na Aminata akimueleza anatamani kufanyike shughuli yoyote itakayowakutanisha wanawake wachache wafurahie maisha.
“Aliniambia kama tunaweza kuandaa jambo lolote zuri la kuwakutanisha wanawake wachache, nikamwambia Agosti 8 nitakuwa na tukio langu la kuchangia damu akasema lazima atakuwepo.”
“Aliniambia anaenda msibani akirudi tutakuwa pamoja. Tukiwa pale bado tunazungumza akapita dada mmoja bila kutusalimia akamwita akamuuliza wewe kwanini unakuta watu halafu husalimii unajuaje kama huyu kesho utamuona?”
Sia ambaye ni mtoto wa kwanza kwenye familia hiyo ya ndugu wanne waliopoteza maisha, hakubahatika kupata mtoto.