Kauli ya Askofu Chilongani kwa wanaomzodoa Rais Samia

Waumini wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT) Kanisa la Angilikana la Roho Mtakatifu, jijini Dodoma
Muktasari:
- John Malecela atangaza msamaha, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda azungumzia uchanguzi nchini.
Dodoma. Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT), Dickson Chilongani amesema wanamzodoa Rais Samia Suluhu Hassan kwamba hawezi lolote licha ya kazi nyingi alizofanya kwa muda mfupi, ni wabinafsi na hawafai kwenye jamii.
Dk Chilongani amesema hayo leo Jumapili Machi 31, 2024, akihubiri katika ibada ya sikukuu ya Pasaka iliyoadhimishwa kwenye Kanisa la Angilikana la Roho Mtakatifu, jijini Dodoma.
Amesema ujumbe wa Mwinjilisti Marko wakati wa Pasaka unaelekezwa katika usawa kati ya mwanamke na mwanaume.
Amesema Dayosisi ya Central Tanganyika hivi karibuni itakuwa na mkutano wa Sinodi na wameanza uchaguzi katika ngazi mbalimbali za kanisa hilo, hivyo anawaomba kuwe na usawa wa kijinsia.
Amewataka kusiwepo nafasi za wanaume pekee kwa sababu watu wote wako sawa mbele za Mungu.
Amesema kama Taifa pia uchaguzi umeanza katika ngazi mbalimbali na linaelekea katika uchaguzi mkuu, nao lazima kuwe na usawa wa kijinsia.
“Tuwaamini wanawake. Kubwa zaidi kumekuwa na baadhi ya wanaume wanaomzodoa Rais wetu Samia kana kwamba hawezi lolote kwa sababu ni mwanamke, kama kwamba hawaoni kazi ambazo Rais wetu alizozifanya katika kipindi chake kifupi cha uongozi,” amesema.
“Watu wa namna hii ni wabinafsi na hawatufai katika jamii na washindwe na walegee kwa jina la Yesu,” amesema Askofu Chilongani.
Amesema kifo cha Yesu kinavunja viambaza kati ya mwanaume na mwanamke na kati ya Wayahudi na Wayunani na kuwafanya wamoja.
Amesema inaonekana kuwa waliokwenda kaburini asubuhi walikuwa wanawake, hivyo inaonyesha kuwa ukiwekeza kwa mwanamke inalipa.
Askofu huyo amesema hiyo haimaanishi kuwa Yesu hakuwadhamini wanaume si sahihi, kama walivyoona kwa wanafunzi wote 12 wa Yesu walikuwa wanaume, hivyo pia aliwadhamini pia.

Waumini wakiwa katika ibada ya Pasaka kitaifa iliyofanyika jijini Dodoma katika Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Central Tanganyika, Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu. Picha na Hamis Mniha
Pia ametaka watu wasikate tamaa, badala yake wajue kuwa Yesu anawajali, anawapenda, anawasamini na anawasamehe.
“Kama leo umekuja katika ibada hii moyo wako umesinyaa na uso wako ukiwa umekunjamana Mungu akutie moyo au akupe matumaini uondoke kwa amani na furaha kwa sababu Bwana amefufuka,” amesema.
Askofu Chilongani amesema kama Yesu alivyomsamehe Petro, Wakristo pia wamepewa wito huo wa kwenda kuwasamehe wengine na kuwapa matumaini.
Rushwa bado changamoto
Askofu Chilongani amesema tangu Rais Samia aingie madarakani nchi haijatetereka, amani imeendelea kuwepo na uchumi umeendelea kukua.
Pia amempongeza Rais Samia kwa kuimarisha demokrasia na utawala bora.
“Eneo moja tu ningemuomba Rais alitupie macho ni kuhusu rushwa, bado inatajwa sana na hasa kwenye eneo la Mahakama. Kama Mwalimu Nyerere (Rais wa kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Nyerere) alivyosema rushwa ni adui wa haki,” amesema.
Amesema wasingependa iendelee kuota mizizi kwenye maeneo nyeti ya Tanzania kama vile Mahakama.

Waziri mkuu mstaaafu, John Malecela akiwa katika ibada ya Pasaka kitaifa iliyofanyika jijini Dodoma katika Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Central Tanganyika, Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu, leo Jumapili Machi 31, 2024. Picha na Hamis Mniha
Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela akitoa salamu katika ibada hiyo, amewataka waumini watafakari baada ya kutoka kanisani iwapo Yesu atakuwa amefufuka kwa mtu ambaye bado ana kisasi na wengine.
“Kwa hiyo wote tukitoka hapa tuondoke na amani ya kusema kuwa sisi tuko huru tumesamehewa na Kristo, kwa hiyo kama kuna watu wengine na hata mimi nataka kusema kama kuna mtu yoyote nilimkwaza katika jumuiya hii naomba leo Yesu kafufuka anisamehe,” amesema.
Amesema wamsamehe kama vile yeye atakavyowasamehe wote waliokosea.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda, aliyeshiriki ibada hiyo amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia iko imara na nchi iko salama.
“Rai yangu kubwa tudumishe amani iliyopo, kuna watu wameshindwa kuisherekea sikukuu hii kwa sababu hakuna amani, wanashindwa kusikiliza nyimbo zuri kama za leo kwa sababu hawana amani. Tuishikilie amani,” amesema.
Amesema mwaka huu waumini hao wanatambua kuwa kuna uchaguzi wa Serikali za mitaa, lakini mwakani pia uchaguzi mkuu na kwamba bila amani uchaguzi hautaenda vizuri.