Prime
Kauli ‘mtoto siyo wako’ ilivyosababisha mauaji

Muktasari:
- Mume afutiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa kisha kubadilishiwa kuwa kifungo cha miaka 10 jela.
Morogoro. Unaweza kuichukulia kuwa kauli nyepesi, lakini siyo wanaume wote wana kifua cha kuhimili.
Hiki ndicho kilichotokea kwa mume kumuua mkewe kutokana na hasira baada ya mke kumtamkia kuwa yeye siyo baba mzazi wa mtoto waliyenaye.
Ushahidi katika kesi ya mauaji unaonyesha mke alimpigia simu mumewe aliyekuwa akiishi eneo tofauti naye, akimwita afike kwa kuwa mtoto wao hakuwa na hali nzuri kiafya.
Mume alipofika mke akamwambia mtoto huyo si wa damu yake.
Mauaji hayo yalitokea saa 11:00 alfajiri Machi 2, 2023 katika Kitongoji cha Kota kijijini Mlimba A, wilayani Kilombero, baada ya Ditrick Mchekanae kumuua mkewe, Doris Mwabusenga, aliyekuwa mtumishi wa Benki ya NMB.
Baada ya mauaji hayo, mume alikamatwa akiwa na kisu chenye damu. Kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani, Jaji Paul Ngwembe wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro alimtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Hakuridhika na hukumu hiyo, akakata rufaa ambayo katika hukumu iliyotolea jana Juni 26, 2025 na nakala kuwekwa mtandaoni leo Juni 27, jopo la majaji watatu waliosikiliza rufaa hiyo wamebatilisha adhabu hiyo.
Baada ya kubatilisha na kufuta hukumu ya awali ya kuua kwa kukusudia, majaji hao, Dk Mary Levira, Sam Rumanyika na Agnes Mgeyekwa wamemtia hatiani kwa kosa dogo la kuua bila kukusudia na kumhukumu kifungo cha miaka 10 jela.
Mauaji yalivyofanyika
Machi 2, 2023 saa 11:00 alfajiri, shahidi wa kwanza wa Jamhuri, Rose Ngole akiwa nyumbani kwake, ghafla alisikia sauti ya mtu akilia: “Nakufa nakufa.”
Aliitambua ni sauti ya Doris aliyekuwa amepanga chumba kilicho jirani na chake.
Katika chumba hicho, Doris alikuwa akiishi na mdogo wake wa kike, hivyo shahidi alikwenda katika chumba hicho kujua kulikoni.
Alipofika mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani, akaenda kuangalia dirishani.
Dirisha halikuwa na pazia bali limefunikwa kwa chandarua, hivyo kupitia upenyo aliona tukio la kuogofya, kwamba Ditrick alikuwa ndani akiwa na kisu na alimchoma (Doris) tumboni na maeneo mengine ya mwili.
Kutokana na alichokiona, shahidi alipiga kelele kuomba msaada, majirani wakajitokeza na wakati huohuo, alikimbilia Benki ya NMB ambako Doris alikuwa mwajiriwa kutoa taarifa kwa mlinzi aliyekuwa lindo.
Mlinzi huyo, Jeremiah Minango aliitikia wito huo wa dharura wakarudi pamoja eneo la tukio.
Baada ya Ditrick kumuona mlinzi huyo, alifungua mlango akijaribu kukimbia lakini mlinzi kwa kushirikiana na wananchi walimkamata.
Mashahidi wengine
Shahidi wa pili, Minango aliyekuwa lindo Benki ya NMB alieleza baada ya Rose Ngole kumfuata lindoni na kumjulisha kuhusu ugomvi unaohusisha kisu, walirudi pamoja eneo la tukio na kukuta umati.
Akiwa hapo, alimuona Ditrick ameshika kisu chenye damu na alipomuona alikitupa kisu na kuanza kukimbia. Alimfukuza akamkamata na kumuamuru achukue kisu chake ambacho kilipokewa kama kielelezo.
Shahidi wa tatu, Samwel Mdeme, ambaye ni mwenyekiti wa kijiji alisema alipopokea taarifa alikwenda eneo la tukio alikokuta wananchi wamekusanyika, huku Ditrick akiwa ameshika kisu kilichokuwa na damu.
Aliwasiliana na Polisi waliofika na kumkamata. Alipokwenda chumbani alimkuta Doris utumbo ukiwa nje. Walimuwahisha Kituo cha Afya Mlimba kwa matibabu.
Dk Helam Mganda, shahidi wa nne alieleza namna alivyompokea Doris huku utumbo ukiwa nje. Alimfanyia upasuaji wa dharura.
Alisema aliendelea vizuri kwa saa 72 kabla ya hali yake kubadilika. Machi 6, 2023 shahidi alishauri mgonjwa apewe rufaa kwenda Hospitali ya St. Francis iliyopo Ifakara kwa matibabu ya juu zaidi.
Ninakuua nikiwa nakupenda
Ofisa wa Polisi namba E.4491 Sajini George wa Kituo cha Polisi Mlimba aliyeshughulikia tukio hilo alieleza alimuona mrufani akipelekwa kituoni na askari Polisi G.1098 Jeremiah.
Jeremiah aliyekuwa shahidi wa saba alimweleza Sajini George (shahidi wa sita) kuwa mrufani amemshambulia kwa kisu mfanyakazi wa Benki ya NMB na wakati huo mrufani alikuwa na kisu kilichochukuliwa kutoka eneo la tukio.
Machi 3, 2023 saa 4:00 asubuhi shahidi huyo wa sita (George), alikwenda Kituo cha Afya Mlimba kuandika maelezo ya Doris aliyemweleza katika tafrani, mrufani alimweleza: “Ninakuua nikiwa bado nakupenda.”
Shahidi wa saba (Jeremiah) alieleza alivyochora ramani ya eneo la tukio na kuwa, Machi 6, 2023 alijulishwa kuwa Doris amehamishiwa St Francis, lakini Machi 13, 2023 akapokea taarifa kuwa majeruhi amefariki dunia.
Shahidi wa tano, Oscar Mbiso, ofisa tabibu wa Kituo cha Afya Kibaoni alieleza alivyouchunguza mwili wa marehemu na kubaini sababu za kifo ni maambukizo ya bakteria yaliyotokana na jeraha.
Utetezi kortini
Katika utetezi wake mshtakiwa (mrufani) alikiri kusababisha kifo cha Doris aliyekuwa mkewe waliyeishi pamoja kwa miaka minne na walikuwa na mtoto mmoja.
Mbali ya huyo, walikuwa na mtoto mwingine ambaye mkewe alimzaa kabla hawajaoana. Alisema siku za mwanzo za uhusiano zilikuwa nzuri.
Alisema waliishi pamoja kwenye nyumba yao iliyopo Kijiji cha Miembeni hadi mkewe alipoajiriwa na Benki ya NMB ndipo mkewe alikodi chumba kimoja Mtaa wa Kota, ulioko Mlimba A, yeye akabaki katika nyumba yao.
Ditrick alisema siku ya tukio usiku wa manane alipokea simu kutoka kwa mkewe akimjulisha mtoto wao (aliyezaa naye) anaumwa. Saa 11:00 alfajiri alijihimu kwenda nyumbani kwa mkewe.
Alipofika alipokewa na dada wa kazi aliyemtaja kwa jina moja la Diana. Baada ya kuingia ndani, mkewe alimwambia yeye si baba wa damu wa mtoto wao na kwamba, uhusiano wao unavunjika siku hiyo.
Kutokana na kushtushwa na kauli hiyo, alisema alijikuta amemzaba kibao mkewe. Katika kujibu kipigo hicho, mkewe alichukua kisu na kumshambulia puani lakini alimnyang’anya na katika hali ya hasira alimshambulia nacho.
Alieleza wakati hayo yakitokea, Diana na mtoto wake walikuwa wamekaa sebuleni. Anakumbuka alitoka nje akiwa bado ameshika kisu hicho.
Alisema alipotoka nje alikuta wananchi na polisi akaamriwa kujisalimisha, yeye alijaribu kutoroka eneo la tukio lakini alikamatwa.
Alieleza kiini cha tukio hilo ni kauli ya uchokozi ya mkewe lakini anajutia kitendo hicho.
Mahakama ya awali iliamini mashahidi wa upande wa Jamhuri na kumtia hatiani na kumhukumu kunyongwa hadi kufa. Hakuridhika na hukumu akakata rufaa Mahakama ya Rufani.
Hukumu ya majaji
Baada ya kusikiliza hoja za pande mbili katika rufaa, majaji walisema walichobaini ni kuwa, mrufani habishi kuwa ndiye aliyesababisha kifo cha mkewe lakini anachobisha ni hoja kuwa alimuua mkewe kwa makusudi au kudhamiria.
“Hoja ya kuipatia majibu katika rufaa hii ni kama mrufani alichokozwa ili kuchokozwa huko ndiyo kuwe utetezi katika kusababisha mauaji,” inasema sehemu ya hukumu ya majaji.
Wakinukuu msimamo wa kisheria, majaji hao wamesema: “Provocation ama uchochezi au uchokozi ni kitendo cha ghafla na kibaya ambacho kingeweza kusababisha mtu mwenye akili timamu ashindwe kujizuia.”
Majaji wamezingatia kwa uzito ushahidi uliopo katika kumbukumbu za rufaa hiyo na kukuta kuwa maneno ya uchokozi yalitolewa na marehemu.
Kwa bahati mbaya, majaji hao walisema katika kesi hiyo, kuna maelezo ya mrufani pekee ambaye alieleza namna alivyoitwa usiku na mkewe kwamba mtoto anaumwa na alipofika ndipo akaambiwa kuwa yeye si baba mzazi wa mtoto huyo.
“Mrufani anaeleza kuwa alifika nyumbani kwa mkewe akiwa hana silaha yoyote na kwamba, kisu kilichotumika kinamilikiwa na marehemu na kilipatikana eneo la tukio,” inaeleza hukumu ya majaji na kuongeza:
“Maelezo haya hayakuwahi kupingwa na mashahidi wa Jamhuri.”
Jopo hilo la majaji linasema uchochezi wa mkewe haukumpa nafasi mume kutuliza akili, badala yake akafanya tukio la kushtukiza kwa hasira.
Wameeleza wamezingatia pia kumbukumbu za kitabibu zilizopo katika jalada la mwenendo wa shauri hilo kwamba, Doris hakufa mara moja kutokana na jeraha hilo la kisu kama Jamhuri walivyoiaminisha mahakama.
Ushahidi huo unaashiria alifanyiwa upasuaji na kupata nafuu na hakuwa tena katika hatari na kwamba, sababu za kifo chake ni maambukizi ya bakteria aliyoyapata saa 72 baada ya kufanyiwa upasuaji.
Majaji wamesema upande wa mashitaka hawakutoa ushahidi madhubuti na wa wazi wa kitabibu kuoanisha kifo na shambulio hilo.
Kwa kukosekana ushahidi huo wa kitabibu, wamesema kunampa mrufani faida ya mashaka.
“Upande wa mashtaka uliweka uzito kwenye maneno ya marehemu kuwa mrufani alimwambia nakuua huku nikiwa bado nakupenda lakini ushahidi huo haukuungwa mkono na ushahidi wowote wa upande wa mashitaka,” inaeleza hukumu.
Kwa ujumla wamesema kunakosekana muunganiko kati ya madai ya uwapo wa dhamira ya kuua na ushahidi uliopo katika jalada, hivyo wanaona mrufani alifanya hayo kutokana na maneno ya uchokozi aliyoambiwa na mkewe.
Wamesema ushahidi unaonyesha Jamhuri hawakuthibitisha shtaka la mauaji ya kukusudia bali mauaji ya bila kukusudia, hivyo wanafuta adhabu ya kunyongwa hadi kufa na kuwa kifungo cha miaka 10 jela.