Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Katiba mpya bado moto, wananchi wafunguka

Aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, DK Damas Ndumbaro

Dar/Mikoani. Kauli ya Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro ya kuanza mkakati wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu Katiba mpya kwa miaka mitatu (2023 hadi 2026), imewagawa wananchi katika makundi mawili.

Kundi moja linaunga mkono muda huo, huku jingine likipinga, likiona ni mrefu na Serikali inauchelewesha makusudi.

Wakizungumza na Mwananchi Digital, wanaounga mkono muda uliotolewa na Serikali walisema si vyema kuharakisha upatikanaji wa Katiba wakati watu wengi hawana elimu nayo.

Wanadai, kuharakishwa kwa upatikanaji wake, kutawaacha nyuma wananchi ambao wamekuwa wakisikia uwepo wa mchakato wa Katiba lakini unamezwa na wanasiasa wenye masilahi yao.

Walisema hawaoni sababu ya kuharakisha kupatikana kwake kwa kuwa kuna uwezekano wa kupitisha dosari kwa kuwa watu wanawaza Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwakani na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, hivyo wanataka mambo mengi yanayogusa maeneo hayo badala ya kuwaza masilahi mapana ya Taifa.

Hata hivyo, wanaopinga muda huo, wanadai kuwa mchakato wa Katiba mpya ulianza muda mrefu, hivyo elimu haipaswi kuchukua miaka mitatu kwa kuwa wananchi wana uelewa wa kile wanachokidai.

Kutozingatiwa kwa matakwa hayo, wanadai ni kuharibu mfumo wa demokrasia alioanza kuujenga Rais Samia Suluhu Hassan, wakisisitiza upatikanaji wa Katiba kwa haraka ni muhimu kwa mazingira ya sasa.

Msisitizo pia upo kwa wananchi hao kuhitaji uchaguzi wa 2025 uendeshwe chini ya Katiba mpya, ili wananchi wawe na nguvu ya kuwawajibisha viongozi wanaogeuka vibaraka wa Serikali na si watumishi wa wananchi.

Walisema suala la Katiba ni la wananchi, sio la viongozi wa siasa pekee, hivyo Serikali isiwe na danadana kwenye suala hilo.

Msimamo wa Serikali

Juzi Waziri Ndumbaro, katika mkutano uliowakutanisha mawaziri wakuu na wanasheria wakuu wastaafu na waliowahi kuwa mawaziri wa Katiba na Sheria, alisema Serikali sasa inaelekeza nguvu zake katika kutoa elimu kwa umma.

“Watanzania wakisema wanataka Katiba mpya kesho, na sisi tutafanya jitihada za kupata Katiba mpya kesho, Watanzania wakisema wanataka Katiba mpya leo na sisi tutafanya jitihada za kupata Katiba mpya leo,” alisema.

Waziri huyo aliongeza maudhui ya Katiba na lini ikamilike siyo suala la Serikali kuweka ukomo wa muda, bali ni suala la wananchi kuamua.

Alisema namna ya wananchi kuamua na kuukwamua mkwamo wa Katiba, ndiyo mchakato unaoendelea sasa wa kushirikisha wadau.

Kuhusu maoni ya wananchi kupata Katiba kabla ya uchaguzi mkuu, Waziri Ndumbaro alionya kwamba Watanzania wasifanye kosa la kudhani kwamba Katiba inahusiana na kipengele kidogo cha uchaguzi.

Mitizamo ya wananchi

Mkazi wa jijini Dodoma, Priscus Kulaya alisema miaka mitatu ni mingi, kwani elimu ya Katiba ilishatolewa nchi nzima wakati wa utawala wa awamu ya nne wa Rais Jakaya Kikwete.

Alisema wakati huo elimu ya Katiba ilitolewa na mchakato huo ulifika mbali baada ya Bunge Maalumu kujadili na kutoa Katiba inayopendekezwa iliyokuwa ikisubiri kura ya maoni ya kukubaliwa au kukataliwa.

“Wakati uliopo ni wa kupata Katiba mpya si wa kutoa elimu ya kuijua Katiba iliyopo,” alisema.

Maembe Julius, mchuuzi katika soko la Mgandini jijini Tanga, alisema kauli ya Waziri Ndumbaro inaweza kuleta shida kwa sababu baadhi ya wananchi watakosa imani na Serikali.

"Sioni mwanga wa demokrasia siku za usoni kwa sababu Waziri Ndumbaro ametoa kauli inayopingana na Rais, tegemeo letu ni kwa Rais wetu Samia ndiye atakayetuondoa kwenye tatizo hili na siyo watendaji wake," alisema Maembe.

Naye Tobith Lubida ambaye ni mfanyabiashara Dar es Salaam alisema suala la Katiba ni jambo la muda mrefu, hivyo kutumia muda mrefu kutoa elimu hakuna mantiki.

Hata hivyo, John Haule, Mkazi wa Manispaa ya Moshi, alisema wananchi wengi hawaelewi maana ya Katiba na kwamba hawana muda wa kuichukua Katiba na kuisoma na wengi wamekuwa wakikurupuka tu kuzungumza vitu ambayo hawavijui.

"Muda wa miaka mitatu uliowekwa kwa ajili ya kutoa elimu ya Katiba ni mzuri, nakubaliana nao kwa sababu sasa hivi ongezeko la watu ni kubwa tofauti na ilivyokuwa hapo awali, watu wakishatoa maoni yao basi Serikali iyafanyie kazi ili yaweze kuleta maendeleo katika Taifa letu," alisema

Mkazi wa Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya, Atanas Joel alisema kwa miaka mingi sasa Watanzania wanasikia tu suala la Katiba na mvutano baina ya chama na chama, lakini uelewa wao umekuwa mdogo.

Joel anaungwa mkono na Ashura Hashimu, muuza duka Coco Beach mkoani Mtwara, aliyesesema Waziri Ndumbaro yuko sahihi kwa hoja kwamba wananchi wapewe elimu kwanza, lakini muda wa miaka mitatu ni mrefu, hasa nyakati hizi ambazo utandawazi umetamalaki na wengi wanapata elimu kwa njia mbalimbali.

"Miaka mitatu ni mingi sana, apunguze ila elimu itolewe kwa njia mbalimbali zinazoweza kutufikia kwa urahisi zaidi ambapo na sisi tutaweza kuungana na wengine kufanya mabadiliko hayo,” alisema.

Wanaharakati wapinga

Jana, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) na Jukwaa la Katiba (Jukata) walikutana na waandishi wa habari makao makuu ya LHRC, Kijitonyama, Dar es Salaam wakikosoa kauli ya Waziri Ndumbaro.

Walisema utoaji wa elimu kwa miaka mitatu ni mpango wa kuchelewesha upatikanaji wa Katiba mpya.

Mkurugenzi wa LHRC, Anna Henga alisema kauli hiyo haina tija na haiendani na dhamira ya Rais Samia ya kurejesha mchakato wa Katiba ili kutimiza azma yake ya 4R, yaani (Mabadiliko) Reform, Reconciliation (Mapatano), Rebuild (Kujenga upya) na Resilience (Uthabiti).

“Matarajio yetu na ya Watanzania walio wengi tulitegemea kuona jitihada mahususi za kurekebisha dosari zilizojitokeza na kusababisha kukwama kwa mchako wa Katiba mwaka 2014 kwa kukosa mwafaka wa kitaifa uliosababisha mivutano mikali ya kisiasa na kusababisha baadhi wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kujitoa kwenye majadiliano ya Katiba,” alisema.

“Hivyo tukisema tutumie miaka mitatu kutoa elimu ya Katiba halafu ndiyo mchakato uanze baadaye, itapelekea kuanza mchakato wa Katiba mpya miaka minne ijayo na tutafika tena kwenye uchaguzi wa 2030 bila Katiba mpya na wakati hatujui nia na mtazamo wa kiongozi atakayekuja kuwa mrithi wa Rais Samia,” alisema.

“Fedha hizi zitumie kuanzisha mijadala ya namna gani tunaweza kuanza mchakato wa katiba ambao ni shirikishi na wa haraka. Elimu ya katiba mpya ilishatolewa na Tume ya Jaji Warioba pamoja na Bunge la Katiba,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Jukata, Dk Ananilea Nkya aliwataka wasaidizi wa Rais Samia kuwezesha kukamilika kwa mchakato huo.

“Chama kilichopo madarakani, kama kinataka kumsaidia Rais Samia kuiweka Tanzania katika hali nzuri, wahakikishe wanakuwa wa kwanza kusimamia Serikali Katiba ipatikane haraka iwezekanavyo,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa jukwaa hilo, Bob Wangwe alisema kitendo cha Serikali kutumia Sh9 bilioni ni kupoteza rasilimali za wananchi.

“Utoaji wa elimu uliozungumziwa na Waziri ni kutaka kupoteza muda na fedha,” alisema.