Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makada 58 Kilimanjaro waitosa Chadema, wamtaja Ndesamburo 

Muktasari:

  • Viongozi hao wametangaza kujivua uanachama huo kwa madai ya kutotendewa haki na chama chao.

Moshi. Viongozi na wanachama zaidi ya 58 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Kilimanjaro, akiwamo Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa, Gervas Mgonja wamejivua uanachama wao kwa madai ya kutoridhishwa na mwenendo wa chama hicho.

Viongozi wengine waliojivua ni Katibu wa Bawacha Kanda ya Kaskazini, Rachael Sadick, Mwenyekiti wa Bawacha Mkoa wa Kilimanjaro, Grace Kiwelu, Mjumbe wa kamati ya Tehama Kanda ya Kaskazini, Answary Kimaro na Mwenyekiti wa Chadema mstaafu Mkoa wa Kilimanjaro, Michael Kilawila.

Miongoni mwa viongozi hao wamo wa Jimbo la Same Mashariki, Same Magharibi, Mwanga, Moshi Vijijini, Vunjo na baadhi ya viongozi wa zamani wa Jimbo la Moshi Mjini.

Akieleza sababu za kujivua uanachama wa chama hicho mbele ya vyombo vya habari leo Jumapili Mei 11, 2025 mjini Moshi, Mgonja amesema hawezi kukitumikia chama ambacho hakina mwelekeo unaoridhisha na hakitashiriki uchaguzi mkuu.

Baadhi ya viongozi waliojivua uanachama wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Kanda ya Kaskazini

"Nimejiunga na Chadema huu ni mwaka wa 17, nimekuwa kiongozi kwenye chama hiki na kufanya kazi ya chama kama Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, mjumbe wa mkutano mkuu Taifa, nimehudumu kwenye chama hiki nyakati ngumu na nyakati za furaha nakijua vizuri sana,” amesema Mgonja. 

Amesema si kwamba leo anafuraha sana anapozungumza na waandishi wa habari, bali hali imemlazimisha aseme.
Mgonja amesema hivi karibuni chama chao kimekuwa na mwenendo usioridhisha huku akidai kuwa wamelelewa katika mazingira mazuri ya mshikamano, umoja na wazee wao  waliowatangulia akiwemo Philemon Ndesamburo.

“Alitujenga kuwa na mshikamano tukawa familia moja, lakini sasa hivi ndani ya chama chetu hatuna mazingira yanayoridhisha, hajulikani mwenyekiti ni nani, katibu ni nani, mwanachama ni nani, matusi na kejeli vimetawala baada ya kupata uongozi mpya,” amelalamika Mgonja.

Amesema wachache waliomuunga mkono Freeman Mbowe katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wao mkuu wa ndani, wanaishi maisha ya shida sana hivi sasa ndani ya chama hicho.

“Miezi kama minne, mitatu hivi sasa tunaendelea kuishi katika mazingira magumu sana, lakini wachache tuliokuwa tunajitosa kukikishauri chama chetu kwamba hatuwezi kukimbia pambano la uchaguzi mkuu, mawazo yetu yalikuwa yakitukanwa, tunaonekana hatufai, wasaliti, tumetumwa ni matusi asubuhi hadi jioni,” amesema Mgonja.

Hata hivyo, amesema leo anakiri mbele ya waandishi wa habari kwamba anajivua rasmi vyeo vyake vyote sambamba na uanachama wa Chadema.

“Leo Mei 11, 2025 uanachama wangu unakoma rasmi Chadema, mimi sijastaafu ni kijana mdogo sisemi kwamba sitafanya siasa, lakini kuanzia sasa nagota uanachama wangu, vyeo vyangu, nahitaji kupumzika na kutafakari upya,” amesema.

Rachael ambaye alikuwa Katibu wa Bawacha Kanda ya Kaskazini na Mwenyekiti wa Bawacha Mkoa wa Tanga, amesema ameamua kujivua uanachama wa chama hicho kutokana na kutosikilizwa anapotoa ushauri na badala yake anaonekana anakisaliti chama.

"Nimefanya kazi Chadema sasa ni mwaka wa 15, nimefanya kazi ndani ya Chadema kwa jasho na damu, nimefanya kazi mpaka nikafilisika na kufukuzwa serikalini na nimeijenga Chadema Mkoa wa Tanga kwa nguvu kubwa sana lakini sisi ndio tunaokaa na kujadiliwa uanachama wetu na kutuona wasaliti hii inatosha,” amesema Rachel. 

Gervas Mgonja, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro

Amesema kwa kinachoendelea ndani ya chama hicho haoni mwanga huko wanakoelekea, hivyo  ameamua kuachia ngazi huku akiendelea kujitafakari kuhusiana na mustakabli wa kufanya siasa.

Akizungumza katika mkutano huo, Kiwelu ambaye pia alikuwa Mwenyekiti kamati ya fedha kanda ya Kaskazini na mjumbe wa kamati tendaji Bawacha Taifa, amesema Chadema aliipenda sana lakini analazimika kuondoka kutokana na mambo yanayoendelea.

"Leo nimesimama mbele yenu kusema asante kwa chama changu Chadema, kimenipa heshima nimekuwa mbunge, nimekuwa mjumbe wa kamati kuu ndani ya chama hiki ambacho nimejiunga toka mwaka 1992 nikiwa binti na leo nazeeka mbele ya chama,” amesema Kiwelu.

Amesema Chadema alikipenda na kukitumikia kwa dhati ya moyo wake, lakini badala ya kuvuna heshima anaambulia kuvuna matusi.

“Mimi pia ni mmoja wa G55, tulikishauri chama kwa nia njema kwamba tunahitaji Reform lakini zisizuie uchaguzi, tumepuuzwa, hapa nilipofika nilijengwa na chadema lakini sasa itoshe kusema kuanzia leo Mei 11,2025 ninajiondoa rasmi chadema, ninakwenda nyumbani, bado nina nguvu,” amesema kada huyo. 

Amesema si kwamba ameacha siasa, bali ameamua kupumzika na anamshukuru Mungu amempatia mjukuu, anenda kumlea akiendelea na tafakuri ya kina.

Naye Kilawila amesema licha ya kujengwa na chama hicho kwa sasa ameona si mahali salama tena kuendelea kufanya siasa hivyo naye amejivua uanachama rasmi.

Rachael Sadick, aliyekuwa Mwenyekiti wa Bawacha Chadema Kanda ya Kaskazini

“Leo mimi Michael Kilawila ninaachana na Chadema, naenda kupumzika. Hakuna aliyenileta Chadema na nimeamua kuondoka mwenyewe kama nilivyojiunga mwenyewe,  bado nitaendelea kuwasemea wananchi wangu kwa sababu wana imani na mimi na bado nafanya kazi na wananchi ambao walinituma nigombee udiwani na bado wana matumaini na mimi. Ninapumzika ila sijastaafu.