Kamati za Bunge zaitwa Dodoma

Muktasari:
- Mkutano wa Bunge wa 12 utaanza Agosti 29, 2023 ukitanguliwa na vikao vya kamati za kudumu za Bunge ambazo zitaanza kukutana kuanzia Agosri 14-25, 2023 jijini Dodoma.
Dar es Salaam. Bunge la Tanzania limesema, vikao vya kawaida vya Kamati za Kudumu za Bunge vitaanza kufanyika Jumatatu Agosti 14-25, 2023 Jijini Dodoma kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano wa 12 wa Bunge utakaonza Agosti 29, 2023.
Kamati tano zitatangulia kuanza vikao, ambapo nne kati ya hizo zitaanza vikao Agosti 7, 2023 na Kamati moja ya Bajeti itaanza Agosti 10, 2023.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na Ofisi ya Bunge leo Jumapili, Agosti 6, 2023 na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa, imesema shughuli za kamati katika kipindi hicho zitakuwa ni: -
(i)Uchambuzi wa Miswada miwili (2) ya Sheria utakaofanywa na Kamati mbili: Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria na Kamati ya Bajeti;
(ii) Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa wakati wa Mkutano wa Kumi na Moja wa Bunge;
(iii) Uchambuzi wa Taarifa za Hesabu zilizokaguliwa na CAG kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Juni 30, 2022;
(iv) Uchambuzi wa Taarifa za Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa lengo la kuliwezesha Bunge kufuatilia ufanisi na tija kwa Mitaji ya Serikali kwenye mashirika mbalimbali na taasisi; na
(v) Uchambuzi wa Taarifa za Utendaji za Wizara kwa lengo la kuliwezesha Bunge kutekeleza jukumu la kuisimamia na kuishauri Serikali.