JWTZ kulinda bwawa la Mindu saa 24

Upandaji wa miti rafiki ya maji inayotekelezwa na Bodi ya maji Bonde la Wami Ruvu pembezoni mwa Bwawa la Mindu.
Muktasari:
- Upandaji miti Bwawa la Mindu waendelea kwa Kasi huku JWTZ pamoja na askari wa akiba wakishiriki ulinzi saa 24.
Morogoro. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Fatma Mwassa amewataka wananchi kuwa walinzi, kuheshimu mipaka ya hifadhi ya vyanzo vya maji hasa Bwawa la Mindu na kwamba hatua kali za kisheria kuchukuliwa kwa watakao husika kuchoma moto hifadhi ya vyanzo hivyo.
Ametoa agizo hilo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kupanda miti rafiki ya maji inayotekelezwa na Bodi ya maji Bonde la Wami Ruvu.
Mwasa amesema atakayebainika kujihususisha kwa namna yoyote na vitendo vya uharibifu wa mazingira kwa kuchoma moto au kufanya shuhguli nyingine za kibanadamu atachukuliwa hatua ikiwemo kifungo cha miaka saba gerezani.
Amesema katika kuhakikisha eneo linabaki katika uhifadhi tayari mamlaka zimekabidhi jukumu la ulinzi kwa kikosi maalumu cha Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa kushirikiana na jeshi la akiba ambao watakuwepo eneo hilo kwa saa 24.
“Bwawa hili linalindwa na kikosi maalumu cha JWTZ) wakishirikiana na jeshi la akiba, sasa mtu yeyote uje ufanye fujo zako utaangukia kwenye sheria, ukijenga kibanda au kuchoma moto utasahaulika,” amesema Mkuu huyo wa mkoa.
Aidha amewataka wale wote wanaofanya shughuli za kibinadamu karibu na bwawa hilo kuacha kabisa kwani atakayebainika kufanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa juu yake kwa mujibu wa sheria ya mazingira.
“Niwambie tu wakazi wa Morogoro ni marufuku kuchoma moto katika eneo hili la hifadhi, sasa wewe njoo tu uchome moto hapa ndio utajua mimi ni kama bendera chuma mlingoti chuma na upepo chuma," amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu, Elibarik Mmassy amesema kampeni hiyo inalenga kupanda miti milioni mbili (2) katika maeneo mbalimbali ya vyanzo vya maji katika Mkoa wa Morogoro.
Amesema kwa sasa Bwawa la Mindu linakabiliwa na changamoto ya tope lililochangiwa na shughuli za kibinadamu kandokando ya bwawa hilo, ikiwemo uchomaji wa miti kwa ajili ya uandaaji wa mashamba hali iliyochangia kupungua kwa kina cha maji na kuathiri upatikanaji wa maji katika mji wa Morogoro.
Amesema zoezi hilo linakwenda sambamba na utekelezaji agizo la Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Philip Mpango kuhusu kupanda miti milioni mbili kila mkoa.
Bodi ya maji Bonde la Wami Ruvu ni miongoni mwa bodi 9 zilizopo nchini ikiwa imeazishwa mwaka 2002 ikitekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria ya usimamizi wa rasilimali za maji namba 11 ya mwaka 2009 na kufanyiwa marekebisho sheria namba 8.