MAHUBIRI: Kufufuka Yesu ndio msingi wa imani ya Kikristo

Muktasari:
- Leo Wakristo ulimwenguni kote wanasherehekea kufufuka Mwokozi Yesu Kristo, ambapo tukio hilo linatajwa kuwa ndipo ulipo msingi ya imani ya Kikristo.
Bwana Yesu asifiwe! Leo tukiwa tunaadhimisha Sikukuu ya Pasaka inayomaanisha kufufuka kwa Bwana Yesu kutoka kaburini, natamani uyafahamu mambo ya msingi kuhusiana na ufufuko huu ili kumwezesha kila mmoja kufaidika na uhalisia wa tukio hili.
Ukristo umezaliwa kupitia Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye ni mwanzilishi pekee wa imani ambaye alikufa na hakubaki kaburini, maana alifufuka baada ya siku tatu kama maandiko yanavyothibitisha. Kufufuka huku kunathibitisha kuwa Yesu aliwahi kuzaliwa, akaishi na baadaye akakamatwa na kusulubiwa na akafa kisha akazikwa ili siku ya tatu afufuke kama ilivyotokea. Imani yetu imejengwa juu ya ufufuko wake, ambao kwetu ni ishara ya ushindi dhidi ya kaburi na mauti pamoja na yeye aliyekuwa na nguvu za mauti.
Kupitia kufufuka kwa Bwana Yesu tunapata aina hizi za imani:
Imani ya wokovu
Wokovu huu ni ule wa mtu kuokolewa kutoka mautini kwasababu ya dhambi zako na madhara yake na kuingizwa uzimani, yaani kuingizwa katika ufalme wa Mungu. Neno la Mungu linatuonyesha kuwa ili mtu aokolewe na mauti hii itokanayo na dhambi ni lazima aamini ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana (yaani ni mtawala wa maisha yako kuanzia unapompokea) na uamini kuwa Mungu alimfufuka katika wafu (Warumi 10:9-10). Imani hii ndiyo itakayokupa ushindi dhidi ya dhambi na mauti hata baada ya kuokoka. (Soma zaidi 1 Wakorintho 15:1-58).
Imani ya kufufuliwa pale tunapokufa
Imani yetu katika kufufuka kwa Yesu inatupa ujasiri kwamba hata siku watakatifu wakifa, Mungu anaweza kuwafufua tena ili kuwapeleka katika raha yake kule mbinguni ambapo hakuna mauti wala kilio tena.
Pili, tunaamini kuwa mtu yeyote akifa tunaweza kumfufua, maana imani aliyokuwa nayo Yesu ndiyo tuliyonayo (Wagalatia 2:20) ya kwamba yeye alikufa baada ya mwili wake kuharibiwa kwa mapigo, lakini bado alifufuka. Pia, Roho aliyemfufua Yesu ndiye aliyepo ndani yetu (Warumi 8:11) na ndiye Roho wa imani ambaye anatupa ujasiri na nguvu ya kuwafufua waliokufa (2 Wakorintho 4:13-14).
Imani ya ushindi dhidi ya kifo na mauti
Kufufuka kwa Yesu kunatupatia uthibitisho kuwa wana wa Mungu wana mamlaka dhidi ya mauti (Ufunuo 1:18). Unajua ni ngumu watu kuamini kuwa mtu anaweza kuishi mbali na mauti kama alivyokuwa Henoko (Waebrania 11:5) na hii siyo kwa sababu Mungu hawezi kufanya, bali kwa sababu ya ujinga wa kutokujua haki zetu katika wokovu tulioupokea. Yesu anamwambia Martha wakati anakwenda kumfufua Lazaro kuwa kwa watu waliokufa Yeye ni ufufuo na kwa watu walio hai yeye ni uzima na wanaoamini hili hawatakufa milele (Yohana 11:23-26).
Ukiamini hili unaweza kutembea pamoja na nguvu ya ufufuo ili kufufua waliokufa na nguvu ya uzima ili kuzuia yeye asipatwe na mauti.
Imani juu ya ahadi zote za Mungu juu yetu
Tukio la kufufuka kwa Yesu kabla ya kuwa halisi lilitanguliwa na unabii kutoka kwa manabii wa agano la kale ambao walitabiri kuhusu maisha yake yote. Isaya ni miongoni mwa manabii hao ambaye alitabiri kuanzia atakayebeba mimba (Isaya 7:14), kuzaliwa kwake (Isaya 9:6-7), mateso yatakayompata (Isaya 52:14, Isaya 53:3-7) na mwisho kufa na kufufuka kwake (Isaya 53:3-11). Kabla ya kutimia kwa unabii kulikuwa na kipindi fulani cha muda ambapo kilipita lakini ulipowadia utimilifu wa wakati Mungu alitimiliza mambo yote kama yalivyotabiriwa na manabii na hii inathibitisha kwamba ahadi zote za juu yetu ni amina na kweli (2 Wakorintho 1:20), kwa hiyo tunahitaji uvumilivu na imani ili kuziona zikitimia juu yetu (Waebrania 6:12,15).
Imani juu ya utendaji kazi wa uweza na nguvu za Mungu
Tatizo kubwa ambalo limekosa ufumbuzi kwa wanadamu mpaka sasa ni kifo. Unapotazama kufufuka kwa Yesu ni muhimu kuangalia na aina ya mateso yaliyompata kabla ya kufa ili uelewe uzito wa muujiza huu na tofauti ya kufufuka kwa Yesu na wengine waliowahi kufufuka na watakaofufuliwa baadaye.
Yesu alichubuliwa kwa mijeledi, alipigwa kichwani huku wakiishindilia taji ya miiba izame kichwani, alichomwa mkuki ubavuni na hapo maji na damu vikatoka, lakini bado siku ya tatu alifufuka. Muujiza huu ni udhihirisho mkubwa wa uweza wa Mungu na imani yetu kuhusu uweza wa Mungu.
Yesu alikubali kufa kwa ajili ya kila mmoja ili kila atakayemwamini asipotee dhambini bali aokolewe na dhambi iletayo mauti. Kubali kumpokea Yesu leo ili usiendelee kukaa kwenye mateso na vifungo vyako.
Askofu Dickson Kabigumila ni mwanzilishi wa makanisa ya ABC Global duniani. Anapatikana Kinzudi Goba, Dar es Salaam. Simu 0759625673