JK kuzindua NBA ya Bongo

Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete
Muktasari:
Mbali na Kikwete, uzinduzi wa ligi hiyo itakayoshirikisha watoto wenye umri kati ya miaka 12-14, utahudhuriwa pia na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Afrika na gwiji wa zamani wa mchezo huo, Amadou Gallou Fall.
Dar es Salaam. Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa msimu wa pili wa Ligi ya Kikapu kwa vijana itakayofanyika kwenye Kituo cha Jakaya Mrisho Kikwete (JMK Park) kilichopo Kidongo Chekundu jijini, Dar es Salaam, Novemba 5.
Mbali na Kikwete, uzinduzi wa ligi hiyo itakayoshirikisha watoto wenye umri kati ya miaka 12-14, utahudhuriwa pia na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Afrika na gwiji wa zamani wa mchezo huo, Amadou Gallou Fall.
Mratibu wa mashindano hayo, Zakayo Edward alisema ligi hiyo itashirikisha shule 30 ambazo kila moja itapewa jina la timu inayoshiriki Ligi ya Mpira wa Kikapu nchini Marekani (NBA).
“Hii ni programu ya ligi ya mpira wa kikapu kwa vijana ya kidunia. Ikihusisha wavulana kwa wasichana na inafundisha stadi za kimsingi za mpira wa kikapu pamoja na tabia njema na nidhamu ya mchezo.
“Pamoja na Kikwete na Amadou, pia Mkurugenzi Mtendaji wa Symbion Power, Paul Hinks na mmoja wa wachezaji mashuhuri wa Ligi NBA watahudhuria,” alisema mratibu huyo.