Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jinsi ya kuwasilisha taarifa mbaya bila kumuathiri mpokeaji

Muktasari:

  • Habari ya kifo cha ndugu, ajali, kuachwa, matokeo ya mitihani, kupoteza mali au kugundulika kwa ugonjwa unaohatarisha maisha ni miongoni mwa taarifa ngumu ambazo mtu anaweza kupokea. Hata hivyo, namna taarifa hizo zinavyowasilishwa kwa mhusika, inaweza kupunguza au kuongeza maumivu, taharuki au mshtuko kwa anayezipokea.



Dar es Salaam. Si jambo la ajabu kuona au kusikia mtu aliyepokea taarifa za ama msiba, ajali, kuachwa, matokeo ya mitihani au kugundulika kwa ugonjwa unaohatarisha maisha amezimia kwa mshtuko au kuapata kiwewe, taharuki, msongo wa mawazo na hata kuchanganyikiwa.

Taarifa mbaya kama kama hizo, wataalamu wanasema zinapowasilishwa ghafla bila kumwandaa mpokeaji, zinaweza kusababisha mshtuko wa kisaikolojia na kuibua athari mbaya za kiafya, zinazohitaji uangalizi wa haraka na wakati mwingine zinaweza kusababisha kifo.

Wataalamu wa afya ya akili na mawasiliano wanasema kwa kawaida, maumivu anayopata mpokeaji wa taarifa, hayachangiwi na uzito wa taarifa yenyewe pekee, bali pia na namna inavyofikishwa kwake.

Kwa mujibu wa wataalamu hao, mawasiliano yenye huruma na yanayomwandaa mpokeaji yanaweza kupunguza athari za kihisia, ilhali taarifa inayotolewa kiholela inaweza kuongeza msongo wa mawazo, wasiwasi na matatizo mengine ya afya, hususan kwa watu wenye historia ya magonjwa ya moyo au shinikizo la damu.

Licha ya mazingira hayo, katika jamii ya sasa, ambako taarifa husambaa kwa kasi kupitia simu na mitandao ya kijamii, si ajabu tena mtu kufahamu kifo cha ndugu au rafiki yake wa karibu kupitia picha, video au ujumbe uliosambazwa mtandaoni kabla yeye hajaarifiwa rasmi wala kuandaliwa.

Wataalamu wanasema tabia hiyo inakosa utu na mawasiliano yenye huruma, hali ambayo inaweza kuongeza maumivu kwa anayepokea taarifa na pengine kusababisha hata vifo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa mawasiliano yenye huruma ni sehemu muhimu ya huduma bora za afya na msaada wa kisaikolojia, hasa wakati wa kutoa taarifa zinazobadili maisha ya mtu.


Kinachotokea mwilini

Kwa mujibu wa watalaamu wa afya, taarifa mbaya anazopokea mtu huamsha mfumo wa mwili wa kukabiliana na hatari, ambapo homoni ya ‘adrenaline’ huongezeka na kusababisha mapigo ya moyo kwenda kasi, pamoja na mabadiliko katika mfumo wa fahamu.

“Mtu anaweza kupata mshtuko, kupoteza fahamu, kuanguka au kupata athari kwenye moyo. Wengine hupata shinikizo la damu la ghafla au hata kujikojolea kutokana na mshtuko mkubwa,” anasema, Daktari Fabian Maricha.

Anashauri kuwa badala ya kumwambia mtu moja kwa moja, mathalan, kwamba ndugu yake amefariki dunia, ni muhimu kuanza kwa mazungumzo ya utulivu yatakayomwandaa kisaikolojia kabla ya kueleza hali halisi.

Aidha, anasema anayetoa taarifa anapaswa kuhakikisha mpokeaji yuko mahali salama, si wakati anaendesha gari au kufanya shughuli inayoweza kuhatarisha maisha yake.

Mbali na madhara hayo ya kimwili, wanasaikolojia wanaeleza kuwa taarifa mbaya zinapotolewa bila maandalizi au kwa namna isiyo na huruma, athari zake zinaweza kuwa kubwa, ikiwemo mshtuko mkubwa wa kisaikolojia, kuongezeka kwa hatari ya msongo wa mawazo na wasiwasi.

Katika baadhi ya matukio, watu wenye historia ya magonjwa ya moyo au shinikizo la damu wanaweza kupata madhara Zaidi ya kiafya kutokana na mshtuko mkubwa unaotokana na namna taarifa ilivyotolewa.


Mwongozo wa afya

Wakati watu wengine wanafanya kadri busara inavyowatuma, wataalamu wa afya wamekuwa wakitumia mwongozo unaojulikana kama ‘Spikes’, uliotengenezwa mwaka 2000 na watafiti Walter Baile na wenzake, kusaidia kada hiyo kuwasilisha taarifa ngumu kwa wagonjwa.

Ingawa ulilenga mazingira ya hospitali, kanuni zake zinaweza kutumika hata katika jamii.

Hatua ya kwanza ni kuhakikisha mazingira aliyomo mgonjwa ni tulivu na yanayotoa faragha.

Taarifa ya kifo au ugonjwa mzito haipaswi kutolewa katikati ya watu, kwenye simu ya sauti kubwa au kupitia ujumbe mfupi wa maandishi, ikiwa kuna uwezekano wa kuonana ana kwa ana na mhusika.

Pili, mtoa taarifa anapaswa kufahamu kiwango cha taarifa ambacho mhusika tayari anakijua kuhusu hali inayoelezwa. Hii humsaidia kuanza mazungumzo kwa utaratibu, badala ya kutoa taarifa ya kushtua ghafla.

Tatu, taarifa inapaswa kutolewa kwa lugha rahisi, isiyo ya kifumbo wala ya kutisha. Badala ya kutumia maneno yanayoweza kuleta mkanganyiko, ni muhimu kueleza ukweli kwa upole na kwa heshima.

Nne, ni muhimu kumpa nafasi anayepokea taarifa kuonyesha hisia zake. Kulia, kunyamaza, kushangaa au kuuliza maswali ni sehemu ya kawaida ya mchakato wa kupokea taarifa nzito.

Mwisho, mtoa taarifa anatakiwa kubaki karibu na mhusika, kujibu maswali yake na kuelekeza hatua zinazofuata, badala yake anatakiwa kuondoka mara baada ya kutoa taarifa husika.


Ushuhuda athari za taarifa mbaya


Inawezekana kila mtu ana simulizi yay a namna alivyowahi kupata taarifa mbaya. Kijana David Deogratius analo la kusimulia:

“Niliwahi kupewa taarifa ya kifo cha baba yangu wakati nikiwa chuoni na ndugu yangu alinipigia simu mchana kweupe na kuniambia moja kwa moja baba amefariki, niliumia sana,” amesimulia

Deogratius amesema taarifa hiyo ya kifo bila kutarajiwa ilimletea madhara ya kutoendelea na masomo kwa siku kadhaa.

“Nafikiri ndugu yangu yule angeniandaa maana ilikuwa siku ya darasani yeye anapiga tu simu na kunipa taarifa kama ile, marehemu hakuwa anaumwa na kifo kilikuwa cha ghafla,” ameendelea.

Simulizi ya Deogratius kutoka Dodoma inaonesha umuhimu wa kumwandaa mpokeaji ili kutomletea kumletea madhara mengine kama kuzimia, msongo wa mawazo na hata kujidhuru.

Akieleza namna alivyowahi kupokea taarifa ya kifo cha mtoto wake mchanga aliyezaliwa, mwanaume ambaye hakutaka jina lake kutajwa anasema alipigiwa simu na shemeji yake aliyekuwa hospitali na mkewe na kuambiwa mtoto sio riziki, akimaanisha amekufa.

“Kwa kweli iliniumiza sana kwa kuwa sikutegemea nilidhani mke wangu atajifungua tu salama na mtoto atakuwa mzima. Nilikuwa kazini ilibidi nitoke nje kwanza nikapoteza na hamu ya kazi,” amesema.

Ipo pia simulizi ya Elizabeth John wa Dar es Salaam, anayesema aliwahi kupigiwa simu baada ya kaka yake kufariki dunia ghafla, taarifa iliyomshtua kiasi cha kutaka kuanguka.

“Nilikuwa nimesimama kwenye daladala natoka Kariakoo, nikapigiwa simu ya namba ngeni (wewe ndio Eliza, kaka yako amefariki sasa hivi shuleni) kisha mtoa taarifa akakata simu. Kwa kweli nilitaka kuanguka kwenye daladala,” amesimulia.

Kwa upande mwingine, zipo simulizi nzuri kama ya Sebastian Pius, anayesema aliwahi kupokea taarifa ya matokeo ya mtihani akiwa chuo, ambapo mwalimu aliwaita darasani na kuwaambia wasiwe na hofu kwa sababu kila mmoja amepata matokeo yake.

“Baada ya kutuandaa, alianza kutangaza matokeo. Nilifurahi niliposikia kuwa nilikuwa nimefaulu vizuri,” ameeleza namna ya kuwasilisha taarifa vyema.