Siyo kila wanaooa wazungu wanaukata majuu
Picha na Akili Unde.
Muktasari:
- Sisi tukiwa wanandoa Waswahili ambao tumeishi nje kwa zaidi ya miongo miwili, huwa tunapokea maombi mengi juu ya kuwaunganisha Waswahili wenzetu na mama au wanamume wa kizungu ili kuoana.
Canada. Kumekuwa na maombi yanayotutaka tujadili ndoa za majuu. Hii ni kutokana na vijana wengi hasa wa kiume kupenda au kukamia kuoa wanawake wa kizungu.
Hatuna ugomvi na hili japo kuna mambo wanapaswa kujua kabla ya kuingia kwenye ndoa hizi ambazo siku hizi zimepamba moto kutokana na ujio wa mitandao.
Sisi tukiwa wanandoa Waswahili ambao tumeishi nje kwa zaidi ya miongo miwili, huwa tunapokea maombi mengi juu ya kuwaunganisha Waswahili wenzetu na mama au wanamume wa kizungu ili kuoana.
Japo wengi wanaulizia namna ya kupata wachumba wa kizungu, msukumo mkubwa siyo mapenzi wala kutaka kufunga ndoa bali kutaka kuukata kama wasemavyo watoto wa mjini.
Kadhalika, hata huku japo hatujapata maombi ya kuunganisha wazungu na Waswahili kwa lengo hili hili, kuna uhitaji wa wanaume. Hii ni kutokana na ndoa huku kuwa ngumu kutokana na uhuria uliopo na mfumo mzima.
Kwa mila za Kiafrika, mwanaume humuoa mwanamke na mwanamke huolewa na mwanaume. Hata hivyo, siku hizi kuna lugha ya kuoana ambapo hata mwanamke anaweza kumuoa mwanaume kama ambavyo wanaume wamekuwa wakiwaoa wanawake.
Kuna visa vingi tumesikia hasa nchi jirani ya Marekani ambapo wenza wawili wakienda kwa kasisi kufunga ndoa, huulizwa nani muoaji na nani muolewaji.
Hivyo, si kitu kigeni kusikia mama akisema mimi ndiye namuoa huyu kuwa mume wangu. Kwa Waswahili, tukiondoa shida, hili ni jambo ambalo si halipo bali hata halijulikani.
Sasa tujiulize. Inakuwaje mwanaume anapokubali kuolewa na mwanamke? Kwa malezi na tamaduni ya Kiafrika, je, hili linawezekana? Na kama linawezekana, linatwambia nini? Je, mwanaume anakuwa amekubali kubeba majukumu ya kike na mke ya kiume?
Bado tunadurusu suala hili lau tuliendee na kulijua kwa undani. Tunachojua ni kwamba ndoa za aina hii, mara nyingi, wahusika huingia kwa kuangalia tatizo moja wasijue wanaweza kutengeneza mengine.
Mifano hii
Kuna visa vinavyothibitisha hilo hapo juu. Wapo wanaume wanaoolewa ili waweze kukaa majuu. Hawa, hupitia mambo mengi ikiwamo kuolewa na watu wasiowapenda mbali na kujikuta wakiishi kwa mila na tamaduni ambazo si zao. Mfano, hivi karibuni mwanaume kutoka Kenya alimuua mkewe mzungu na kujimaliza baada ya mke kupiga simu polisi ili waje wamtoe mumewe nyumbani kwao. Kwa nchi za magharibi, hili ni jambo la kawaida.
Mume akishitakiwa kwa kumnyanyasa mke kwa namna yoyote au kutomhitaji tena, anapiga simu polisi nao wanakuja na kumtoa nje baba kwa nguvu na mambo yanaishia hapo.
Kwa mtu ambaye ametoa kila kitu ili aishi majuu na saa nyingine kubeba maboksi kama wasemavyo wengi wanaokuja huku kukimbia umaskini, anajisikiaje mfano wameishajenga nyumba ambayo sasa hawawezi kuishi wala kuimilki.
Hapa, hatujaongelea tofauti za mila ambapo mila za huku zinampa mama nguvu kubwa kuliko baba. Bado hatujaongelea ubaguzi wa rangi na hata kunyonywa kulingana na mtu alivyo hasa ikizingatiwa kuwa mfumo wa huku umejengwa kuwasaidia wenye mfumo na si wageni.
Kutokana na uhuru wa kupita mipaka, si jambo la ajabu kwa mke wa kizungu kupanga kwenda kujivinjari nchi nyingine na wanawake wenzake bila kutegema kama mumewe anataka au hataki.
Je, kwa malezi yetu Waswahili, wahusika wanamezaje kidonge hiki kichungu? Na kama wanakubali kukimeza, je, wanaridhika, kukubali, na kuona ni jambo la kawaida?
Kuna visa vingi tumeshuhudia ambapo wanaume wa Kiafrika wameoa wanawake wa kizungu. Ndoa hizi, hasa zile zitokanazo na uhitaji wa kuishi majuu, huvunjika pale wanandoa wanapokaribia au kumaliza kulipia nyumba zao. Hapo ndipo mama huanza vituko na kuhitimisha kwa kumuitia mume polisi na kuondolewa na yeye akabaki na nyumba na mali nyingine hasa kama wana watoto.
Mbali na hayo juu, wapo wanaoawaacha waume zao kwa sababu mbalimbali za kibinadamu kama vile kutopata kile walichotegemea, kuwachoka, au kushindwa kuendana. Pia, wapo wanaoacha kutokana na kukidhi matarajio yao kama vile kupata mali na watoto na mengine. Hivyo, wahusika kujikuta hawahitajiki tena.
Tumalizie. Kuna sababu nyingine hasa ile hali ya kutofautiana kimila. Mfano, si rahisi mama wa kizungu kukubali kumilikiwa na kutawaliwa na mume kama ilivyo kwenye mfumo dume na mila za Kiafrika, ambapo baba huwa na mamlaka makubwa kuliko baba.