Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bakwata yavunja ukimya sakata la Sheikh Walid

Muktasari:

  • Baraza la Ulamaa la Bakwata lilitangaza kuwasimamisha masheikh watatu wa mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma na Singida kwa kile kilichoelezwa kuwa ni ukiukwaji wa misingi ya kiuongozi ya taasisi hiyo, huku uchunguzi ukiendelea.



Dar es Salaam. Wakati aliyekuwa Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Walid Omar amekabidhi rasmi ofisi kwa Kaimu Sheikh wa Mkoa huo, Abasi Ramadhani, Bakwata imesema inaona yanayoendelea kwenye mitandao ya kijamii na inafuatilia.

Sheikh Walid, leo Julai 18, 2026, amekabidhi rasmi ofisi kwa Kaimu Sheikh wa Mkoa huo aliyeteuliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Abasi Ramadhani, katika hafla iliyofanyika makao makuu ya Bakwata Mkoa wa Dar es Salaam.

Julai 14 mwaka huu, Baraza la Ulamaa la Bakwata lilitangaza kuwasimamisha uongozi masheikh watatu wa mikoa, Sheikh Walid (Dar es salaam), Sheikh Hassan Kiburwa (Singida) na Sheikh Issa Nasor (Kigoma).

Uamuzi huo umezua mjadala mpana ndani na nje ya mitandao ya kijamii, hususan kuhusu Sheikh Walid, ambapo wananchi, viongozi wa dini na wadau mbalimbali walitoa maoni yanayokinzana kuhusu hatua hiyo kupitia majukwaa ya Facebook, X na mitandao mingine ya kijamii.

Katika majukwaa ya Facebook na X, watumiaji wamekuwa wakisambaza picha, video fupi na kumbukumbu mbalimbali zinazomwonyesha Sheikh Walid akihubiri, akiongoza swala, kushiriki shughuli za kijamii na kutoa nasaha katika matukio tofauti ya kidini na kijamii.

Watoa maoni wameibua hisia kadhaa huku baadhi wakidai Sheikh Walid amekuwa karibu na jamii na amejenga ushawishi kutokana na mahubiri yake, namna anavyoshughulikia changamoto za waumini na uwezo wake wa kuwasiliana na makundi mbalimbali ya kijamii.

Mbali na waumini wa Kiislamu, baadhi ya viongozi wa dini nyingine pia wamejitokeza kutoa maoni yao kuhusu tukio hilo. Miongoni mwao ni Mchungaji Anthony Lusekelo, maarufu kama Mzee wa Upako wa Kanisa la Maombezi.

Katika video iliyosambazwa kupitia mitandao yake ya kijamii, Mchungaji Lusekelo, alisema hakutarajia kuona Sheikh Walid akiondolewa katika nafasi aliyokuwa akiitumikia.

Alisema licha ya umri wake, Sheikh Walid ameonyesha busara na uwezo wa kuwasiliana na watu wa makundi mbalimbali ya dini na kijamii.

“Wewe mpiganie Mungu, wewe bado kijana wala huna makosa. Sheikh Walid ana uwezo wa kuzungumza na watu hata ambao sio Wakristo wala Waislamu...” alisema Mchungaji Lusekelo katika ujumbe wake wa video.


Bakwata inaona

Akizungumzia mjadala unaoendelea katika mitandao ya kijamii kumhusu sheikh huyo, Katibu wa Baraza la Ulamaa la Bakwata, Sheikh Hassan Chizenga, amesema taasisi hiyo inaona na kufuatilia maoni yote yanayotolewa na wananchi pamoja na waumini.

Sheikh Chizenga amesema kwa sasa Baraza hilo halina mpango wa kuingia katika mjadala wa hadharani kuhusu suala hilo, likiamini kuwa wakati ukifika litaeleza msimamo wake kwa kina.

“Tunawaacha kwanza wazungumze wanayotaka kuzungumza, nasi tukiona kuna haja ya kuzungumza tutawaita waandishi wa habari na kuzungumza,” alisema.

Sheikh Chizenga alisisitiza kuwa Bakwata ni taasisi inayofuata katiba, kanuni na taratibu zake katika kufanya maamuzi, hivyo hatua zilizochukuliwa haziwezi kutazamwa kama maamuzi ya kiholela.

Alisema endapo viongozi wa taasisi hiyo wataona kuna ulazima wa kutoa ufafanuzi zaidi kwa umma, watafanya hivyo kupitia njia rasmi.