Jeshi la Polisi latoa hakikisho la usalama kwenye Eid el Fitr

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) David Misime
Muktasari:
- Jeshi la Polisi limeonya jamii kuhusu kushindana na maji ya mvua yanapokuwa yanatembea kwa kasi tofauti.
Dar es Salaam. Wakati waumini wa dini ya Kiislamu wakitarajia kusherehekea sikukuu ya Eid el Fitr wiki hii, Jeshi la Polisi limetoa hakikisho la usalama, likisisitiza wananchi kuzingatia sheria.
Waumini wa dini ya Kiislamu nchini na duniani kila mwaka husherehekea Sikukuu ya Eid el Fitr baada ya kufanya ibada ya kufunga kwa takribani siku 30 za mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Hakikisho la usalama limetolewa leo Jumanne Aprili 9, 2024 na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime kupitia taarifa kwa vyombo vya habari.
Jeshi hilo limesema litakuwa na mikakati kuhakikisha waumini na Watanzania kwa ujumla wanashiriki ibada na kusheherekea sikukuu katika mazingira ya amani, utulivu na usalama.
“Sikukuu ya Eid huambatana na ibada katika misikiti na Baraza la Eid, waumini hukusanyika kwa wingi kwa ajili ya sala, hivyo tutahakikisha kunakuwa na usalama,” imeeleza taarifa ya jeshi hilo.
Hata hivyo, Misime amesisitiza ili kufanikisha ulinzi wa amani katika sikukuu hiyo, wananchi wanapaswa kuzingatia kanuni za kiusalama kwa kujiepusha na vitendo vinavyosababisha uvunjifu wa sheria.
Kwa upande wa usalama barabarani, jeshi hilo limetaka kila Mtanzania kuhakikisha anazingatia sheria ili kuepuka ajali zinazosababishwa na uzembe.
Wazazi na walezi, wametakiwa kuwalinda watoto ipasavyo wanapoenda maeneo yaliyoruhusiwa kwa kuhakikisha wanakuwa na ulinzi wa mtu mzima.
“Kila mmoja wetu anakumbushwa kuzingatia tahadhari zinazoendelea kutolewa kuhusu mvua zinazoendelea kunyesha na kamwe mtu asijaribu kushindana na maji ya mvua yanayotiririka kwa kasi tofauti na siku nyingine katika eneo lolote lile kwani kunaweza kuhatarisha maisha,” amesema.