Polisi yawahakikishia wananchi usalama Sikukuu ya Pasaka

Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, SACP, Jumanne Muliro katika moja ya tukio akizungumza na waandishi wa habari. Picha na mtandao
Muktasari:
- Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema hali ya usalama kwa jiji hilo ni shwari na kwamba litaendelea kusimamia mifumo ya kiusalama kuzuia matukio ya uvunjivu wa amani kuelekea sherehe ya Sikukuu ya Pasaka.
Dar es Salaam. Kuelekea Sikukuu ya Pasaka, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limesema linaendelea kusimamia mifumo ya kiusalama kuzuia matukio ya kihalifu, huku likishauri wenye nia hiyo kuacha ili kujiepusha na msuguano wa kisheria.
Pasaka itasherekewa Aprili 9, siku ya Jumapili, ni sikukuu inayofsnyika kila mwaka yenye maana kubwa zaidi kiimani kwa Mkristo yeyote kuliko sikukuu nyingine kwa sababu ni ukumbusho wa kufufuka kwa mkombozi wao Yesu Kristo siku ya tatu baada ya kusulubiwa, kufa na kuzikwa kwake.
Akizungumza na vyombo vya habari leo, Aprili 06, 2023 Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, SACP, Jumanne Muliro amesema hali ya usalama ni shwari kwa jiji hilo, lakini hawatasita kuwachukulia hatua watakaobainika kupanga kutenda matendo kinyume na sheria.
“Jeshi linaendelea kutahadharisha juu ya kuwepo kwa mtizamo kuwa kila inapokaribia sikukuu mbalimbali ikiwemo (Pasaka) baadhi ya watu hujenga fikra za kujihusisha na vitendo vya kihalifu kwa kisingizio kuwa wanatafuta pesa za sikukuu,”amesema Muliro.
Amesema Jeshi hilo halikubaliani na hali matendo ya kuvuruga usalama hivyo ufuatiliaji kuhakikisha amani inatawala utakuwa wa kiwango cha juu na yeyote atakayejihusisha na vitendo vya kihalifu atakamatwa.
“Akikamatwa atahojiwa kwa kina na baadaye atafikishwa kwenye nyombo vingine vya kisheria kulingana na ushahidi utakaokuwa umekusanywa,”amesema.
Kamanda Muliro amesema jeshi hilo linaendelea kuwashukuru wananchi wanaochukia uhalifu na kuendelea na kuwataka kutoa taarifa mapema wakioa viashiria vya uvunjivu wa usalama ili wahalifu waweze kushughulikiwa haraka kwa mujibu wa sheria.