Serikali yavunja mkataba na mkandarasi Barabara ya Tanga - Bagamoyo

Muktasari:
- Uamuzi wa Serikali kuvunja sehemu ya mkataba na Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group ni hatua ya wazi ya uwajibikaji na kulinda masilahi ya umma.
Dar es Salaam. Serikali imevunja mkataba na Mkandarasi wa Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group anayejenga barabara ya Tanga - Pangani - Mkwaja - Bagamoyo (Makurunge), baada ya kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa mkataba licha ya kulipwa zaidi ya Sh40 bilioni.
Hatua hiyo imetangazwa leo Mei 12, 2025 na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa kipande cha barabara hiyo katika Wilaya ya Pangani, Mkoa wa Tanga.
"Mkandarasi huyu ametuangusha. Tumeshamlipa zaidi ya Sh40 bilioni lakini kazi imefikia asilimia 48 tu. Vifaa hajaleta, wafanyakazi hawajafika wote, hivyo siwezi kukubali mradi huu uendelee kutelekezwa. Nimemnyang’anya sehemu ya kazi," amesema Ulega.

Waziri huyo ameeleza kuwa Serikali imeamua kuondoa kipande cha kilomita 25 ambacho hakijaguswa, na kitakwenda kutangazwa upya kwa zabuni ili mkandarasi mwenye uwezo apatikane mara moja.
“Tunachofanya hapa ni kulinda masilahi ya nchi. Tukivunja mkataba wote, tungepoteza miezi sita hadi mwaka mzima kupata mkandarasi mpya, na wananchi wangepata hasara ya kuchelewa kwa mradi huu muhimu,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Ulega ameagiza mkandarasi huyo kulipa fidia kwa Serikali kutokana na ucheleweshaji wa mradi, huku akimtaka Katibu Mkuu wa Ujenzi, Balozi Aisha Amour, kuhakikisha jina la kampuni hiyo linaingizwa kwenye orodha ya makandarasi wasiotekeleza vizuri miradi ya Serikali.
Kwa upande wake, msimamizi wa mradi kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Julius Msofe amesema hadi sasa ujenzi wa barabara hiyo umefikia asilimia 47.82, licha ya kuwa muda wa mkataba wa miezi 36 umeisha tangu Machi 31, 2025.

Waziri Ulega pia ameagiza tathmini ya fidia ya ucheleweshaji wa mradi huo ifanyike ili Serikali ilipwe.
Mradi huo wa barabara unatarajiwa kuwa kiungo muhimu cha maendeleo kati ya mikoa ya Tanga na Pwani, na kusaidia kuinua uchumi wa wananchi wa maeneo ya Pangani, Mkwaja, Mkange na Bagamoyo.