Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watishia kuchoma shule kisa kukataliwa mahafali

Wanafunzi wa shule ya Sekondari Milambo wakisiliza maagizo ya mkuu wa mkoa wa Tabora. Picha na Hawa Kimwaga

Muktasari:

  • Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Milambo iliyopo Manispaa ya Tabora, wamedaiwa kufanya vitendo ambavyo ni kinyume na taratibu za shule ikiwemo kuwa na simu, kutoroka shule kwenda kuzurura mitaani na kufanya vitendo mbalimbali vya kihalifu.

Tabora. Wahitimu wa kidato cha sita zaidi ya 130 katika Shule ya Sekondari Milambo, iliyopo mkoani Tabora wametakiwa kuondoka shuleni hapo haraka baada ya kumaliza mitihani yao, kutokana na tishio la kuchoma shule hiyo.

Agizo hilo limetolewa  leo Mei 12, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha akiwataka kuondoka shuleni hapo chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi, kwani kitendo hicho ni kosa kubwa na haliwezi kufumbiwa macho.

Wanafunzi hao zaidi ya 130 wamedaiwa kula njama ya kutaka kuchoma shule, kutokana na kuzuiliwa kufanya mahafali baada ya kumaliza mitihani yao ya kidato cha sita, ambapo kitendo hicho kimetajwa kuwa ni uvunjifu wa amani.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paulo Chacha akiongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mkoa wa Tabora amelazimika kufika shuleni hapo na kuwaamuru waondolewe mara moja, huku baadhi yao wakiwa chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha utovu wa nidhamu.

“Hatuwezi tukavumilia eti kisa mahafali, wanafunzi wachome shule na mimi nimekaa hapa nafanya nini na kamati yangu ya ulinzi na usalama iko hapa,” amesema Chacha.

Aidha Chacha amewataka viongozi wa shule hiyo kuwachukulia hatua kali za kisheria, ikiwemo kuwafukuza shule wanafunzi ambao watakuwa wakienda kinyume na sheria za shule hiyo, ili kuhakikisha nidhamu inarejea katika shule hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Paul Chacha akitoa maelekezo katika shule ya sekondari Milambo mara baada ya kupata taarifa za wahitimu kutishia kuchoma shule hiyo kufuatia kukataliwa kufanya mahafali. Picha na Hawa Kimwaga

Hata hivyo amelitaka Jeshi la Polisi kuendelea kuimarisha ulinzi katika eneo lote la shule hiyo, kwani kuna wanafunzi ambao bado wanaendelea na masomo, lakini wapo wa kidato cha sita ambao wanaendelea na mitihani ya kuhitimu.

“Askari hakikisheni ulinzi unaimarika hapa, lazima watu wawe salama wakati wote katika eneo hili,” amesisitiza.

Tukio hilo si la kwanza kwa mwaka huu, kwani Februari 25, 2025 Bodi ya Shule ya Sekondari Geita iliwafukuza shule wanafunzi saba na kuwasimamisha kwa vipindi tofauti wengine 64 wa kidato cha sita, baada ya kubainika kushiriki kwenye vurugu zilizotokea shuleni hapo Februari 20, 2025 na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh2.9 milioni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi leo Februari 24, 2025, uchunguzi uliofanywa na jeshi hilo kwa kushirikiana na bodi, ulibaini vurugu hizo zilifanywa na wanafunzi 71 wa kidato cha sita.

Baadhi ya viongozi wa serikali ya mkoa wa Tabora walioongozana na mkuu wa mkoa wa Tabora katika shule hiyo. Picha na Hawa Kimwaga.

Mbali na waliofukuzwa, wanafunzi 19 wamesimamishwa kuendelea na masomo hadi Mei 5, 2025 huku wengine 45 wakisimamishwa kwa muda wa siku 21.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo alisema katika uchunguzi wanafunzi 71 walihojiwa na kubainika kuhusika kwenye tukio hilo.