Wananchi wachoma moto gari lililowagonga wanafunzi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi
Mwanza. Watu wenye hasira wameteketeza kwa moto basi dogo la abiria linalofanya safari zake kati ya jiji la Mwanza na eneo la Igombe Wilaya ya Ilemela baada ya kuwagonga watoto wawili waliokuwa wakienda shuleni na kusababisha kifo cha mmoja wao.
Shuhuda wa ajali hiyo iliyotokea leo Juni 7 eneo la Kayenze Ndogo Kata ya Igombe, Baraka Mathew ameiambia MCL Digital kuwa hasira za wananchi hao zilichochewa na kitendo cha dereva wa gari hilo aina ya Isuzu Journey aliyefahamika kwa jina moja la Maguberi kutimua mbio na kulitelekeza gari hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amethibitisha taarifa hizo na kuahidi kutoa taarifa baadaye.