Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wahitimu sasa watumia vyeti kuombea mikopo ya kausha damu

Muktasari:

  • Kwa wengi, shahada ya chuo kikuu iliwahi kuwa ishara ya uthabiti, heshima na matumaini ya maisha bora, lakini sasa imegeuka kuwa "sarafu ya dharura" kwa wahitimu wanaokumbwa na hali ngumu ya maisha. 

Dar es Salaam. Katika kipindi ambacho ukosefu wa ajira na ajira zisizo rasmi unazidi kuwa tatizo kubwa, wahitimu wa vyuo vikuu nchini Tanzania wameamua kutumia vyeti vyao vya taaluma kama dhamana ya kujikimu kimaisha kwa kuombea mikopo ikiwamo ile maarufu kwa jina la ‘kausha damu’.

Kwa wengi, shahada ya chuo kikuu iliwahi kuwa ishara ya uthabiti, heshima na matumaini ya maisha bora, lakini sasa imegeuka kuwa "sarafu ya dharura" kwa wahitimu wanaokumbwa na hali ngumu ya maisha.

Jackson Gwandu, mhitimu wa sayansi ya siasa kutoka Iringa, anasema:

“Nilihitimu miaka minne iliyopita. Nimewahi kuwa mhudumu wa malipo, mtoa huduma kwenye kituo cha simu, na sasa ni muuzaji dukani. Kazi hizi hazihitaji ulichosomea. Niliwahi kuweka cheti changu rehani ili nipate mkopo wa Sh250,000. Ilionekana haina maana kukihifadhi cheti kwenye droo huku nikiwa na njaa,” anasema.

Si yeye pekee, yupo Eliza Komba (jina si lake) anayesema: “Sikuwahi kufikiria kuwa shahada yangu ya elimu ingeishia kwenye droo ya mtu mwingine, eti kwa sababu nilihitaji Sh300,000 kulipa kodi na ada ya shule ya mwanangu,”

Komba, mwalimu mwenye umri wa miaka 29 anasema aliajiriwa na shule binafsi mkoani Mbeya.

Mshahara wake wa mwezi hauzidi Sh400,000 na hulipwa kwa kuchelewa; pia shule yake haitoi mikopo wala malipo ya mapema.

Kama ilivyo kwa wenzake wengi, anasema alilazimika kukopa kwa mtu binafsi ambaye alimtaka awasilishe cheti chake halisi cha shahada kama dhamana.

“Alisema ndiyo njia pekee ya kuhakikisha nitalipa mkopo. Nilipomkabidhi, nilihisi kama nimekabidhi sehemu ya utambulisho wangu,” anasimulia.

Hadithi ya vijana hawa wawili si ya kipekee.

Kote nchini, wahitimu wa vyuo vikuu na vya kati hasa wanaofanya kazi zisizo na uhakika au zenye malipo duni, wanazidi kuweka vyeti vyao rehani ili kupata mikopo midogo kutoka kwa watu binafsi au taasisi zisizo rasmi za kifedha.

Wengine wanakubali kufanya hivyo kwa kiasi kidogo cha mkopo wa Sh200,000.

Hivi karibuni, wakati wa uchaguzi wa Tume ya Walimu mkoani Njombe, Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Juma Sweda alitoa onyo kali kwa walimu akisema:

“Acheni kutumia vyeti vya taaluma kama dhamana ya mkopo.”

Alieleza matukio ya kusikitisha ambapo walimu walishindwa kuwasilisha vyeti vyao wakati wa uhakiki, kwa kuwa vilikuwa mikononi mwa wakopeshaji kutokana na madeni ambayo hawajayalipa.

“Hii ni hatari,” alionya Sweda na kuongeza: “Hivi vyeti vilichukua miaka kuvikamilisha. Ni nyaraka za mtu binafsi na za kitaifa. Walimu wanapaswa kuvithamini na kuvilinda.”


Nguvu ya karatasi

Lakini kwa wengi, ukweli mchungu ni kwamba vyeti hivi ambavyo hapo awali vilikuwa ni alama ya matumaini vimepoteza thamani ya kiuchumi.

Godwin Deus, mhitimu mwenye miaka 33 aliyesomea kilimo ngazi ya stashahada, analima mihogo mkoani Lindi.

“Kila msimu wa kilimo nahitaji mtaji kidogo wakati mwingine Sh150,000 tu kumuajiri mtu au kununua mbolea,” anasema.

Anaongeza: “Benki zinahitaji vitu ambavyo sina: nyumba, gari, au hati ya ardhi. Kwa hiyo natumia cheti changu. Ndani ya saa chache napata fedha.”

Kwake, cheti si kingine bali ni zana ya kuishi… “Ni kama jembe au panga. Unatumia ulichonacho ili kulisha familia yako.”

Wataalamu wa elimu wanasema kuwa, ingawa hali hii inaeleweka kutokana na ugumu wa maisha, tabia ya kutumia vyeti kama dhamana,  ni mwenendo wa kutisha unaoweza kudhoofisha thamani ya elimu.

“Vyeti ni vya mtu binafsi, ni  vya siri, na haviwezi kurudiwa kirahisi,” anasema Dkt Lilian Mbwambo, mtaalamu wa sera za elimu jijini Dar es Salaam.

“Kama watu wanalazimika kuvitumia kama dhamana, hiyo ni ishara kuwa kuna tatizo kubwa kwenye mifumo yetu ya kifedha na ajira. Tunapaswa kujiuliza: kwa nini mtu mwenye shahada ya uhasibu, au stashahada ya uuguzi, au mwalimu mwenye uzoefu wa miaka mitano hawezi kupata mkopo wa maana kutoka taasisi rasmi? Je, hali hii inaonyesha nini kuhusu uchumi wetu?” anahoji.


Gharama ya ukosefu wa ajira

Kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), zaidi ya wahitimu 800,000 huingia kwenye soko la ajira nchini kila mwaka, lakini ni chini ya 100,000 wanaopata ajira rasmi.

Tofauti hii huacha maelfu wakihangaika katika ajira za kujikimu zisizo na uhakika, zenye mishahara midogo, na mara nyingine za kinyonyaji.

“Elimu iliwahi kuwa daraja la usawa wa kijamii,” anasema mtaalamu wa sosholojia kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Alfred Magessa.

Anaongeza: “Lakini sasa tunaona matokeo kinyume chake. Mtu anapokuwa na elimu zaidi, ndivyo anavyozidi kuvunjika moyo kwa sababu matarajio hayakidhiwi. Si ajabu kuona wahitimu wakihisi kuwa vyeti vyao havina maana isipokuwa vikigeuzwa kuwa fedha. Ni hali ya kusikitisha, lakini baadhi ya wahitimu wanaanza kuwaonea wivu wajasiriamali wadogo ambao hawakupita darasani lakini wanamiliki nyumba, pikipiki (boda boda), na vibanda vya chakula vinavyonawiri.”

Sekta ya benki pia haijabaki nyuma. Taasisi rasmi za kifedha mara nyingi huweka masharti magumu ambayo vijana wengi hawakidhi.

“Kuna uwiano mbovu kati ya bidhaa za kifedha na hali halisi ya vijana wengi wa Kitanzania,” anasema Aisha Mwalimu, mtaalamu wa ujumuishaji wa kifedha na kuongeza: “Kama benki zinahitaji hati za ardhi kutoka kwa mtu aliyehitimu mwaka jana tu, basi zinawafungia wengi nje.”

Katika pengo hilo, wakopeshaji binafsi wakati mwingine wanaokaribia kuwa wanyonyaji, hujitokeza na kutoa mikopo ya haraka yenye masharti magumu ya marejesho. Hapo ndipo mahitaji ya cheti yanapoingia.


Je, thamani ya elimu inashuka?

Mwenendo huu unaozidi kushika kasi wa kutumia vyeti kama dhamana ya mkopo, unazidi kuchochea mjadala mpana zaidi: je, thamani ya elimu nchini Tanzania inazidi kushuka?

Mwalimu mstaafu, Bakari Heri anasema kwa kinachotokea na kwa kuzingatia thamani ya kile cheti tena cha elimu ya juu, ni dhahiri kuna dosari mahala.

‘Unajua cheti cha elimu ya juu ni kama kito cha thamani, hata kwenye ajira tunapeleka vyeti vya nakala tu na kama ni vyeti rasmi, labda kukaguliwa na kisha mhusika anarudishiwa. Sasa leo uniambie kwa sababu ya mkopo unachukua cheti changu halisi, hili ni tatizo.’’ anafafanua.

Hata hivyo, baadhi ya wadau wa elimu wanapinga mtazamo huo.

“Thamani ya elimu si tu ya kiuchumi,” anasema mtaalamu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia aliyeomba kutotajwa jina.

Anaongeza: “Elimu hufungua milango, hujenga fikra pana, na kuandaa fursa nyingi, si za haraka, lakini za maisha.”

Hata hivyo, anakiri kuwa kuna haja ya dharura ya kuimarisha ajira, kuwapa vijana mwongozo wa kitaaluma, na kubuni mifumo mbadala ya kifedha.

“Tunapaswa kuwalinda vijana wetu dhidi ya wakopeshaji wa kiharamia. Lakini zaidi ya hapo, tunapaswa kuwajengea njia za kuhakikisha elimu yao inakuwa na maana katika maisha yao,” anasema.

Kile kilichoanza kama hatua ya mtu mmoja aliyekata tamaa, sasa kinageuka kuwa janga la kitaifa; janga linalotishia mustakabali wa vijana walioelimika na heshima ya taaluma nchini.

Kadri taifa linavyoendelea kusonga mbele kwenye ajenda ya maendeleo, huenda huu ndiyo wakati mwafaka wa kuwa na mjadala wa kitaifa kuhusu maana halisi ya thamani ya shahada na kama inapaswa kweli kubadilishwa kwa kiasi kidogo hivyo, kisa mikopo! 


Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917.