Polisi wataka jamii ishiriki miradi ya ulinzi, usalama

Muktasari:
- Kamanda wa Polisi Kamanda Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amewaomba wananchi kuendeleza ushirikiano na jeshi hilo, hasa kwenye utoaji wa taarifa wa viashiria vya uhalifu
Mufindi. Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amezindua kituo kipya cha polisi kilichopo katika kijiji cha Rungemba wilayani hapa huku akiomba wadau kusaidia miradi ya ulinzi na usalama.
Miongoni mwa wadau waliochangia ujenzi wa kituo hicho kilichojengwa kwa zaidi ya Sh40 milioni ni kiwanda cha Lush Chanzo kinachotengeneza samani kwa kutumia mabaki ya miti.
Akizungumza na wananchi katika uzinduzi huo jana, Kamanda Bukumbi amewashukuru wamiliki wa kiwanda hicho huku akisema suala la ulinzi na usalama kwa wananchi ni jambo la muhimu kwa uchumi wa nchi.
Amewaomba wananchi wa maeneo hayo kuendeleza ushirikiano na Jeshi la Polisi hilo hasa kwenye utoaji wa taarifa zenye viashiria vya uhalifu.
"Unapoona kiashiria cha uhalifu toa taarifa kwenye vyombo husika ili waweze kuzifanyia kazi, lakini niwaahidi huduma bora zitakazotolewa kituoni hapo ikiwa ni pamoja na kuendeleza ushirikiano baina ya Jeshi la Polisi na wananchi," amesema Bukumbi.
Mwakilishi kutoka kwenye kiwanda hicho, Justine Mligo amesema ushirikiano mzuri uliopo baina ya Jeshi la Polisi na wananchi wa eneo hilo umewezesha kukamilisha ujenzi huo.
"Kufanikisha ujenzi wa kituo hiki sio sisi pekee yetu bali ni ushirikiano mzuri uliopo baina ya wananchi na kiwanda tunashukuru, wananchi wameweza kushiriki kulinda vifaa tulivyokuwa tunaviacha kwa ajili ya ujenzi huo," amesema Mligo.
Upendo Mbembati, mkazi wa Kijiji cha Rugemba amesema kwa muda mrefu kijiji hicho hakikuwa na kituo cha polisi, hivyo walikuwa wakilazimika kufuata huduma katika kituo cha wilaya kilichopo Mafinga kwa ajili kupata huduma hiyo.