Jela maisha kwa kumbaka mtoto wa miaka 10

Muktasari:
- Mkazi wa Mlandege Manispaa ya Iringa Method Muhimba amehukumiwa kifungo cha maisha jela na kulipa faini ya Sh5 milioni kwa kukutwa na hatia ya kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 10 aliyekuwa akisoma darasa la tano.
Iringa. Mahakama ya Wilaya ya Iringa imemuhukumu kifungo cha maisha jela na kulipa faini ya Sh 5 milioni Method Muhimba (33) baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 10 aliyekuwa akisoma darasa la tano.
Muhimba ambaye ni mkazi wa Mlandege Manispaa ya Iringa alikuwa akijishughulisha na biashara ndogondogo ambazo wanaozifanya huwa maarufu kwa jina la machinga.
Method aliyekuwa akiishi nyumba moja na familia ya mtoto huyo kama wapangaji ambapo siku ya tukio mtuhumiwa alimuita mtoto huyo chumbani kwake akamfanyia kitendo hicho na baada ya kumaliza alimuahidi kumpa pesa ya kununulia chipsi.
Wazazi wa mtoto huyo mara kadhaa wamekuwa wakishinda katika shughuli zao na mtoto alikuwa akirudi nyumbani na kushinda peke yake.
Mama wa mtoto huyo aligundua mwanaye kuwa hayupo sawa na baada ya kumuuliza alimwambia kitendo alichofanyiwa na Method ndipo juhudi za kumkamata zikafanyika.
Kesi hiyo ilikuwa na mashahidi watano akiwepo Daktari aliyempima mtoto huyo na kugundua kuwa alikuwa na michubuko ya kuingiliwa.
Kesi hiyo imesimamiwa na waendesha mashtaka wa Serikali Nashoni Saimon na Blandina Manyanda ambao waliiambia Mahakama kuwa mshtakiwa hana taarifa yoyote ya kihalifu lakini kutokana na tukio hilo waliiomba mahakama kutoa adhabu kali ili kuwa fundisho kwake na kwa wengine wenye tabia hizo.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mkuu Said Ally Mkasiwa amesema mahakama imepitia ushahidi wa pande zote mbili na kujiridhisha kuwa upande wa Jamhuri umeweza kuthibitisha kuwa tukio la ubakaji lilifanywa na Method kwa binti huyo wa miaka 10.
Method alipopewa nafasi ya kujitetea alisema kuwa yeye ni mfanyabiashara mdogo na ana ndugu wanamtegemea na kuwa mguuu wake mmoja umevunjika hivyo hawezi kufanya kazi ngumu na nzito.
Hata hivyo mahakama ikamuhukumu kifungo cha maisha jela na faini ya Sh5 milioni kwa kosa la kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 10 aliyekuwa akisoma darasa la tano.