Jamhuri ilivyojibu pingamizi kesi ya Niffer na wenzake
Muktasari:
- Niffer na wenzake wanakabiliwa na kesi ya uhaini, kufuatia maandamano ya kupinga uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025. Mawakili wao wakiongozwa na Peter Kibatala walipinga pamoja na mambo mengine uhalali wa hati ya mashtaka, leo Jamhuri imemjibu hoja hizo na Mahakama imepanga kutoa uamuzi wa pingamizi hilo Novemba 25.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam imepanga kutoa uamuzi wa uhalali wa hati ya kesi ya uhaini inayomkabili mfanyabiashara Jenifer Jovin (26), maarufu Niffer na wenzake 21, Novemba 25, 2025.
Mahakama hiyo imepanga tarehe hiyo kutoa uamuzi huo, leo Jumanne, Novemba 11, 2025, baada ya kukamilisha usikilizwaji wa pingamizi dhidi ya hati hiyo lililotolewa na jopo la mawakili wao linaloongozwa na Peter Kibatala.
Leo Mahakama hiyo imesikiliza majibu ya Jamhuri pamoja na majibu ya utetezi dhidi ya majibu ya Jamhuri.
Niffer ambaye alikamatwa mapema kabla ya siku ya kupiga kura na wenzake hao waliokamatwa siku ya kupiga kura, Oktoba 29, 2025 katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, wakihusishwa na maandamano ya kupinga uchaguzi huo. Walipandishwa kizimbani mahakamani hapo Ijumaa, Oktoba 7, 2025.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo Wakili Kibatala aliieleza Mahakama wateja wao walipokuwa Polisi waliteswa kwa kupigwa kwa lengo la kuwashinikiza kukubali kuandika na au kusaini maelezo yao ya onyo, na licha ya wengine kujeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao lakini hawakuwahi kupatiwa matibabu.
Hivyo aliomba Mahakama ielekeze msimamizi wa gereza ambako watapelekwa mahabusu iwapatie matibabu na taarifa za matibabu yao ziwasilishwe mahakamani kuwa sehemu ya kumbukumbu za kesi hiyo.
Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya anayesikiliza kesi hiyo katika hatua hiyo ya uchunguzi wa awali kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu yenye mamlaka ya kuisikiliza, alikubaliana nayo na akatoa maelekezo hayo.
Pia, Kibatala alipinga hati ya mashtaka akidai ina kasoro kwa kujumuisha makosa mawili yaani kula njama na kosa mama la uhaini, ambayo hayapaswi kuwekwa katika hati moja.
Baada ya upande wa utetezi kumaliza kuwasilisha hoja zake, kesi hiyo iliahirishwa mpaka leo kwa ajili ya upande wa mashtaka kujibu hoja hizo.
Majibu ya Jamhuri
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Hemed Halfan, akijibu hoja hizo, kuhusu madai ya washtakiwa kupigwa wakiwa kituo cha Polisi ili wasaini maelezo yao ya onyo, amesema hoja hiyo imeletwa kabla ya wakati wake.
Wakili Hemed amesema hoja hiyo haikupaswa kuletwa katika hatua hii ya kesi hiyo katika Mahakama ambayo haina mamlaka ya kuisikiliza.
Pia amesema ni maneno yanayohitaji uthibitisho na kwamba yametolewa na wakili (Kibatala) ambaye si shahidi na wala hakuwahi kuapishwa kuwa shahidi.
"Kuonesha kuwa yameletwa sehemu isiyohusika, katika hatua hii hakuna mahali ambako upande wa mashtaka umetoa taarifa utayatumia maelezo haya na hayo maelezo hayako hata mbele yako Mheshimiwa Hakimu, kwa hiyo ni taarifa za kufikirika na hivyo yanainyima uhalali mahakama yako kusema chochote," amesema.
Kuhusu huduma ya matibabu, pia wakili Hemed amedai imeletwa mahali pasipohusika kwa kuwa mpaka sasa hakuna malalamiko washtakiwa hao wakiwa Polisi hawakupata huduma ya matibabu.
Kuhusu hoja ya kasoro ya hati ya mashtaka, Wakili Hemed amedai katika hatua hii Mahakama hiyo haina mamlaka ya kuzungumzia chochote kuhusiana na hati ya mashtaka, kwa kuwa ni ya ukabidhi tu na itakayoisikiliza ni Mahakama Kuu.
Katika kusisitiza hoja hiyo, amerejea uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika kesi ya Jamhuri dhidi ya Faridi Hadi Ahmed na wenzake 21, rufaa ya Mwaka 2015,
"Kwa hiyo Mheshimiwa Hakimu mahakama hii isijiingize huko kuanza kudadavua kuhusiana na uhalali wa hati ya mashtaka ambayo haina uwezo nayo," amesema.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Clement Kato amedai pingamizi hilo halipaswi kuletwa kabla mshtakiwa hajajibu shtaka lake (kukubali au kukataa).
Amedai msimamo huo umewekwa na Mahakama ya Rufani katika rufaa namba 250 ya 2012 kati ya SHU Chin Tai na wenzake dhidi ya Jamhuri maarufu kama kesi ya Samaki wa Magufuli.
Kuhusu hoja ya washtakiwa kuteswa Wakili Kato amedai mahakama imekataa mara nyingi kuwa wakili hawezi kuwa shahidi kwenye kesi na kwamba kitendo cha wakili kuleta ushahidi na kutaka uingie kwenye kumbukumbu si sahihi.
Amedai katika kesi hiyo Wakili Kibatala alimsimamisha mmoja wa washtakiwa na kuionesha mahakama majeraha yake akaomba maelezo hayo yaingie kwenye rekodi, akidai kuwa katika hali hiyo Wakili Kibatala alikuwa anatoa ushahidi jambo ambalo halikubaliki.
Majibu ya Kibatala
Akijibu hoja za Jamhuri amesema waliomba maelezo hayo yaingie kwenye kumbukumbu awali kabisa ili wakati itakapoletwa isionekane kuwa imeletwa kwa kuushtukiza upande wa mashtaka.
Amedai hoja iliyotolewa ni ya kisheria na uteswaji ni jambo linalozuiwa na hata mikataba ya kimataifa.
Amedai hakuna wakili aliyetoa ushahidi bali alitoa hoja kuiomba mahakama na kwamba si kwamba katika mazingira yote wakili anazuiwa kutoa kiapo, akitaja mashauri mbalimbali ambayo mawakili wanatoa viapo.
Kuhusia hoja ya matibabu amedai kuwa hilo mahakama ilishalitolea maelekezo hivyo haina mamlaka tena kilizungumzia, na kama upande wa mashtaka hawakuridhika na maelekezo hayo wanapaswa kufuata taratibu nyingine za kisheria.
Kuhusu hati ya mashtaka amesema kuwa walieleza kwamba kuwa ni makosa kumshtaki mtu kwa kula.njama pamoja na shtaka mama lenyewe ( uhaini na kwamba walitoa na uamuzi wa Mahakama ya Rufani kuunga mkono hoja hiyo.
Wakili Kibatala amesisitiza kuwa Mahakama hiyo ina mamlaka ya kushughulikia shtaka la kula njama, hivyo ikiona kuwa limeletwa kimakosa ina mamlaka ya kuliondoa.
"Kwa hiyo tunasisitiza kuwa shtaka la kula njama halikustahili kuwepo na tunaomba mahakama hii iliondoe, kwani ina mamlaka kamili ya kulishughulikia," amesisitiza Wakili Kibatala.
Kuhusu hoja ya kwamba pingamizi hilo limeletwa kabla ya wakati wake kwa kuwa washtakiwa hawajatakiwa kujibu shtaka, amesema kesi rejea zilizotolewa na upande wa mashtaka zina mazingira tofauti na mazingira ya kesi hiyo.
Amedai katika kesi ya Samaki wa Magufuli washtakiwa walishasomewa mwenendo kabidhi (committal Proceedings) na wakati wakiwa Mahakama Kuu kabla ya kusomewa hati ya mashtaka ndipo mawakili wakaibua hoja ya pingamizi.
Amesisitiza kwa namna walivyoleta pingamizi lao mahakama ina mamlaka kamili ya kufanyia kazi hoja ya kasoro ya hati ya mashtaka.
Hata hivyo, amesema kama Mahakama ikiona inafungwa mikono na kesi ya Faridi Hadi na wenzake kuliondoa shtaka la uhaini, basi ina mamlaka ya kuwashauri upande wa mashtaka waondoe hilo shtaka la kula njama au yote, kwa mujibu wa uamuzi wa kesi hiyo.
Hakimu Lyamuya baada ya kusikiliza hoja za pande zote, ameahirisha kesi hiyo mpaka Novemba 25, 2025 saa 5:00 asubuhi kwa ajili ya uamuzi.
Katika kesi hiyo uchunguzi wa awali (PI) namba 26388 ya mwaka 2025, shtaka la kwanza, washtakiwa hao (Niffer na wenzake) kwa nyakati tofauti kati ya Aprili Mosi na Oktoba 29, 2025 walikula njama za kutenda kosa la uhaini.
Katika shtaka la pili washtakiwa 21 wenzake na Niffer, Oktoba 29, 2025 katika maeneo mbalimbali wilayani Ubungo jijini Dar es Salaam wakiwa chini ya utii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitengeza nia kuzuia Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Wanadaiwa walitengeneza nia hiyo kwa lengo la kuitisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuithibitisha nia hiyo kwa kusababisha hasara kubwa kwa mali za Serikali zilizokusudiwa kutoa huduma muhimu.
Shtaka la tatu ambalo ni la uhaini linamkabili Niffer peke yake.
Anadaiwa kati ya Agosti Mosi na Oktoba 24, 2025, alionesha nia ya kutenda uhaini kwa kuwahamasisha umma kuzuia Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 na alithibitisha nia hiyo kwa kuwahamasisha watu kununua dukani kwake vifaa vya kujikinga na mabomu ya machozi.