Jaji Werema: Wananchi washirikishwe utungaji sheria

Mwanasheria Mkuu mstaafu wa Serikali, Jaji Frederick Werema
Muktasari:
Mwanasheria Mkuu mstaafu wa Serikali, Jaji Frederick Werema amesema kutoshirikishwa kwa wananchi katika utungaji wa sheria ndiyo chanzo cha wananchi kulalamikia sheria hizo.
Dar es Salaam. Mwanasheria Mkuu mstaafu wa Serikali, Jaji Frederick Werema amesema kutoshirikishwa kwa wananchi katika utungaji wa sheria ndiyo chanzo cha wananchi kulalamikia sheria hizo.
Werema ameishauri Serikali kabla ya sheria hazijatungwa na Bunge ni lazima ushirikishwaji ufanyike zaidi ya mara moja ili kuwapa fursa Watanzania watoe maoni yao kusaidia kuboresha na kujua wanachotaka.
Jaji Werema alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, baada ya kuwasilisha maoni yake kwenye kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa, alisema msingi wa hoja yake ni maridhiano yanapaswa kufanyika kwenye changamoto zote zinazolalamikiwa ili kujua Watanzania wanataka kuongozwa na Serikali yao kwa msingi upi.
“Nimezungumzia Sheria ya Uchaguzi na Vyama vya Siasa msingi ni hivi, utaratibu wa sasa ni ushirikishwaji kabla ya sheria haijatungwa na Bunge ushirikishwaji wake unapaswa kuwa dhahiri na thabiti, usiwe ushirikishwaji wa siku moja au mbili, lazima Watanzania washirikishwe na watoe maoni na kufanya hivyo wakati fulani lazima utapata maoni tofauti na kujua wao wanachotaka,” alisema.
Alisema si sheria zote zina upungufu ambazo watu wengi wamekuwa wakisema japo kweli kuna baadhi zina mapungufu lakini kuna nyingine ndivyo zilivyo na ikibainika changamoto hiyo zinatakiwa kufanyiwa masahihisho na kuboreshwa.
Alisema malalamiko yapo kwenye maeneo mengi, si kwenye sheria pekee isipokuwa maridhiano yanapaswa kufanyika katika mambo yote ya kitaifa ili maboresho yafanyike.
“Si kwenye sheria tu, bali kila jambo linalofanyika nchini linapaswa kuwa na maridhiano na si mtafaruku.”
Alisema hata wale wachache ambao mawazo yao hayachukuliwi wana haki ya kufikiriwa na wana haki ya kusema.
“Watu wa aina hiyo wana haki lakini wasitumie fursa hiyo kufanya fujo au kulazimisha mambo yao kutekelezwa... Kwa kawaida jambo linalozaliwa leo linakuwa kubwa linazeeka, linakwisha na linaanza jambo lingine, inawezekana jambo likakataliwa leo lakini kesho likawa jambo linalopigiwa upatu kwamba ni sahihi, kwa hiyo maridhiano ni jambo muhimu,” alisema Werema
Alisema suala la maridhiano halipaswi kuwa kauli ya Rais pekee, bali linapaswa kuhubiriwa na Watanzania wote na inapaswa kuwa ajenda ya kudumu hata kwa waandishi wa habari kwa sababu wana jukumu la kuhakikisha kunakuwa na utulivu katika Taifa.
Kuhusu Katiba mpya, Jaji huyo alisema mchakato ulioanza wa Jaji Warioba uendelezwe na ufikie mwisho, huku akieleza hatua zote zilifuatwa, ikiwemo kuchukua maoni ya wananchi.
“Kama kwenye Katiba mpya ni vizuri tukawa na maridhiano, japo kuna mgawanyiko, kuna wanaosema tuandike mpya wengine tufanyie mabadiliko na viraka kwenye hii iliyopo, hilo si suala, tunapoteza muda, kwa sababu suala la kuandika Katiba mpya lilishaamuliwa na mimi nafikiria lifanyike,” alisema Jaji Werema.
Naye Katibu Mkuu wa Tamisemi, Profesa Riziki Shemdoe alisema wao kama wadau muhimu, wanasimamia chaguzi za serikali za mitaa hadi vitongoji na waliowasilisha mawazo yao namna ya kuboresha chaguzi hizo kwa kuzingatia malalamiko yaliyojitokeza.
“Tamisemi tunawakilisha wananchi na tumetoa maoni yetu namna ya kuboresha, ikiwemo chaguzi hizo kurudi kwenye Tume huru ya Uchaguzi Ili isimamie, yaliyobaki ni ya kikosi kazi,” alisema.